Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hoja zao zafunikwa, kibao chawageukia Kinana, Makamba

Ni wiki ya tatu sasa tangu makatibu wakuu wastaafu wa CCM, Abdulrahman Kinana na Yusuf Makamba walipotoa waraka unaoeleza madhila wanayopitia na kuzua mjadala nchini.

Wastaafu hao wameeleza mambo ambayo yanapaswa kufanyiwa kazi na mamlaka husika na ikibidi kujibiwa, basi iwe kwa utulivu na umakini mkubwa.

Watu mbalimbali wakiwamo viongozi wa CCM wamejitokeza na kutoa majibu ambayo kwa kiasi kikubwa, yapo nje ya hoja zilizoibuliwa na makatibu hao wastaafu, kinyume na kanuni za kujenga hoja kimantiki.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Faraja Kristomus anasema kuna tatizo kubwa kwenye jamii la kuacha hoja zinazotolewa na mtu, badala yake kujielekeza katika kumkosoa mtu aliyetoa hoja husika.

Anasema suala hilo halipo serikalini pekee bali sekta binafsi pia, pamoja na taasisi za kijamii. Hiyo ni kasumba inayosambaa ambayo inayopaswa kushughulikiwa mapema ili kupata jamii inayojali hoja za mtu bila kuangalia tofauti zilizopo.

Yeye anaamini samaki huoza kuanzia kichwani kwenda mkiani, hivyo anashauri uzingatiaji wa hoja kuanza kufundishwa shuleni na kushuka hadi ngazi ya familia.

Mabadiliko ya fikra yaanzie kwa vijana wadogo kuondokana na hali hii ili tujielekeze kwenye hoja, hii itasaidia kutatua kero zilizopo,” anasema.

Hoja zenyewe

Kwenye andiko lao walilolitoa Julai 14, Kinana na Makamba waliainisha hoja kadhaa ambazo yeyote anayewajibu kimantiki anapaswa kujielekeza kwazo.

Jambo la mojawapo, katika kuandaa waraka wao, Kinana na mwenzake wameishirikisha jamii. Kwa maneno yao wanasema wamepata ushauri kutoka kwa watu mbalimbali wakiwamo viongozi wakuu wastaafu wa CCM, viongozi wa dini, wanataaluma, wanahabari, wana-CCM na wananchi kadhaa.

Baada ya kushauriwa ndipo wakatoa tamko kuhusu ‘uzushi unaoenezwa’. Lakini wanaojibu, kila mmoja anajisemea mwenyewe. Hakuna anaeleza ameshauriwa na yeyote, bali kwa kuamini ana mawazo bora kuliko yaliyotolewa na viongozi wastaafu, dini, wanataaluma na wanahabari.

Makundi hayo yote yapo, yashirikishwe kuwajibu wazee hawa. Hakuna wazo bora la mtu mmoja kuliko wengine wote. Hata hawa wanaolalamika, waliamini mawazo ya wengine ni muhimu kufikisha ujumbe wao.

Wazee hawa wanalalamika kuhusu kutuhumiwa kumkwamisha Rais wa Tanzania kutekeleza majukumu yake. Kwa kuwa tuhuma zimetolewa zaidi ya mara moja, wanasema waliamini viongozi wangeyaona na kuchukua hatua lakini haikuwa hivyo. Hakuna aliyekemea wala kuzuia “upotoshaji dhidi yao.”

Kati ya wote waliojitokeza na kuzungumzia waraka huo, hakuna anayethibitisha uwezekano wa wastaafu hao kufanya wanayodaiwa kufanya au kwa jinsi gani mtandao wao unavyoweza kuzuia kuruhusiwa kwa Rais John Magufuli kugombea tena mwakani. Bila shaka ni hofu ya wanaomuunga mkono Rais.

Ipo pia hoja inayohusisha muungano. Wazee hao wanaeleza jinsi wanavyoumia kuona viongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar nao wanatuhumiwa kumhujumu Rais bila kujali athari za kauli hizo kwa muungano.

Kati ya waliojitokeza kutoa majibu hadi sasa, hakuna aliyeligusia hili. Hakuna anayeeleza kama ni sawa kuwatuhumu viongozi wa Zanzibar kumhujumu Rais Magufuli wala kufafanua hujuma hizo zinafanywa namna gani.

Tuhuma hizi zinatolewa huku kukiwa na malalamiko mengi kuhusu muungano na tuhuma zinazotolewa hazilengi kuzitatua kero zilizopo bali kuongeza udhaifu mwingine.

Kinana na Makamba wanaamini tuhuma zinazotolewa dhidi yao hazina ukweli bali zina malengo maalumu ambayo ni kuwadhalilisha, kuwavunjia heshima,

kujenga chuki na kuwachafulia majina ndani na nje ya chama.

