Dk Tulia: Bunge kujadili ushirikiano wa bandari
Muktasari:
Spika wa Bunge Dk Tulia Ackson amesema azimio la Bunge kuhusu kuridhia ushirikiano wa uendelezaji na uboreshaji wa utendaji wa bandari Tanzania, litawasilishwa bungeni Juni 10, 2023 kwa ajili ya kujadiliwa na kupitishwa na wabunge.
Dodoma. Spika wa Bunge Dk Tulia Ackson amesema azimio la Bunge kuhusu kuridhia ushirikiano wa uendelezaji na uboreshaji wa utendaji wa bandari Tanzania, litawasilishwa bungeni Juni 10, 2023 kwa ajili ya kujadiliwa na kupitishwa na wabunge.
Azimio hilo ni mapendekezo ya kuridhia makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai kuhusu ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kwa ajili ya katika uendelezaji na uboreshaji wa utendaji wa Bandari Tanzania la 2023.
Akizungumza leo Alhamisi Juni 8, 2023, Dk Tulia amesema kuwa azimio hilo bado liko katika kamati ya pamoja ya Bunge inayojumuisha Uwekezaji na Mitaji ya Umma (PIC) na Miundombinu ambayo bado inaendelea kupokea maoni ya wadau ambao hawakuweza kufika Juni 6, 2025.
Amesema maoni ya kuhusu azimio hilo yanapokewa kupitia pia anwani za barua pepe zilizowekwa katika barua ya kuitisha maoni ya wadau.
“Azimio sasa bado liko katika ngazi ya kamati ya pamoja kwa mujibu wa kanuni na mara baada ya kamati kumaliza kazi yake azimio hilo limepangwa kuingia bungeni Juni 10, 2023 kwa ajili ya mjadala na kupitishwa na Bunge,” amesema.
Amesema Bunge litaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan katika kukuza uchumi na maendeleo Tanzania.
“Bunge liko tayari kupitia kamati zake kupokea na kujadili na kutoa maoni yale ambayo wananchi wameileta kule yenye lea kuboresha utekelezaji wa mipango ya Serikali,”amesema.