Hakimu akwamisha kesi ya Gugai

Muktasari:

  • Kesi ya utakatishaji fedha na kumiliki mali zisizolingana na kipato chake, inayomkabili aliyekuwa Mhasibu Mkuu wa Takukuru, Godfrey Gugai na wenzake watatu imeshindwa kuendelea kutokana na hakimu anayesikiliza kesi hiyo kutokuwepo.

Dar es Salaam.Kesi ya utakatishaji fedha na kumiliki mali zisizolingana na kipato chake, inayomkabili aliyekuwa Mhasibu Mkuu wa Takukuru, Godfrey Gugai na wenzake watatu imeshindwa kuendelea katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kutokana na hakimu anayesikiliza kesi hiyo kutokuwepo.

Wakili wa Serikali, kutoka Takukuru Vitalis Peter ameeleza hayo mahakamani leo Januari 23, 2019 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kuendelea na usikiluzwaji.

Wakili Peter amedai kuwa kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kuendelea kusikilizwa kwa ushahidi lakini hakimu anayeisikiliza shauri hilo wamepata taarifa kuwa hayupo hivyo kuomba tarehe nyingine.

Baada ya maelezo hayo, Hakimu Mashauri ameahirisha kesi hiyo hadi Februari 5, mwaka huu  kwa ajili ya kuendelea na usikilizwaji.

Tayari mashahidi sita wa upande wa mashtaka wameshatoa ushahidi akiwemo Msajili wa Hati Msaidizi, kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Joanitha Kazinja na msaidizi wa hati Kanda ya Kaskazini kutoka wizara hiyo, Emmanuel Bundala.

Mbali na Gugai, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni George Makaranga, Leonard Aloys na Yasin Katera.