Biashara ya nyama yadoda Ijumaa Kuu Mwanza

Muktasari:

 Baadhi ya wafanyabiashara Mwanza wamepunguza kilo za nyama kutoka machinjioni wakihofia hasara

Mwanza. Wakati wakristo wakianza sikukuu ya Pasaka kwa kusherehekea ‘Ijumaa Kuu’, wafanyabiashara  wa nyama jijini Mwanza wamesema biashara ya kitoweo hicho imedorora huku wengine wakihofia kupata hasara.

Ijumaa ya mwisho wa juma kabla ya Pasaka hutumiwa na wakristo kuabudu huku wakitakiwa kutokula kitoweo chenye damu ikiwa ni kutimiza takwa la kiimani katika baadhi ya madhehebu ya kikristo duniani.

Akizungumza na Mwananchi leo, Ijumaa Machi 29, 2024, muuzaji nyama eneo la Buhongwa jijini Mwanza, Alphonce Fortunatus amesema kutokana na mwenendo kuonyesha kuwapo idadi ndogo ya wateja amelazimika kupunguza kiasi cha nyama anayochukua machinjioni kutoka kilo 1,000 hadi 500.

Fortunatus amesema pamoja na kupunguza kiwango cha nyama anayoagiza hadi kilo 500 bado hajauza hata nusu ya kiasi hicho huku akihofia huenda nyama hiyo isimalizike leo na kuingia kwenye hatari ya kuharibika.

“Siku za kawaida saa 3 asubuhi ingekuwa nimeshauza angalau kilo 300 za nyama kwa sababu eneo hili kuna msongamano mkubwa wa watu lakini hadi sasa nimeshauza kilo 50 tu. Ninawasiwasi nyama inaweza kulala nikalazimika kuiuza kesho au kupata hasara kabisa,” amesema Fortunatus.

Mfanyabiashara mwingine, Emmanuel Nyamoyo amesema kwa kutambua uwepo wa Ijumaa Kuu amelazimika kutoagiza nyama kutoka machinjioni kwa hofu ya kukosa wateja huku akifungua bucha yake ili kumalizia kilo 15 zilizosalia jana.

“Kwa kawaida siku ya Ijumaa Kuu kwa miaka iliyopita tilikuwa hatufungua bucha kabisa, huu mwaka ni mara ya kwanza tumefanya hivi kwa kwa sababu tulibakiza nyama ya jana. Lakini binafsi leo sijaleta nyama kabisa kwa sababu hamna walaji,” amesema Nyamoyo.

Mkazi wa Mkolani jijini Mwanza, Esther Mwita ambaye ni muumini wa Kanisa Katoliki (RC) amesema baada ya kuamka alfajiri ya leo amehudhuria ibada kanisani huku mafundisho aliyosisitizwa ni pamoja na kusisitizwa kutokula nyama hadi kesho.

“Tumekuwa tukifuata misingi ya kiroho na kiimani, kwa sababu ni kumbukizi mbaya kwetu wakristo kwamba mwokozi wetu alisurubiwa na kuteswa msalabani. Akamwaga damu nyingi, hatupaswi kumuenzi kwa maumivu tena,” amesema Esther.

Kwa nini wakristo hawali nyama leo?

Miongoni mwa maswali yaliyoko vichwani mwa wengi, ni kwa nini wakristo hawali nyama siku ya Ijumaa Kuu.

Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Yohanne Mtume wa Mwinjilisti jijini Dar es Salaam, Padri Revocatus Paul amesema Ijumaa Kuu ni siku ambayo Yesu Kristo alikufa msalabani, inatumiwa na waumini kutafakari wokovu uliokuja kwa njia ya msalaba.

Padri Revocatus amesema katika siku hii wakristo hawatakiwi kufanya shamrashamra kwa kile alichotaja kuwa ni siku ya maombolezo ya kifo cha cha Yesu Kristo hivyo hawatakiwi kula nyama kwa kile kinachoelezwa nyama ni ishara ya sherehe.

“Tunakuwa katika maombolezo na kutafakari ndiyo maana hatutakiwi kula nyama kwa sababu nyama ni ishara ya sherehe, na ndiyo suala ambalo waumini wanatakiwa walizingatie tunatakiwa kukaa kimya na kusali njia ya msalaba. Huo ni utaratibu wa kanisa ulimwenguni, sikukuu ya pasaka,” amesema Padri Revocatus.

Akizungumzia kubadilika kwa tarehe ya Pasaka mwaka hadi mwaka, padri Revocatus amesema Biblia inaonesha  ni mapokeo ya enzi na enzi kwa kuwa walitegemea mapokeo ya upevu wa mwezi kuanzia mwezi kuwa nusu (tarehe mosi) na mwezi mpevu kamili (tarehe 15).

“Katika mahesabu hayo ya mwezi kuizunguka dunia kuna calculations (hesabu) zipo kwa hiyo kwenye hesabu hizo watalaamu wanapiga hesabu na kufahamu Pasaka itakuwa siku ipi. Ningewaonyesha lakini hayo mahesabu yanahitaji mzunguko mrefu mno,” amesema.

Amewaonya waumini wanaotumia Sikukuu ya Pasaka kutenda matendo yasiyofaa ukiwamo ulevi, uzinzi na kusherehekea katika namna isiyofaa huku akiwataka kuitumia kufanya takafuri ya kiimani ya kumrudia Mungu.