DPP atinga mahakamani kutoa ushahidi, mshtakiwa augua ghafla

Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Tanzania (DPP), Slyvester Mwakitalu

Muktasari:

Leo Jumanne Julai 5, 2022 katika kesi ya Jinai namba 99/2021 inayomkabili Joshua  Kamalamo(37) na mwenzake Yahaya Kapalatu(31), wanaokabiliwa na kesi ya kujitambulisha kuwa wao ni maofisa Usalama wa Taifa( TISS) kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini( DPP), Slyvester Mwakitalu.

Dar es Salaam. Katika hali isiyotarajiwa, Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Tanzania (DPP), Slyvester Mwakitalu, ametinga katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, kwa ajili ya kutoa ushahidi.

Ni leo Jumanne Julai 5, 2022 katika kesi ya Jinai namba 99/2021 inayomkabili Joshua  Kamalamo (37) na mwenzake Yahaya Kapalatu(31), wanaokabiliwa na kesi ya kujitambulisha kuwa wao ni maofisa Usalama wa Taifa (TISS) kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini( DPP), Slyvester Mwakitalu.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka mawili ya kujitambulisha kwa DPP kuwa wao ni maofisa kutoka Ofisi ya Raisi, Idara ya Usalama wa Taifa, jambo ambalo ni uongo.

Kesi hiyo ilipangwa leo Jumanne kwa ajili ya usikilizwaji, lakini mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo, Kamalamo aliugua ghafla akiwa mahakamani na hivyo kesi hiyo kuahirishwa.

Waongezewa maelezo katika hati ya mashtaka:

Mbali na DPP kutinga Mahamani hapo, upande wa mashtaka uliwasilisha ombi la kuwaongezea maelezo katika hati ya mashtaka ya washtakiwa hao.

Maelezo hayo yameongezwa katika hati ya mashtaka ya washtakiwa hao chini ya kifungu 234(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA).

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Grace Mwanga, amewasilisha ombi hilo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Godfrey Isaya, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ushahidi.

"Mheshiwa hakimu tunaomba kufanya mabadiliko kidogo kwenye hati ya mashtaka chini ya kifungu namba 234(1) cha CPA," amesema wakili Mwanga huku akiomba kuwasomea upya mashtaka yao

Mwanga baada ya kueleza hayo, Hakimu Isaya aliwauliza washtakiwa iwapo wapo tayari kusomewa mashtaka upya bila kuwepo wakili wao.

Hata hivyo washtakiwa hao walikubali na upande wa mashtaka uliwasomea mashtaka.

Akiwasoma upya mashtaka yao, wakili Mwanga amedai washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka mawili ya kujitambulisha kuwa wao ni maofisa Usalama kutoka TISS, wakati wakijua kuwa sio kweli.

Katika shtaka la kwanza, linalomkabili Kamalamo peke yake, inadaiwa Juni 11, 2021 katika ofisi ya Taifa ya Mashtaka nchini (NPS) ilizopo katika jengo la Wizara ya Mambo ya Ndani, jiji hapa, alijitambulisha kwa Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DDPP) Joseph Pande kuwa anatoka Ofisi ya Raisi, Idara ya Usalama wa Taifa (TISS).

Mwanga amedai Kamalamo alimwambia Pande kuwa amepewa maelekezo kutoka kwa raisi kuwa wasiendelee na majadiliano ya kuimaliza kesi (Ple Bargaining) katika kesi ya uhujumu uchumi namba 27/2017 inayomkabili Harbinder Seth na wenzake, mpaka hapo watakapopewa maelekezo mengine.

Shtaka la pili, linawakabili washtakiwa wote ambapo wanadaiwa Juni 12, 2021, katika ofisi ya Taifa ya Mashtaka nchini (NPS) zilizopo katika jengo la Wizara ya Mambo ya Ndani, jiji hapa, Kamalamo na Kapalatu walijitambulisha kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) Slyvester Mwakitalu kuwa wanatoka Ofisi ya Raisi, Idara ya Usalama wa Taifa(TISS).

"Kamalamo na Kapalatu, wanadaiwa walimueleza DPP kuwa wamepewa maelekezo kutoka kwa raisi wasiendelee na majadiliano ya kuimaliza kesi (Ple Bargaining) katika kesi ya uhujumu uchumi namba 27/2017 inayomkabili Harbinder Seth na wenzake, mpaka hapo watakapopewa maelekezo mengine, Jambo ambalo wanajua kuwa ni uongo" amedai Wakili Mwanga.

Washtakiwa baada ya kusomewa mashtaka yao, walikana kutenda.

Mwanga amedai upande wa mashtaka unaye shahidi mmoja na kwamba wapo tayari kuendelea na ushahidi.

Wakili Mwanga baada ya kueleza hayo, mshtakiwa Kamalamo amenyoosha mkono juu na alipopewa nafasi na hakimu ya kuongea, alidai yeye ni mgonjwa anaumwa sana kichwa na ana presha hivyo mwili wake hauna nguvu na kwamba wiki iliyopita alichoma sindano, hivyo hataweza kusikiliza kesi hiyo.

"Mheshimiwa hakimu, mimi naumwa tangu asubuhi ningepata muda wa kuonana na wewe pengine saizi ningekuwa hospitali, maana naumwa kichwa, Nina presha na mwili wangu hauna nguvu na wiki iliyopota nilichoma sindano machoni" amedai mshtakiwa.

Hata hivyo hakimu Isaya aliahirisha kwa muda wa dakika tano kesi hiyo na kuwapa nafasi upande wa mashtaka waweze kuwasilina na shahidi kujua atakuwa na nafasi tarehe ngapi ili kesi hiyo iweze kuendelea siku hiyo.

Baada ya dakika tano kuisha wakili wa Serikali Timotheo Mmari alidai kuwa kutokana na majukumu aliyonayo shahidi huyo uwezekano wa kumpata kwa mara ya pili ni mgumu kwa sababu kesi hiyo ilishaahirishwa mara kadhaa wakimsubiri shahidi hiyo muhimu katika kesi hiyo.

Hata hivyo baada ya majadiliano ya kina na kutokana na mshtakiwa wa kwanza kuwa mgonjwa, Hakimu Isaya aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 14, 2022 itakapoendelea.

Hakimu atoa onyo kwa washtakiwa na wakili wao:

Awali, kabla ya kesi hiyo kuanza, wakili wa washtakiwa hao Marietha Mollel hakuwepo mahakamani hapo na walipoulizwa washtakiwa walidai kuwa aliwaaga kwenda Mahakama Kuu ambapo huko alikuwa na kesi nyingine.

"Mheshimiwa hakimu wakili wetu ameenda Mahakama Kuu anakesi nyingine huko saa sita mchana huu( Jana) , tumejaribu kumtafuta kwenye simu yake  hapatikani" alidai Kapalatu.

Hakimu Isaya alihoji sababu ya yeye kuondoka bila kutoa taarifa wakati asubuhi alikuwepo mahakamani hapo Ni Nini?

Hakimu Isaya alisema Wakili Mollel alipaswa kutoa taarifa Mahakamani hapo.

"Mwambieni wakili wenu( Mollel) kitendo alichofanya sio kizito, hata Kama anakesi Mahakama Kuu, alitakiwa afuate utaratibu wa kutoa taarifa Mahakamani hapa na sio pembeni!? Mwambieni taarifa za pembeni sizitaki Mimi" alisema Hakimu Isaya.

Pia alimtaka mshtakiwa Kamalamo kupeleka udhibitisho wa cheti cha daktari kinachodhibitisha kuwa ni mgonjwa na amepata matibabu.