VIDEO: Serikali yatoa ahadi mpya, mgawo wa umeme kuisha Machi

Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga akizungumza wakati akijibu swali la nyongeza la mbunge wa Lupembe (CCM), Edwin Swalle leo Ijumaa, Februari 16, 2024. Picha na Merciful Munuo

Muktasari:

  • Serikali imesema imekamilisha majaribio ya mtambo namba 9 wa kuzalisha umeme utakaozalisha megawati 215, hivyo kumaliza tatizo la mgawo wa umeme ifikapo Machi, 2024

Dar/Dom. Serikali imeendelea kupiga kalenda suala la kumalizwa kwa kero ya mgawo wa umeme, ikisema tatizo hilo sasa litakwisha ifikapo Machi, 2024.

 Akijibu maswali ya wabunge, Februari mosi, Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga aliwataka wavumilie hadi Februari 16, akisema zitapatikana megawati 215 zitakazomaliza tatizo hilo.

“Kwa hiyo tunaendelea kuwaomba ifikapo tarehe 16 Februari mwezi ujao tutakuwa tumekamilisha majaribio kwenye bwawa la Mwalimu Nyerere (JNHPP).

“Tunategemea Megawati za mwanzo 215 tutaanza kuzipata, kwa hiyo tumebakisha muda mchache kulinganisha na kule tulikotokea, tunaomba mwendelee kutuvumilia, ili tukamilishe zoezi hili mpate umeme wa uhakika,” alisema Kapinga akijibu swali la mbunge wa Viti Maalumu, Stella Fiyao.

Hata hivyo, leo Februari 16, 2024, Kapinga akibu swali la nyongeza la mbunge wa Lupembe (CCM) Edwini Swalle, amesema mgawo utaisha ifikapo Machi, 2024 baada majaribio ya mtambo namba 9 wa uzalishaji wa umeme kwenye Bwawa la Mwalimu Nyerere kufanikiwa jana.

“Naomba nilifahamisha Bunge lako tukufu kwamba, jana tumefanikiwa kufanya majaribio kwa ukamilifu kwa mtambo kwa uwezo wake wa mwisho yaanni megawati 235.

“Kama ambavyo tulisema ratiba ya awali yatakamilika tarehe 16 kwa siku ya jana tumefanmikisha majaribio hayo kwa kiasi kikubwa sana. Kwa sasa hivi wataalamu wetu wanaendelea na fine tuning na kuweka ulinzi wa mitambo kwa ajili ya kwenda kwenye uzalishaji,” amesema.

Mgao wa umeme kuisha Machi

Hata hivyo, Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson, naye amehoji mgawo wa umeme utaisha lini?

Akijibu swali hilo, Kapinga amesema mgawo wa umeme unategemeana na matumizi ya kila siku ya nishati hiyo nchini.

Amesema mtambo namba 9 utazalisha megawati 235 na mtambo namba 8 utakaoanza uzalishaji wake Machi mwaka huu utazalisha megawati 235.

“Kwa kweli mgawo utakuwa umepungua kwa kiasi kikubwa, lakini kwa sababu mtambo wa namba tisa utazalisha megawati 235 na namba nane utakaoanza uzalishaji Machi utazalisha megawati 235, jumla zitakuwa megawati 470. Uhakika ni kwamba kufikia Machi, mgawo wote utakuwa umeisha,” amesema.

Kauli hiyo ilimuibua tena Dk Tulia aliyesema Serikali awali ilitangaza kuwa mgawo ungemalizika Juni mwaka huu, lakini baadaye walirudisha nyuma hadi Machi, 2024.

Baada ya maelezo hayo, Spika wa Bunge ameipa Serikali hadi Juni, 2024 ili kusiwe tena na mgawo wa umeme kama alivyoahidi Naibu Waziri, Kapinga.


Mgawo ulivyoanza

Mgawo wa umeme nchini Tanzania ulianza Septemba, 2023 kutokana na upungufu kwa uwezo wa uzalishaji wa umeme kutoka kwenye vyanzo mbalimbali ikiwemo vya maji.

Septemba 25, 2023, Rais Samia Suluhu Hassan alimpa miezi sita bosi mpya wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), GIssima Nyamo-Hanga kuhakikisha umeme wa uhakika unapatikana nchini.

Miezi sita aliyopewa na Rais Samia kuhakikisha mgawo wa umeme nchini inakwisha Machi 25, 2024.

Septemba 28, 2023, Nyamo-Hanga amesema changamoto ya umeme inayoendelea nchini hadi kufikia Machi mwaka huu itakuwa imekwisha.

Februari 6, 2024, Bunge liliazimia Serikali ihakikishe mradi wa JNHPP unakamilika haraka na kuanza uzalishaji kuanzia Februari 2024 kama ilivyoahidi.

Hata hivyo, kuanzia jana usiku, kipeperushi kilichoandikwa mtuvumilie mgawo kumalizika Februari 16 kilikuwa kikitembea katika mitandao ya kijamii na kuibua mjadala.