‘Homework’ za likizo chanzo cha ukatili huu
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kakanja, Wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera, Isaya Emmanuel akimchapa mwanafunzi kwenye nyayo kama inavyoonekana kwenye video. Picha na Mtandao.
Bukoba. Ni ukatili wa kutisha, ndivyo unavyoweza kusema kwa tukio la Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kakanja, Wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera, Isaya Emmanuel kuwachapa viboko kwenye nyayo wanafunzi wawili wa darasa la nne, Salmon Kakwezi (9) na Anord Kweyamba (10).
Katika video iliyosambaa mitandaoni, mwalimu huyo anaonekana akiwachapa watoto viboko kwenye nyayo za miguu huku wakilia.
Tukio hilo lililotokea Januari 10, siku moja baada ya shule za msingi na sekondari kufunguliwa, limevuta hisia kali miongoni mwa Watanzania, wakitaka ukatili kwa watoto ukomeshwe haraka.
Juzi baada ya video hiyo kusambaa, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima aliwataka wananchi kutoa taarifa wanapoona matukio kama hayo ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa.
“Unapoona vitendo vya ukatili, tuma ujumbe kwenye DM au kwenda namba 0734124191 ili tuweze kushirikiana dhidi ya vitendo hivi. Tunaomba taarifa zaidi kuweza kujua ni shule gani na mkoa gani. Asanteni nyote kwa kuendelea kuibua vitendo vya kikatili dhidi ya watoto,” ameandika Waziri Gwajima katika ukurasa wake wa Twitter.
Waziri wa Elimu
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda ametoa ufafanuzi wa mwalimu mkuu Kagera, aliyewaadhibu watoto wawili kwa kuwachapa viboko isivyostahili kuwa ameshushwa cheo na kusimamishwa kazi.
Jana, Waziri Mkenda alitoa taarifa iliyosambaa mitandaoni akisema tayari hatua zimeshaanza kuchukuliwa.
Alitaja hatua zilizochukuliwa ni kufukuzwa, huku akisubiri hatua nyingine za kinidhamu.
“Ndugu zangu niliona klipu ya video inayozunguka sana ikimuonyesha mwalimu mkuu wa shule ya msingi Kakanja akiwaadhibu wanafunzi kwa kuwachapa viboko, tumeshafuatilia.”
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Albert Chalamila akizungumza na waandishi wa habari jana alisema tukio hilo lilitokea Januari 10, mwaka huu, siku moja baada ya muhula wa masomo wa mwaka 2023 kufunguliwa.
Chalamila alimwagiza Katibu Tawala wa mkoa huo, Toba Nguvila kumwajibisha ofisa elimu wa Kata ya Kimuli kwa kushindwa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwenye shule hiyo.
Pia, aliagiza kuchukuliwa hatua kwa walimu wanne waliokuwa ofisini hapo wakicheka wakati mwalimu huyo akitoa adhabu kwa wanafunzi.
Aliwataja walimu hao wanne kuwa ni Godson Rwamwisho, Beatrice Osward, James Josia na Delifina Leonsi ambao alimwagiza katibu tawala kuwachukulia hatua za kinidhamu kwa kushindwa kumshauri mwalimu huyo wakati anafanya tukio la kuwaadhibu watoto.
Alieleza sababu ya mwalimu huyo kuwapa adhabu wanafunzi ni kukataa kufanya maswali waliyopewa wayafanyie nyumbani wakati wa likizo, hivyo akawapa adhabu kwa kuwachapa viboko kwenye nyayo za miguu huku akiwa amewakanyanga miguu yao.
Katika andiko lake lililotumwa mitandaoni, Ofisa Elimu wa Shule za Msingi wa Wilaya ya Kyerwa, Marwa R.Y aliomba radhi kwa kitendo cha mwalimu huyo kutoa adhabu kwa wanafunzi hao na kusema kuwa ameshaandikiwa barua kwa mamlaka ya nidhamu ya Tume ya Utumishi ya Walimu (TSC) ili akajibu tuhuma zake.
“Tumeshachukua hatua kwa mwalimu kusimamishwa na kutenguliwa kwa nafasi yake kama mwalimu mkuu, pia ameshaandikiwa charge (mashtaka) kwa mamlaka ya nidhamu ya TSC ili akajibu tuhuma zake.
Pamoja na yote tumeongea na watoto waliopata kadhia hii na kuwatia moyo ili wasijisikie vibaya kwa wenzao na kuwapa moyo wa kuendelea na masomo,” inasema sehemu ya maelezo ya Marwa.
Mmoja wa wazazi, Fulgence Kosmas alilaani kitendo cha mwalimu huyo kuwachapa viboko wanafunzi katika nyayo za miguu, akisema huenda hiyo ikawa sababu ya baadhi ya wanafunzi kukataa kuendelea na masomo na kuwa watoro.
Mzazi mwingine, Emiliana Michael alisema adhabu hiyo ni ukiukwaji wa haki za watoto.
Mtoto aliyepigwa na baba yake
Askari wa Jeshi la Polisi namba H. 4178 PC Abati Nkalango wa Bariadi mkoani Simiyu alimpiga fimbo mtoto wake sehemu mbalimbali za mwili na kumsababishia majeraha makubwa.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Blasius Chatanda, mtoto huyo wa miaka saba, mwanafunzi wa Shule ya Msingi Gappa alipigwa na baba yake kwa madai ya kushindwa maswali ya hisabati.
Maelekezo ya adhabu kwa walimu
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-(Tamisemi) Angellah Kairuki amewakumbusha walimu kutoa adhabu ya vikobo kwa wanafunzi kwa kuzingatia maelekezo ya waraka namba 24 wa mwaka 2002 na kanuni zake.
Waziri Kairuki alitoa kauli hiyo jana, wakati wa kikao kazi cha mapitio na tathmini ya utekelezaji wa shughuli za uboreshaji na usimamizi wa elimu mwaka 2022 Mkoa wa Dar es Salaam.
Waziri Kairuki anatoa ufafanuzi huo ikiwa ni siku chache baada ya mjadala wa video iliyosambaa mitandaoni ikionyesha adhabu kwa mwanafunzi.
“Ukitoa adhabu kinyume na waraka huo ni kosa la jinai na adhabu zake zipo, tayari tumeshaanza kuchukua hatua, lakini pia ni kinyume cha haki za binadamu,” alisema Waziri Kairuki.
Kwa mujibu wa waraka huo, adhabu ya viboko itatolewa kwa mwanafunzi aliyeonyesha utovu wa nidhamu uliokithiri, kosa la jinai au kosa linaloshusha heshima ya shule.
Imeandikwa na Peter Elias, Kelvin Matandiko (Dar) na Alodia Dominick (Kagera).