Corona chanzo RwandaAir kusitisha safari zake Uganda

Friday June 11 2021
rwanda safari pic
By Mariam Mbwana

Dar es Salaam. Shirika la ndege la Rwanda limetangaza kusitisha safari zake za ndege kwenda nchini Uganda.

 Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na shirika hilo leo Ijumaa Juni 11, 2021 inaeleza kuwa uamuzi huo unatokana na kuongezeka kwa maambukizi ya ugonjwa wa Covid -19 unaosababishwa na virusi vya corona.

“Kutokana na kuongezeka kwa visa vya Covid-19 nchini Uganda, RwandAir inatangaza kusitishwa kwa safari zake za ndege za kuelekea na kutoka Entebbe kuanzia Juni 10,  2021  hadi tangazo lingine litakapotolewa,” inaeleza taarifa hiyo na kuwaomba radhi abiria kwa usumbufu uliosababishwa na hatua hiyo.

rwanda safari pic 2

Shirika hilo limesema abiria walioathiriwa na  kusitishwa kwa safari hizo wanaweza kupanga upya safari na kusafiri baadaye safari hizo zitakaporejeshwa tena sambamba na kuwarejeshea fedha waliokata tiketi.

“Uganda imepata ongezeko kubwa la idadi ya watu walioambukizwa virusi vya corona, jambo lililowalazimisha maofisa wa nchi hiyo kuweka sheria inayowataka watu kupunguza shughuli na matembezi yasiyo ya lazima kwa muda wa wiki sita,” inaeleza taarifa hiyo.

Advertisement
Advertisement