Majibu kwa hoja hiyo yanapaswa kugusa haya na kufafanua ni kwa kiasi gani heshima ya viongozi wa SMZ inalindwa au kwamba kinachofanywa dhidi yao kinavyowachafua.

Mpaka sasa hakuna aliyeeleza kama kinachofanywa na mwanaharakati Cyprian Musiba kinasaidia kujenga umoja wa kitaifa na kudumisha amani.

Hoja nyingine kwenye waraka wa wazee hawa ni matumizi mabaya ya mamlaka. Wanaamini yupo mtu mwenye mamlaka makubwa ambaye anamkingia kifua mwanaharakati anayewatuhumu na kuwakashifu Watanzania wenzake, viongozi na watendaji wa Serikali, taasisi za umma na kijamii hata sekta binafsi.

Hata anapotumia lugha za vitisho, hakuna hatua zinazochukuliwa dhidi yake. Jeshi la polisi lenye jukumu la kulinda raia na mali zao ni kama halimuoni. Labda nalo halina meno ya kutosha kumsogelea Musiba.

Ukiwasikiliza waliojitokeza kuzungumzia waraka huu, hakuna anayesema Musiba anakamatika au anaweza kuhojiwa. Wao wanamuunga mkono na kuendeleza tuhuma kwa viongozi hao wastaafu.

Kwa kipindi cha uongozi wao ndani ya chama hata serikalini, Kinana na Makamba wamewaandaa vijana wengi ambao wameshika nafasi kubwa kwenye ofisi za umma sasa hivi.

Kwenye waraka wao wanasema kuna kila dalili kuwa lengo la mkakati huu ni kuwahusisha wao, wastaafu wengine na walio kazini na matendo ya kihalifu, kimaadili na kihaini ili kuhalalisha wanayokusudia kuyafanya.

Majibu yanayotolewa au yatakayotolewa yanapaswa kueleza hili. Kama kuna mtandao umeachwa na makatibu wakuu hawa wa CCM ubainishwe na uhalifu walioufanya au wanaoendelea kuufanya uelezwe bayana na hatua kuchukuliwa kama zinastahili.

Hatua zozote zilizochukuliwa na vyombo vya ulinzi na usalama kuchunguza mtandao huo pia zibainishwe na kama kuna msaada wowote kutoka vyombo vya kimataifa uelezwe.

Makatibu hao wameamua kuandika barua kwa Katibu wa Baraza la ushauri la viongozi wastaafu wa CCM, kwa kuzingatia ibara ya 122 ya katiba ya CCM ya mwaka 2017 ili kulishughulikia jambo hili.

Wanaojibu hawaelezi wanatumia kifungu gani cha Katiba ya chama wanachotumia kuwajibu na kushambuliwa wastaafu hao. Majibu ya makada yajielekeze kufafanua tuhuma na mkakati uliopo kama unaimarisha umoja, mshikamano na utulivu ndani ya chama na Taifa.

Baada ya maelezo hayo yote, bila shaka kwa ushauri waliopewa na wadau waliowashirikisha kabla ya kuandika na kuutoa waraka huo, wanasema wameamua kutokwenda mahakamani, walau kwa sasa.

Kwa kuwa jinai haina mwisho, ‘kinga’ ya Musiba ikiisha watakwenda mahakamani kudai haki yao. Kwa kuwa sasa kinga inafanya kazi, wameamua watulie wakijipanga namna ya kuishinda vita iliyopo mbele yao.

Wamefanya hivyo kwa sababu jambo hili wanaona lina taswira ya kimkakati na lengo la kisiasa. Wao ni wanasiasa waandamizi hivyo wanashughulikia kisiasa kwanza. Mahakamani watakwenda baadaye.

Wanajua kwenda mahakamani baada ya kuchafuliwa kunahusisha kudai fidia, wanaamini thamani yao ni kubwa kuliko fidia wanayoweza kulipwa na anayewachafua pamoja na anayemlinda bila shaka.

Kinana na Makamba wametimiza wajibu wao. Wanasema wamepata ushauri kutoka kwa watu wanaostahili, wakawasilisha malalamiko yao sehemu husika huku wakijipanga kuishughulikia jinai iliyomo kwenye tuhuma zinazotolewa dhidi yao.

Yeyote anayejitokeza na kurusha maneno bila kujielekeza kwenye hoja walizozitoa, anapoteza muda na nguvu zake. Kinachohitajika ni suluhu ya yaliyoelezwa kwenye waraka wao.

Na ni vyema wakakumbuka kuwa wazee hawa wameweka kiporo kwenda mahakamani, hivyo wanaojitokeza na kuunga mkono tuhuma zinazowalenga wasishangae wakiguswa na mkono wa sheria watakapoona inafaa kufungua kesi, baada ya kinga iliyopo kuondoka.