Hoteli ya Ngurdoto yageuzwa hosteli

Hoteli ya Ngurdoto yageuzwa hosteli

Muktasari:

Hoteli hiyo ilikuwa ikimiliki na mfanyabiashara, Melau Mrema aliyefariki mwaka Agosti 2017 na wanahisa wengine,ilifunguliwa rasmi mwaka 2003 ikiwa na vyumba 300 ikiwemo vya kulaza wageni wenye hadhi ya wakuu wa nchi saba na wasaidizi wao.

Arusha. Hoteli ya kitalii ya Ngurdoto mountain lodge yenye hadhi ya nyota tano iliyopo wilayani Arumeru Mkoa wa Arusha, imegeuzwa hosteli ya chuo cha Uhasibu Arusha baada ya kufungwa kwa siku kadhaa kutokana na ukosefu wa wateja, baada watalii kutoka nje kupungua kutokana na janga la ugonjwa wa virusi vya corona, Covid-19 duniani.

Hoteli hiyo ilikuwa ikimiliki na mfanyabiashara, Melau Mrema aliyefariki mwaka Agosti 2017 na wanahisa wengine,ilifunguliwa rasmi mwaka 2003 ikiwa na vyumba 300 ikiwemo vya kulaza wageni wenye hadhi ya wakuu wa nchi saba na wasaidizi wao.

Hoteli ya Ngurdoto itaendelea kukumbukwa kutokana na kupokea wageni kutoka maeneo mbalimbali duniani katika mkutano wa Sullivan mwaka 2008.

Pia kipindi cha awamu ya nne, hoteli hiyo ilitumiwa na Serikali kwa kufanyika semina elekezi kwa viongozi wote walioteuliwa wakiwepo mawaziri, makatibu wakuu na watendaji wengine.

Ngurdoto pia itakumbukwa kama hoteli pekee iliyokuwa ikifanyika mikutano ya wakuu wa nchi za Afrika ya Mashariki hasa kutokana na kuwa na vyumba maalumu ambavyo vilikuwa na uwezo wa kulaza marais na kuwa na kumbi kubwa zenye uwezo wa kuchukua zaidi ya wajumbe 2,000 wakati mmoja.

Akizungumza na Mwananchi jana, Mkuu wa chuo cha Uhasibu Arusha, Profesa Eliamani Sedoyeka alithitisha chuo hicho kukodi hoteli hiyo na sasa zaidi ya wanafunzi 1,000 wamepata sehemu ya kulala.

Profesa Sedoyeka alisema chuo hicho kililazimika kutafuta eneo la hosteli ya wanafunzi baada ya mwaka huukupokea idadi kubwa ya wanafunzi.

“Chuo baada ya kuona ongezeko la wanafunzi, tulianza mkakati kutafuta eneo la kulala wanachuo. Tulizungumza na kampuni Landmark ambayo inasimamia hoteli ya Ngurdoto na yaliyokwenda vizuri,” alisema.

Hata hivyo, alisema kuna mabadiliko yameanza kufanyika ili kupokea wanafunzi wengi ikiwepo kutengenezwa vitanda vya kulala watu wawili wawili (double deka).

“Baada ya mabadiliko tumewapatia vyumba vya kulala wanachuo 1,000 lakini uongozi wa hoteli unaeleza kuna uwezekano wa wanafunzi 2,000 kupata nafasi hivyo. Tunaendelea na maboresho,” alisema.

Alisema makubaliano ambayo wamefikia ni kuwa kwa mwaka mmoja wanafunzi watalipia Sh400,000 kwa mwaka.

Profesa Sedoyeka alisema pia wanachuo watapata sehemu ya kula hapo hapo na mazungumzo yameanza kupata madarasa kutokana na hoteli kuwa na kumbi nyingi zinazofaa kutumika kama madarasa. Pia alisema hadi jana chumba cha kompyuta kimefungwa katika hoteli hiyo, wanafunzi wanaweza kuendelea na masomo.