CCM yapangua safu kimyakimya

Naibu Katibu Mkuu wa CCM-Bara, Rodrick Mpogolo

Muktasari:

  • Katika kinachoonekana kama mpango wa maandalizi ya uchaguzi mkuu na chaguzi za Serikali za Mitaa, Chama cha Mapinduzi (CCM) kimeanza kupangua safu za uongozi kwa kuwagusa makatibu wake wa wilaya na mikoa huku baadhi yao wakirudishwa makao makuu.

Dar/mikoani. Ikiwa imesalia miezi 23 kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu, Chama cha Mapinduzi (CCM) kimeanza kusuka upya safu ya uongozi kimyakimya kwa kuwapangua na kuwaweka kando baadhi ya makatibu wake wa mikoa na wilaya.

Pia, mabadiliko hayo yanafanyika ikiwa imebakia miezi takribani 10 kabla ya kufanyika kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Makatibu hao wa Tanzania bara, waliotangazwa Machi 27 mwaka jana na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole baadhi yao wamerejeshwa makao makuu ya chama hicho.

Kati ya makatibu 31 wa mikoa walioteuliwa wakati huo, kumi na moja walipandishwa kutokana na utendaji wao na 20 walikuwa wapya huku Polepole akisema sifa zilizotumika kuwapata ni maadili, weledi, jinsia na mpango wa kuachiana vijiti kwa kuzingatia rika.

Jana, Naibu Katibu Mkuu wa CCM-Bara, Rodrick Mpogolo alipoulizwa na Mwananchi kuhusu mabadiliko hayo alisema, “Kilichofanyika ni mabadiliko ndani ya chama sioni kama ni mambo ya magazeti.”

Hata hivyo, msemaji wa chama hicho visiwani Zanzibar, Catherine Peter Nao alisema hadi jana hakukuwa na mabadiliko yoyote ambayo wameyapokea kutoka makao makuu. “Lakini tunafahamu kwamba chama chetu kina nia ya kufanya mabadiliko hayo.

Katika mabadiliko hayo, aliyekuwa kaimu katibu mkuu wa UVCCM, Shaka Hamidu Shaka amepelekwa kuwa katibu wa chama hicho Mkoa wa Morogoro kuchukua nafasi ya Kulwa Milonge ambaye sasa ni msimamuzi wa ujenzi wa chuo cha diplomasia, itikadi, uzalendo na uadilifu cha CCM mkoani Pwani.

Kabla ya Miloge kupelekwa chuoni hapo, alirejeshwa makao makuu na nafasi yake kukaimiwa na Allan Kingazi aliyetokea Tanga.

Milonge alisema anaamini kuwa uhamisho wake ni wa kawaida.

Nafasi ya Kingazi mkoani Tanga ilichukuliwa na Shaibu Akwilombe ambaye aliripoti Agosti 10. Akwilombe alisema jana kwamba hakukuwa na mabadiliko wilayani.

Elias Mpanda aliyekuwa Arusha, amehamishiwa mkoani Mara na nafasi yake imejazwa na aliyekuwa katibu wa CCM Wilaya Arusha, Musa Matoroka. Mwenyekiti wa CCM mkoani Arusha, Loota Sanare alisema hadi jana alikuwa hana taarifa za mabadiliko mengine baada ya Mpanda kuhamishwa.

Katibu wa CCM Mkoa wa Manyara, Pazza Mwamlima amehamishwa mkoani Njombe kuchukua nafasi ya Hossea Mpagike.

Katibu wa siasa na uenezi Mkoa wa Manyara, Pasian Siay alisema baada ya Mwamlima kuhamishiwa Njombe, Naomi Kapambala aliyetokea mkoani Kigoma amemrithi.

Aliyechukua nafasi ya Kapambala ni Dastan Shayo aliyetoka makao makuu ya chama hicho.

Mabadiliko hayo yameikumba Wilaya ya Kibondo. Katibu wake, Salome Luhingulanya amehamishiwa Wilaya ya Tabora.

Clemence Mkondya ameteuliwa kuwa katibu wa CCM Mkoa wa Mwanza kujaza nafasi ya Raymond Mangwala aliyeteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa UVCCM.

Wilayani Biharamulo, Kagera, katibu wa wilaya hiyo, Joyce Massi alistaafu na nafasi yake kuchukuliwa na Hassan Millanga aliyewahi kuwa diwani wa Muleba.

Wilayani Ngara, aliyekuwa katibu wa wilaya hiyo, Jacob Makune uteuzi wake ulitenguliwa na nafasi yake kuchukuliwa na Mwajemi Balagama.

Mhadhiri mwandamizi wa Sayansi ya Siasa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Benson Bana akizungumzia mabadiliko hayo alisema chama hicho kipo huru kufanya mabadiliko ya viongozi wake kwa kadri inavyoona inafaa lakini si vibaya kikatoa taarifa kwa umma.

“Wanaruhusiwa kubadilisha viongozi wao kulingana na mikakati yao ya ndani waliyonayo. Hata hivyo, chama kama CCM kikifanya mabadiliko kama hayo hakuna ubaya kikautangazia umma,” alisema Dk Bana.