Bangi na pombe London ni shauri ya upweke

Muktasari:

  • Kati ya mengi yanayoshangaza unapofika Ulaya mara ya kwanza ni ulevi na dawa za kulevya.

Kati ya mengi yanayoshangaza unapofika Ulaya mara ya kwanza ni ulevi na dawa za kulevya.

Sasa ukiwa mgeni umekuja zako kusoma au kutafuta uchumi...(ambao msemo wetu Wabongo majuu ni “kupiga boksi”) huoni sababu za kulewa au kuvuta misokoto ya kishetani. Ila wapo Waafrika wachache wanaozamia ndani ya usaha huu uvurugao roho na akili.

Kisa kikuu cha wenzetu weupe kuwa hivi (pamoja na weusi waliozaliwa huku), ni upweke.

Safu hii imezungumzia sana tofauti za kitamaduni na hali ya hewa unapotoka kwenu kwenda kwa wenzako.

Weupe wanao utamaduni wa “kila mtu na lake.” Mila na desturi za kutoingilia yasiyokuhusu. Ndiyo maana mtu anaweza kuwa jirani yako miaka kumi wala hamjuani. Baadhi yetu Waafrika hatuyazoei hata tulioishi huku miaka lukuki.

Utamaduni huu umetokana na uchumi wa kibepari. Uchumi unaokutaka mwanadamu kujituma, kutafuta riziki kwa kazi binafsi. Changanya hali ya hewa ya baridi ambayo imeanza kujongea Oktoba hii.

Ukitilia haya maanani utaelewa kwa nini wenzetu huwa vile.

Tupo pia Wamatumbi toka nchi zenye tafrani. Tuliokuja si kupiga boksi, bali kuomba hifadhi au ukimbizi.

Tunawaona wenyeji wakimaliza kazi Ijumaa wanamiminika katika mabaa kulewa. Hilo ni zito jamaa zangu. Wenyeji huenda baa kulewa, sio kuburudika. Kwa Kiingereza yaitwa “binge” (tamka binji).

Ukijumuika nao kustarehe utashangaa unavyomiminiwa mtungi. Utamaduni si wa kula kwanza. Hunywa hivyo hivyo na njaa na matokeo ni kutapika tapika kishenzi baadaye.

Ndiyo hutokea labda mkienda kula kwanza ila siyo kanuni. Na si nchi zote za Kizungu ziko hivyo. Ukitua Ufaransa, Italia , Hispania, Urusi au Ugiriki, wana utamaduni wa kushindilia msosi mzito, kwanza.

Jumamosi iliyopita nilikuwa mitaani na washikaji wenzangu. Kuna jamaa katoka nchi moja ya Kiafrika yenye tafrani na ugaidi, huranda randa sana nje ya klabu tuliyotembelea.

Tukamzungumzia.

“Huyu msela alikuwa safi kabisa miaka mitano iliyopita. Leo anaokota okota vyakula mapipani. Hafanyi kazi. Hana ndugu wala rafiki. Kisa nini?”

Tukamdadavua.

Mmoja wetu: “Alipomaliza kusoma alikuwa akifuatana sana na hawa wenyeji. Wakitoka kulewa na huko mlikuwa pia bangi kwa jam. Kaingilia bangi kwa pupa. Sasa bangi aliyokuwa akivuta marehemu Bob Marley na marasta wa zamani si bangi ya siku hizi. Siku hizi bangi imewekwa vidude chungu nzima. Keshakuwa chizi. Halafu hizi dawa za kulevya hazitaki pupa. Wenzetu weupe wana fedha. Nchi yao hii. Ukikutana naye mitaani kalewa chakari amevaa viraka viraka sasa nenda kwake. Utashangaa katokea familia nzuri. Nyumba ina kila aina ya ahueni. Ile lewa lewa mitaani ni jambo la muda tu, kutafuta utofauti! Mwenzetu katokea kwenye vurugu mechi za fisi na kuuana uana, akaparamia ushetani. Wenzetu wako tofauti. Akifanya kazi, hela yote ni yake mwenyewe. Wazazi wake wako vizuri hawahitaji hata senti yake moja. Sisi ukipata mshahara inakubidi ugawane na familia kumi kwenu Umatumbini. Sasa jamaa kaparamia visivyo vyake muone.”

Na kweli jamaa anazungumza peke yake. Omba omba. Hajui tena cha msikitini, hafahamu kuoga, kula ugali kwa nyama na kachumbari. Bangi kwa maskini ni wazimu.