‘Biti’ la Mbarawa kwa mkandarasi
Muktasari:
- Mradi wa maboresho wa bandari za Kemondo na Bukoba mkoani Kagera wafikia asilimia 25, waziri Mbarawa aagiza ukimilike Mei mwaka 2024.
Dar es Salaam. Waziri wa Uchukuzi Profesa, Makame Mbarawa amtaka mkandarasi mradi wa maboresho ya bandari za Kemondo na Bukoba mkoani Kagera, kukamilisha Mei mwakani, na hivyo kurahisisha shughuli za uchukuzi katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Bandari hizo ni miongoni mwa miradi ambayo Novemba 9 mwaka huu, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo, wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Paul Makonda, aliitolea maelekezo wakati wa ziara yake mkoani Kagera, huku akimuagiza Mbarawa kuhakikisha anaifuatilia kwa ukaribu.
Taarifa iliyotolewa leo Jumamosi Novemba 25, 2023 na Wizara ya Uchukuzi, imeeleza kuwa waziri huyo ametembelea miradi hiyo na kumtaka mandarasi wa Kampuni ya China Railway Major Bridge Enginnering Limited (CRMBEG) kukamilisha kazi hiyo kwa wakati.
Akizungumza mara baada ya kukagua miradi hiyo Profesa Mbarawa amesema kukamilika kwa miradi hiyo kutarahisisha shughuli za uchukuzi baina ya bandari hiyo, mikoa ya Kanda ya Ziwa na nchi jirani zinazunguka mikoa hiyo.
“Nawapongeza kwa hatua iliyofikiwa lakini niwakumbushe kuwa ujenzi wa meli ya MV. Mwanza uko katika hatua mbalimbali za kukamilishwa na itakapokamilika itatumia bandari hizi mbili kutoa huduma. Lazima tuongeze kasi ya ujenzi hususani kwenye gati angalau moja kwa kila bandari ili kuruhusu meli yetu ya MV Mwanza kutoa huduma," amesema Waziri Mbarawa.
Mbali na hilo Profesa Mbarawa ameitaka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) pamoja na maboresho ya bandari hizo, kuhakikisha Ziwa Victoria linafungiwa vifaa maalumu vya kuongozea meli, ili kuziwezesha kutoa huduma katika hali ya usalama.
Mkuu wa Wilaya ya Misenyi, mkoani Kagera, Kanali Wilson Sakulo amesema mradi huo ukikamilika utachochea ukuaji wa biashara kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Mhandisi Mkazi wa Kampuni ya Dar Al Handah Consultants, Joshua Lesha amemuhakikishia Profesa Mbarawa kuwa kasi itaongezwa katika utekelezaji wa miradi hiyo miwili kwa kuwa sehemu kubwa ya vifaa vya ujenzi, vipo kwenye eneo la mradi.
Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Juma Kijavara amesema miradi inayohusisha maboresho ya bandari ya Kemondo na Bukoba imefikia asilimia 25 na kwamba taasisi hiyo itahakikisha inamsimamia mkandarasi ili aikamilishe kwa wakati.