Wananchi wataka ratiba, mikakati kukabiliana na mgawo wa umeme

Muktasari:

  • Wakati kelele za kukatika kwa umeme zikiendelea kusikika kila kona na matamko mbalimbali juu ya ushughulikiwaji wa tatizo hilo yakiendelea kutolewa, wananchi wataka ratiba ya mgawo huo.

Dar es Salaam. Wananchi wametaka kutolewa kwa ratiba ya kukatika kwa umeme katika maeneo yao ili kuwawezesha kupanga ratiba na kutosimamisha shughuli zao za uzalishaji.

Pia, wametaka kuwapo kwa mikakati ya kumaliza tatizo hilo la mgawo wa umeme kwa sababu ni changamoto iliyokuwa kwa muda mrefu.

Wametoa maoni hayo usiku wa leo Jumatano, Februari 21, 2024 wakati wakizungumza katika Mwananchi X Space iliyoandaliwa na Mwananchi Communications Limited (MCL), ikijadili mada isemayo ‘changamoto ya upungufu wa umeme nchini na mikakati ya Serikali kuimaliza’.

Akichangia mada katika mjadala huo, Mjasiriamali wa kuoka keki, Grlorie Mahecha amesema kujua ratiba mapema kuhusu upatikanaji wa umeme ungewasaidia kujipanga katika utekelezaji wa shughuli zao.

Amesema hilo  litasaidia mteja anapotoa oda yake inakuwa ni rahisi kujua wakati gani wa kuzalisha ili kuepuka hasara.

“Utakuta unachukua zabuni ya mtu ya kutengeneza keki lakini unafanya kwa hisia hujui umeme utakatika saa ngapi, ikitokea umekatika unalazimika kurejesha fedha, wakati umeshanunua vifaa mwisho wa siku unapata hasara,” amesema Mahecha.

Kauli hizi pia zinatolewa wakati ambao vilio vya kukatika kwa umeme vimeendelea kusikika kila kona, huku baadhi ya wafanyabiashara wadogo wakiendelea kulia hasara ya kuharibika kwa bidhaa zao.

Alichokisema Mahecha kiliungwa mkono na Mhariri wa Takwimu wa Mwananchi, Halili Letea ambaye amesema tatizo sio mgawo, bali taarifa sahihi za kukatika kwa umeme ili mtu ajipange vizuri katika shughuli zake.

 Amesema umeme ndio msingi wa uchumi katika Taifa lolote duniani. “Uimara wa uchumi wa nchi yoyote duniani unahitaji upatikanaji wa umeme wa uhakika.”

“Kwa siku za hivi karibuni kumekuwa na changamoto kubwa ya upatikanaji wa umeme katika maeneo mbalimbali hali inayoathiri shughuli za kiuchumi, hasa kwa wafanyabiashara wanaotegemea nishati hiyo kwa kiwango kikubwa kuendesha biashara zao,” amesema Letea.

Amesema hata mwekezaji yeyote anayekuja lazima aangalie upatikanaji wa uhakika wa nishati hiyo na kwa wananchi wa kawaida wanaoendesha biashara kama saluni, watengenezaji wa juisi ndio waathirika wakubwa wa changamoto hii.

Mwananchi mwingine, Makene Naluyanga amesema Serikali iwekeze kwenye wataalamu wa umeme ambao watafanya makadirio sahihi ya mahitaji, matumizi ya nishati hiyo kwa miaka 100 ijayo.

“Tunakwenda kupata mafanikio kwenye upatikanaji wa nishati hiyo, jambo la kwanza ni tuwekeze kwa wataalamu watakaojua hapa tulipo mpango wetu upoje kwa miaka 100,” amesema.

 Amesema kama nchi inatakiwa kupanga mkakati wa muda mrefu wa kuhakikisha matumizi yakizidi, basi uzalishaji utakuwa kwa kiwango hicho huku akipendekeza wataalamu wa kutosha wapatikane ili kuwe na makisio na tathimini za siku nyingi zijazo.

Naye Mkurugenzi wa Chama cha Walaji Tanzania, Bernard Kihiyo amesema kukatika kwa umeme limekuwa jambo endelevu kuanzia utawala wa awamu ya tatu.   

 “Hili tatizo kwa ujumla wake linatia kichefuchefu, halipendezi kwa sababu ya madhara yake, kila Rais aliyepita amejaribu kukabiliana nalo. Kama bwawa (Julius Nyerere) limejaa kwa nini huo umeme usipatikane?”

“Tatizo hatuna vipaumbele vya kutatua tatizo, hili ndilo jambo linalotuingiza hasara, sasa maisha ni magumu, chanzo kinachoweza kukupa kipato hakipo, kila siku unaambiwa kesho, mwarobaini unakuja, umepatikana lakini hakuna linaloeleweka,” amesema Kihiyo.

Mkazi wa Mwanza, Peter Saramba amesema wananchi wanataka umeme wa uhakika na si vinginevyo.

Amesema madhara ya kukatika kwa umeme yapo katika nyanja zote za maisha, kuanzia kiuchumi, kiusalama, upatikanaji wa maji na huduma za afya.

“Shughuli zote za kiuchumi zinakwama umeme unapokosekana, ninachotaka kusema Watanzania tunahitaji umeme kutoka Tanesco, unapatikanaje au kwa njia gani hilo sio tatizo letu wananchi, bali tunahitaji umeme," amesema Saramba na kuongeza;

“Jinsi tulivyo Watanzania ni kama vile watoto ndani ya familia ambao wakimuona baba au mama wanachohitaji ni chakula na mahitaji ya shule. Ili tupate umeme lazima tuwe na mikakati na mipango endelevu ya upatikanaji wa nishati hii muda mfupi, wa kati na mrefu, lazima tuweke kwenye uzalishaji na usambazaji,” amesema Saramba.


Kauli ya Tanesco

Akijibu hoja hizo, Msemaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Kenneth Boymanda amesema hali ya upatikanaji wa umeme inalinganishwa na uzalishaji pamoja mahitaji ya watumiaji wa nishati hiyo.

Amesema mahitaji ya umeme ndani ya nchi yanakua, kwa sasa yamefikia megawati 1,660 akisema mahitaji hayo ni makubwa katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2019/24.

Boymanda ametaja sababu mbalimbali zilizochangia mahitaji ya umeme kuwa juu ni pamoja ongezeko la wateja wanaounganishwa na huduma hiyo, matumizi ya nishati safi ya kupikia, mabadiliko ya tabianchi (ongezeko la joto watu kununua vipozeo), wingi wa viwanda kutokana na sera za uwekezaji za Serikali.

“Sasa haya yote ndio yanatuleta mahitaji makubwa ya umeme, lakini ya uzalishaji wa umeme umekuwa ukibadilika kutokana na vyanzo vya uzalishaji hususani mitambo ya kufua umeme kwa kutumia maji au gesi,” amesema Boymanda.

Boymanda amesema ndani ya muda mfupi vinu vitatu vya kuzalisha umeme vilivyopo katika Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere, vitazalisha umeme wa megawati 705, hatua itakayowezesha kuondokana na changamoto ya upungufu wa umeme uliopo.

“Changamoto iliyopo tutaipungia mkono wa kwaheri, tumekaribia kumaliza tatizo hili,” amesema.