Biteko afuta likizo kwa watumishi wote Tanesco

Naibu Waziri Mkuu, Dk Doto Biteko akisikiliza maelezo ya hali ya maji kwenye bwawa la kuzalisha umeme la Kidatu leo Februari 23, 2024 kutoka kwa Meneja wa Kituo cha Kuzalisha Umeme Kidatu, Mhandisi Manfred Mbyallu (katikati). Kulia ni Waziri wa Maji, Jumaa Aweso. Picha Hamida Shariff

Muktasari:

  •  Waziri wa Nishati Dk Doto Biteko ametoa maelekezo hayo leo Februari 23, 2024 alipotembelea Bwawa la Kidatu Morogoro na kubaini meneja wa Tanesco katika mkoa huo yupo likizo

Dar es Salaam. Naibu Waziri Mkuu, Dk Doto Biteko, ameagiza kusitishwa likizo zote za wafanyakazi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) hadi pale tatizo la mgawo wa umeme litakapotatuliwa.

Dk Biteko ambaye pia ni Waziri wa Nishati ametoa maelekezo hayo leo Februari 23, 2024 alipotembelea Bwawa la Kidatu mkoani Morogoro na kubaini meneja wa Tanesco katika mkoa huo yupo likizo.

Mbali na hilo, ameagiza kupatiwa maelezo ya aliyetoa kibali cha likizo kwa meneja huyo na sababu za yeye kwenda likizo wakati kukiwa na changamoto ya mgawo wa umeme.

“Nimeshangaa kukuta meneja wetu wa mkoa ameenda likizo katikati ya changamoto hii, nitoe wito kwa menejimenti ya Tanesco kuwa hakuna likizo tena kwa mtu yeyote anayefanya kazi Tanesco. Niliposema Tanesco hamtolala wakati huu wa mgawo nilimaanisha watu wote tuwe kazini, sisi wenyewe tunazunguka kila mahali kuhakikisha wananchi wanapata umeme, haiwezekani wengine wanapata likizo na kwenda mapumziko,” amesema.

Dk Biteko amesema, “nimemuelekeza kamishna wa nishati nataka kujua ni nani ametoa kibali cha likizo katika kipindi hiki na tujue hata huyo aliyepewa ruhusa ametoa wapi ujasiri wa kuomba likizo katika kipindi hiki kigumu. Kwa hiyo tutachukua hatua za ndani kuhakikisha kila mmoja anatekeleza wajibu wake.”

Amewasihi Watanzania kuendelea kuwa watulivu kwa kuwa Serikali imefikia hatua za mwisho kuhakikisha umeme wa uhakika unapatikana nchini.

“Serikali inaendelea kufanya jitihada mbalimbali kushughulikia tatizo la umeme, niwaeleze wananchi kuwa changamoto tuliyonayo ya umeme iko mwishoni. Niwasihi Watanzania kuwa hatua tuliyofikia ni ya mwishoni, tutaanza kuondoa mgawo muda wowote kuanzia sasa kwa sababu tumeshafika hatua nzuri maji mnayaona yapo,” amesema.

Dk Biteko amesema, “habari njema ni kwamba, Rais Samia Suluhu Hassan ameshatoa kila aina ya rasilimali inayohitajika kwa ajili ya kuwapatia umeme. Hatuwezi kugeuka kuwa kikwazo cha kumrudisha nyuma. Tumekuja na Waziri wa Maji, lengo ni kuwa na juhudi za pamoja kulinda hivi vyanzo, tukitoka hapa tunakwenda kutengeneza timu ya pamoja ya Serikali itakayohakikisha vyanzo vyote vinavyotuletea umeme vinalindwa kwa gharama yoyote.”

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amewataka watendaji wa sekta hizo mbili kuacha visingizio hasa pale wanaposhindwa kutoa huduma bora kwa wananchi.

"Tushirikiane kutunza vyanzo vya maji kupitia mabonde yetu tisa tuliyonayo, utunzaji wa vyanzo hivi ni jambo shirikishi," amesema Aweso.

Pia, amewataka maofisa wa mabonde hayo kuacha tabia ya kukaa ofisini, akisema haiwezekani ofisa akae ofisini anachezea kompyuta mwaka mzima.

Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga akijibu swali la nyongeza la mbunge wa Lupembe, Edwin Swalle bungeni hivi karibuni alisema mgawo utaisha Machi baada majaribio ya mtambo namba tisa wa uzalishaji wa umeme kwenye Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP) kufanikiwa.

Kapinga alisema mtambo namba tisa utazalisha megawati 235 na namba nane utakaoanza uzalishaji Machi, mwaka huu utazalisha megawati 235.

“Kwa kweli mgawo utakuwa umepungua kwa kiasi kikubwa, lakini kwa sababu mtambo wa namba tisa utazalisha megawati 235 na namba nane utakaoanza uzalishaji Machi utazalisha megawati 235, jumla zitakuwa megawati 470. Uhakika ni kwamba kufikia Machi, mgawo wote utakuwa umeisha,” alisema

Februari mosi, mwaka huu, akijibu maswali ya wabunge Kapinga aliwataka wavumilie hadi Februari 16, akisema zitapatikana megawati 215 zitakazomaliza tatizo hilo.

“Kwa hiyo tunaendelea kuwaomba ifikapo tarehe 16 Februari tutakuwa tumekamilisha majaribio kwenye bwawa la Mwalimu Nyerere. Tunategemea megawati za mwanzo 215 tutaanza kuzipata, kwa hiyo tumebakisha muda mchache kulinganisha na kule tulikotokea, tunaomba muendelee kutuvumilia ili tukamilishe zoezi hili mpate umeme wa uhakika,” alisema Kapinga akijibu swali la mbunge wa Viti Maalumu, Stella Fiyao.

Septemba 25, 2023, Rais Samia Suluhu Hassan alimpa miezi sita bosi mpya wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Gissima Nyamo-Hanga kuhakikisha umeme wa uhakika unapatikana nchini. Muda huo utafikia tamati Machi 25, 2024.

Septemba 28, 2023, Nyamo-Hanga alisema changamoto ya umeme inayoendelea nchini hadi kufikia Machi mwaka huu itakuwa imekwisha.

Februari 6, 2024, Bunge liliazimia Serikali ihakikishe mradi wa JNHPP unakamilika haraka na kuanza uzalishaji kuanzia Februari 2024 kama ilivyoahidi.