Dk Mwinyi: Nandy festival kukuza utalii Z'bar

Dk Mwinyi: Nandy festival kukuza utalii Z'bar

Muktasari:

  • Tamasha la Nandy festival lilianza mwaka 2019 na wasanii wametembelea mikoa ya Kigoma, Mwanza, Dodoma na Arusha lengo ni kusaidia vijana kupata ajira na kukuza muziki wa kizazi kipya barani Afrika

Unguja. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi amesema tamasha la Nandy festival kufanyika visiwani humo ni fursa ya kuutangaza utalii.


DK Mwinyi ametoa kauli hiyo leo Alhamis Julai 22, 2020 Ikulu jijini Zanzibar wakati akizungumza na wasanii wa tamasha hilo wakiongozwa na mwanamziki wa kizazi kipya Faustina Mfinanga maarufu Nandy.


Amepongeza utayari wa wasanii hao kwenda Zanzibar kufanya maonyesho akisema ni faraja maana yataendelea kuitangaza Zanzibar kitaifa na kimataifa.


“Matamasha yana umuhimu mkubwa sana kwasababu yanaleta watu kutoka nje na muziki wa kizazi kipya nao unaweza kuleta watu wengi hapa nchini kutoka ndani na nje ya Tanzania, nimefarijika sana na tamasha lenu,” amesema.

Kuhusu muziki wa taarab, Dk Mwinyi amesema:"Hiyo Zanzibar ni nyumbani hivyo ni vyema hatua za makusudi zikachukuliwa katika kuuinua maana siku za nyuma uliimarika zaidi na palikuwapo hata  mashindano yake yaliyohusisha nchi za ukanda wa Afrika Mashariki. Hatua hiyo  ilikuwa inanyanyua vipaji vya wasanii wa ndani na kuleta hamasa na kukuza utalii.”

Amesema sanaa ni njia moja wapo ya kutoa ajira kwa vijana na iwapo wasanii hao watasaidiana na wasanii wa Zanzibar hatua hiyo itasaidia kuwapa ajira vijana.

Amesema Serikali anayoiongoza itatumia njia ya kuwasaidia wasanii wa ndani ili waweze kuinua vipaji vyao maana sanaa mbali nakutoa burudani lakini inatoa ajira.

Naye Nandy amesema mbali ya kufanya tamasha hilo pia, wakiwa hapa Zanzibar wamepata fursa ya kutembelea vivutio kadhaa vya utalii vilivyopo hapa nchini.

Tamasha la Nandy festival lilianza mwaka 2019 na wasanii wameshatembelea mikoa ya Kigoma, Mwanza, Dodoma na Arusha lengo ni kusaidia vijana kupata ajira na kukuza muziki wa kizazi kipya barani Afrika.

Nandy ameahidi kushirikiana na wasanii wa Zanzibar ili kuupeleka mbele muziki huo.