Mkurugenzi TPA asema makubaliano ya ukomo wa muda uwekezaji bandari haujafikiwa

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Plasduce Mbossa

Muktasari:

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Plasduce Mbossa amesema makubaliano ya ukomo wa muda wa mkataba baina yake na kampuni ya Duban Port World (DPW) inayomilikiwa na Serikali ya Dubai haujawekwa wazi hadi bunge litakapopitisha azimio lake kuhusu ushirikiano huo.


Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Plasduce Mbossa amesema makubaliano ya ukomo wa muda wa mkataba baina yake na kampuni ya Duban Port World (DPW) inayomilikiwa na Serikali ya Dubai haujawekwa wazi hadi bunge litakapopitisha azimio lake kuhusu ushirikiano huo.

Mbossa ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Juni 8, 2023 wakati wa mahojiano yaliyofanyika katika Kituo cha Matangazo cha Clouds 360, asubuhi ikiwa ni mwendelezo wa kutoa ufafanuzi wa hoja na elimu kuhusu makubaliano ya mkataba huo kwa Taifa.

Amesema mkataba huo wa ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kwa ajili ya uendelezaji na uboreshaji wa utendaji kazi wa bandari (IGA) upo katika hatua za majadiliano kabla ya Bunge la Tanzania kuuridhia.

“Mkataba huu hatutajadiliana wala hakuna muda wala hatujui kwa sababu kuna maeneo ya ushirikiano lakini hatujui atafanyia kazi sehemu gani, ama tutamkodisha ama ataendeleza sehemu gani, yako maeneo Bandari ya Dar es Salaam tunaweza kuongea naye tukafikia suala la muda,” amesema Mbossa.

Kwa mujibu wa mkataba huo, muda wa utekelezaji Mkataba huu haujawekwa bayana, bali Ibara ya 23 1) inasema kuwa ukomo wa Mkataba huu ni mpaka hapo shughuli za mradi huu zitakapokuwa zimekamilika. Serikali iombwe kutoa ufafanuzi kuhusu jambo hili la ukomo wa Mkataba.

Ibara ya 27 inaweka masharti kwamba, pale ambapo mkataba huo utaanza kutumika rasmi, Serikali yeyote haitaingia au kuwa sehemu ya makubaliano ya ndani ya nchi au ya kimataifa wakati wa utekelezaji wa mkataba, Sekretarieti ya bunge ikiitaka Serikali kutoa ufafanuzi wa kutokuwa na ukomo.