Halmashauri kikaangoni fedha za uchumi wa vijana

Muktasari:
- Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru, Sahil Geraluma ameziagiza halmashauri saba za Mkoa wa Kagera kuhakikisha Sh217.5 milioni za mfuko wa vijana zilizotolewa na Serikali kusaidia shughuli za kiuchumi zinarejeshwa.
Biharamulo. Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru, Sahil Geraluma ameziagiza halmashauri saba za Mkoa wa Kagera kuhakikisha Sh217.5 milioni za mfuko wa vijana zilizotolewa na Serikali kusaidia shughuli za kiuchumi zinarejeshwa.
Bila kutaja halmashauri hizo, Geraluma alisema kati ya halmashauri nane, ni moja pekee ndiyo imesimamia vyema fedha za mfuko wa maendeleo ya vijana.
Akizungumza wakati wa hafla ya kuupokea Mwenge wa Uhuru kutoka kwa viongozi wa Mkoa wa Kigoma juzi, Geraluma alimwagiza Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Albert Chalamila kusimamia utekelezaji wa agizo hilo kabla Mwenge wa Uhuru haujafika kwenye wilaya zenye tatizo hilo.
“Viongozi wa wilaya na halmashauri husika wahakikishe fedha hizo zinarejeshwa kabla Mwenge wa Uhuru haujafika katika halmashauri zao, maana Mwenge wa Uhuru hautaondoka kabla fedha zote hazijarejeshwa,” alisema Geraluma.
Kuhusu miradi ya maendeleo, kiongozi huyo wa mbio za Mwenge aliwaagiza watendaji kuhakikisha miradi yote inatekelezwa kwa wakati kulingana na thamani halisi ya fedha.
Akitoa taarifa ya utekelezaji, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Albert Chalamaila alisema miradi 37 ya Sh13.6 bilioni itakaguliwa, kuwekewa mawe ya msingi na kuzinduliwa.