DPP awafutia kesi waliodaiwa kujipatia Sh23 bilioni za ujenzi wa mradi wa maji

Muktasari:

 Washtakiwa  hao wamefutiwa kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 10/2021, baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) kuieleza Mahakama hiyo kuwa,  hana nia ya kuendelea na kesi

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemfutia kesi na kumwachia huru, Mkurugenzi wa Kampuni ya M/S Badr East African Enterprise  Limited, Giafar Beder (71) na wenzake watatu, waliokuwa wakikabiliwa na mashtaka 10 yakiwamo ya kuongoza genge la uhalifu, kughushi na kujipatia Dola10.6 milioni za Marekani (Sh23 bilioni)  kwa njia ya udanganyifu.

Pia, walikuwa wanadaiwa kughushi nyaraka ya kutolea fedha na kuiwasilisha kwa Katibu Mkuu Wizara ya Maji na Umwagiliaji na kujipatia fedha.

Washtakiwa  hao wamefutiwa kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 10/2021, baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) kuieleza Mahakama hiyo kuwa,  hana nia ya kuendelea na kesi dhidi ya washtakiwa hao.

Mbali na Beder ambaye ni mkazi wa Masaki, washtakiwa wengine waliofutiwa kesi hiyo ni Badr Mohamed (59) ambaye ni Meneja wa kampuni hiyo na mkazi wa Tabata;  Ahmed Badr- Al Katiyr(69) Mkurugenzi wa kampuni hiyo na mkazi wa Kariakoo pamoja na Mhasibu wa kampuni hiyo, Akil Hassanali(56) mkazi wa mtaa wa Mkwepu jiji hapa.

Washtakiwa hao wamefutiwa mashtaka yao chini ya kifungu namba 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ( CPA) Sura ya 20, iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2022.

Uamuzi wa kuwafutia kesi hiyo na kuwaachia huru, umetolewa leo Aprili 2, 2024  na Hakimu Mkazi Mkuu, Amir Msumi baada ya upande wa mashtaka kuieleza Mahakama kuwa DPP hana nia ya kuendelea na mashtaka dhidi ya washtakiwa hao, hivyo wanaomba kuliondoa shauri hilo.

Wakili wa Serikali, Titus Aaron ameieleza Mahakama hiyo kuwa kesi hiyo imeitwa kwa ajili ya kutajwa lakini DPP, hana nia ya kuendelea na kesi hiyo dhidi ya washtakiwa hao.

Wakili Aaron baada ya kueleza hayo, Hakimu Msumi alisema kupitia kifungu hicho,  Mahakama imewafutia mashtaka washtakiwa hao na kuwaachia huru.

Hata hivyo, Hakimu Msumi amesema kupitia kifungu hicho hicho, DPP ana mamlaka ya kuwakamata tena na kuwafungulia mashtaka.

Washtakiwa baada ya kuachiwa walishuka haraka katika ngazi na kuingia katika gari na kuondoka.

Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo Februari 17, 2021 na kusomewa mashtaka yanayomkabili.

Kati ya mashtaka 10 yaliyokuwa yanawakabili; mashtaka matatu ni ya kughushi, mashtaka matatu ni ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, mashtaka matatu ni ya kutoa nyaraka za uongo na shtaka moja ni la kuongoza genge la uhalifu.

 Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kuongoza genge la uhalifu, tukio wanalodaiwa kulitenda kati ya Oktoba 24, 2016 hadi Agosti 31, 2018, katika maeneo mbalimbali ya wilayani Ilala.

Wakiwa na nia ovu  waliongoza genge la uhalifu kwa kuandaa mradi kwa lengo la kulaghai kwa kutumia njia za uongo na kuweza kujipata fedha hizo.

Katika shtaka la kughushi, washtakiwa wanadaiwa kabla ya Oktoba 24, 2016 eneo la  Tabata Matumbi  Wilaya ya Ilala, walighushi nyaraka ya malipo ya awali namba CRD 16-IGT 815 ya Oktoba 24,2016 wakionesha kwamba imetolewa na Benki ya CRDB kwenda kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa ajili ya kutoa malipo ya awali kwa kampuni hiyo Dola 5 milioni za Marekani wakijua si kweli.     

Katika shtaka la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kati ya Desemba 12, 2016 na Septemba 27, 2018 eneo la Tabata Matumbi, kwa njia ya udanganyifu walijipatia malipo ya awali kutoka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dola5  milioni za Marekani ( Sh 11 bilioni) kuhusiana na ujenzi wa Mradi wa Maji wa Same- Mwanga- Korogwe wa awamu ya kwanza na awamu ya pili.

Inadaiwa kuwa katika kipindi hicho, washtakiwa walidanganya kwamba Benki ya CRDB imewapatia malipo ya awali kupitia dhamana (Guarantee) namba CRDB  16-IGT 815 iliyotolewa Oktoba 24, 2016 inayohusiana na Katibu Mkuu Wizara ya Umwagiliaji.

Hata hivyo, malipo hayo ya awali yaliweza kulipwa kwa Kampuni ya M/S Badr East African Enterprise Limited, jambo ambalo walijua sio kweli.