Guinea inavyomchagua rais wake katikati ya dimbwi la damu

Muktasari:

Kuna koloni la zamani la Hispania, Spanish Guinea ambayo sasa inaitwa Equatorial Guinea, ipo Guinea ya Ureno inayoitwa Guinea-Bissau na Guinea ya Ufaransa, kwa maana ya Guinea.

Ukiacha New Guinea ambacho ni kisiwa kilichopo kwenye nchi za Bahari (Oceania), Afrika ina mataifa matatu yanayoitwa Guinea.

Kuna koloni la zamani la Hispania, Spanish Guinea ambayo sasa inaitwa Equatorial Guinea, ipo Guinea ya Ureno inayoitwa Guinea-Bissau na Guinea ya Ufaransa, kwa maana ya Guinea.

Hata hivyo, kwa sababu ya kuzidi kuitofautisha Guinea na nyingine, wengine huiita Guinea Conakry. Ni kwa sababu mji wake mkuu ni Conakry. Sasa, Oktoba 18, yaani leo, Guinea (Conakry) inafanya uchaguzi wa kupata viongozi wapya, lakini zaidi watamchagua rais ambaye ataliongoza taifa hilo kwa miaka sita ijayo.

Ahmed Sekou Toure, Rais wa Kwanza wa Guinea, wakati akipigania uhuru wa nchi hiyo, aliwaambia Wafaransa (wakoloni) kuwa; “Guinea inaona afadhali umaskini kwenye uhuru kuliko utajiri katika utumwa.”

Tangu Oktoba 2, 1958, Guinea ilipopata uhuru mpaka sasa ni miaka 62, na raia wa Guinea bado wapo kwenye mapambano -- kutoka kupigania uhuru na sasa ni kilio cha demokrasia. Leo wapiga kura milioni 5.4 wanatarajiwa kupanga foleni katika vituo vya kupiga kura kuchagua viongozi wapya.

Utakuwa upigaji kura katikati ya dimbwi la damu. Waguinea watachagua rais baada ya mwaka mmoja na mwezi mmoja na siku 10 za maandamano yaliyosababisha majeruhi na vifo.

Mapema mwezi huu, Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International lilitoa ripoti kuwa kati ya Oktoba 14, mwaka jana na Julai mwaka huu, watu zaidi ya 50 walikuwa wameuawa kwa sababu ya maandamano.

Hata hivyo, muungano wa vyama vya upinzani unaojiita Umoja wa Kitaifa wa Kuilinda Katiba (FNDC), wanasema waliouawa ni zaidi ya 90.

Chanzo cha machafuko

Oktoba 7, mwaka jana, FNDC waliitisha maandamano nchi nzima kupinga mabadiliko ya Katiba.

Mpaka wakati huo, tayari kulishakuwa na fununu kwamba katiba ingepinduliwa, kipengele cha ukomo wa mihula miwili ya uongozi kwa rais wa nchi hiyo kingeondolewa, kisha Rais Alpha Conde, angegombea kwa muhula wa tatu.

Oktoba 14, mwaka jana, watu watano walipigwa risasi na kuuawa, ikiwa ni siku ya kwanza ya maandamano ya kupinga kupinduliwa kwa katiba. Pamoja na hivyo, maandamano yaliendelea kwa makundi. Desemba mwaka jana, Rais Conde alitangaza rasimu mpya ya katiba.

Wapinzani waliiita rasimu hiyo kuwa ni mapinduzi ya kikatiba, wakaitisha maandamano makubwa zaidi. Dola nayo ikatumia nguvu kubwa kudhibiti waandamanaji. Waguinea wakaendelea kuuawa.

Machi 22, mwaka huu, Waguinea walipiga kura ya kikatiba na kupitisha mabadiliko yaliyoondoa ukomo wa vipindi viwili vya uongozi kwa rais wa nchi hiyo.

Agosti 6, mwaka huu, chama tawala cha RPG kilimuomba Conde awe mgombea wake wa urais. Septemba 2, Conde alikubali kugombea kipindi cha tatu.

Kukubali kwa Conde kuwa mgombea urais wa RPG, kulisababisha maandamano makubwa zaidi. Septemba 30, Waziri Mkuu wa Guinea, Ibrahima Kassory Fofana akiwa na msafara wake kwenye mji wa Fouta-Djalonuliopo Kaskazini ya nchi hiyo, alishambuliwa kwa mawe na waandamanaji. Watu wengi walijeruhiwa, ingawa Fofana alitoka salama.

Na hiyo ndio hali ya siasa na usalama wa Guinea tangu Oktoba mwaka jana. Maandamano hayajawahi kukoma. Hata sasa kipindi ambacho nchi imo kwenye uchaguzi, maandamano yanaendelea. Na hakuna dalili kwamba yatakoma baada ya uchaguzi.

Kinachokwenda kutokea

Septemba 9, mwaka huu, kinara wa siasa za kupinga Conde kugombea kwa muhula wa tatu, Cellou Dalein Diallo, alijitenga kwenye kuhamasisha vuguvugu la maandamano, badala yake alitangaza kumkabili kwenye uchaguzi. Kwa sasa, idadi ya wagombea urais Guinea wapo 12, lakini mchuano upo kwa watu wawili; Conde na Diallo.

Uwepo wa wagombea wengi unasababisha kuwepo kwa shaka kwamba huenda asipatikane mshindi atakayezidi asilimia 50 ya kura.

Na endapo itatokea hivyo, maana yake wagombea wawili watapepetana katika duru ya pili. Inadhaniwa kwamba watakuwa Conde na Diallo.