Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

 Jamhuri yaomba muda zaidi kesi ya Lissu, yeye alilia uchaguzi

Muktasari:

  • Lissu anakabiliwa na kesi mbili za jinai, moja ya uhaini na nyingine ya kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni.

Dar es Salaam. Upande wa Jamhuri katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, umeieleza mahakama kuwa jalada la kesi hiyo limeshaanza kupitiwa na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) na liko tayari kwa ajili ya kutolewa uamuzi, hivyo kuomba shauri lipangiwe tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Wakati upande wa Jamhuri ukieleza hayo, Lissu amelalamikia kuendelea kuwekwa mahabusu ili asishiriki uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu.

Lissu anakabiliwa na kesi hiyo pamoja na nyingine ya kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Kesi hizo, ambazo zinasikilizwa na mahakimu wawili tofauti, zimeitwa leo Julai 1, 2025, kwa hatua tofauti.

Wakati kesi ya uhaini ilipangwa kwa ajili ya kutajwa na Serikali kutoa mrejesho wa hatima ya upelelezi, kesi ya kuchapisha taarifa za uongo ilipangwa kwa ajili ya kuendelea na usikilizwaji.

Katika kesi ya uhaini, upande wa Jamhuri umeieleza Mahakama kuwa DPP ameshaanza kulisoma jalada la kesi hiyo (kupitia ushahidi uliowasilishwa na wapelelezi).

"Baada ya kusomwa na kutolewa maoni ya kisheria, jalada hili liko tayari kwa ajili ya kutolewa uamuzi," amesema kiongozi wa jopo la waendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga na kuongeza:

"Hivyo tunaomba Mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa."

Lissu anayejitetea mwenyewe katika kesi hiyo licha ya kuwa na jopo la mawakili takribani 30, ameiomba Mahakama isisikilize maombi ya Jamhuri ya kutoa ahirisho lingine, akidai hawana sababu ya msingi.

Amesema Juni 16, 2025, upande wa mashtaka uliieleza Mahakama kuwa upelelezi umeshakamilika na kwamba jalada liko kwa DPP kwa ajili ya kusomwa na kutolewa uamuzi.

"Hivyo, leo upande wa mashtaka walitakiwa waje watoe uamuzi, na si kuomba ahirisho tena," amesema Lissu na kuongeza:

"Inachukua muda gani na kwa kiasi gani kujiridhisha na upelelezi wa kesi hii ili ipelekwe Mahakama Kuu (kwa ajili ya kuanza kusikiliza ushahidi)? Na kama hawana ushahidi wa kutosha, wa-enter nolle prosequi (waliondoe mahakamani)."

Kwa mujibu wa Lissu, kifungu cha 245(4) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) kinaeleza kuwa upelelezi ukikamilika, DPP au mwakilishi wake wanapelekewa jalada la Polisi kulisoma ili kuona kama kuna ushahidi wa kutosha kumshtaki mtuhumiwa au la.

Lissu ameiomba Mahakama iwaamuru upande wa mashtaka, kama ushahidi unatosheleza wawasilishe taarifa Mahakama Kuu ili kesi ianze kusikilizwa, na kama wanaona ushahidi hautoshelezi waiondoe kesi mahakamani, na si kuahirisha tena.

"Masilahi ya umma hayahitaji shauri hili kuahirishwa ili kutenda haki. Hivyo, mamlaka aliyonayo DPP na mawakili wake yanatakiwa yafanyike leo (kutoa uamuzi). Huu ni mwaka wa uchaguzi, kiongozi mkubwa wa chama cha upinzani yuko gerezani kwa siku 90 sasa," amesema Lissu.

Amesema hata kama Msajili wa Vyama vya Siasa ana mamlaka ya kufuta chama, kwenye kipindi cha uchaguzi hawezi kukifuta, na kwamba hata kama msajili ana hoja za msingi, hana mamlaka ya kumzuia kushiriki uchaguzi.

"Sasa mwendesha mashtaka anaendelea kuniweka Gereza la Ukonga ili nisishiriki uchaguzi, mheshimiwa," amesema Lissu.


Uamuzi wa Mahakama

Akitoa uamuzi baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Hakimu Mkazi Mfawidhi, Franco Kiswaga amesema hajaelekezwa kifungu kinachoipa Mahakama mamlaka ya kutoa amri ya kumlazimisha DPP kufuta kesi au kuiwasilisha Mahakama Kuu.

Hata hivyo, ameuelekeza upande wa mashtaka kukamilisha uamuzi wa hatima ya kuendelea na kesi hiyo, ili kama wana ushahidi wa kutosha wamshtaki mshtakiwa au la, na si kuendelea kumweka mahabusu kwa muda mrefu.

Hivyo, ameahirisha kesi hiyo hadi Julai 15, 2025 kwa hatua hiyo.

Katika kesi hiyo, Lissu anakabiliwa na shtaka moja la uhaini kinyume cha kifungu cha 39(2)(d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, akidaiwa kutenda kosa hilo Aprili 3, 2025, jijini Dar es Salaam.

Anadaiwa kuwa, kwa nia ya uchochezi, alishawishi umma kuzuia kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, huku akitamka na kuandika maneno ya kumshinikiza Kiongozi Mkuu wa Jamhuri ya Tanzania.

Katika kesi ya kuchapisha taarifa za uongo, Mahakama imelazimika kusimamisha usikilizwaji wa ushahidi kutokana na Lissu kufungua mashauri mawili Mahakama Kuu dhidi ya uamuzi wa Mahakama hiyo.

Uamuzi huo umetolewa leo na Hakimu Mkazi Mkuu, Geofrey Mhina, anayesikiliza kesi hiyo, kufuatia maombi ya upande wa mashtaka.

Katika kesi hiyo, Lissu anakabiliwa na mashtaka matatu ya kuchapisha taarifa za uongo katika mtandao wa YouTube, kinyume na Sheria ya Makosa ya Kimtandao Na. 14 ya mwaka 2015, kifungu cha 16.

Kesi hiyo ilikuwa imepangwa kuanza kusikilizwa ushahidi Juni 2, 2025, lakini Mahakama hiyo ililazimika kuahirisha kutokana na maombi ya upande wa mashtaka ya kutaka kusubiri shauri la maombi madogo ya kuwalinda mashahidi katika kesi hiyo.

Lissu hakuridhika na uamuzi huo, ndipo akafungua shauri la maombi ya mapitio Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Dar es Salaam, akiomba Mahakama iitishe jalada la kesi hiyo ya msingi na kupitia mwenendo wa siku hiyo ili kujiridhisha na usahihi na uhalali wake.

Pamoja na mambo mengine, Lissu anapinga uamuzi wa Mahakama hiyo wa kukataa hoja zake kupitia mawakili wake kutaka Mahakama hiyo iwasilishe shauri Mahakama Kuu kuhusiana na madai ya ukatiba wa kifungu cha 188 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA).

Kifungu hicho, ambacho upande wa mashtaka ulikitumia kuomba ahirisho la usikilizwaji wa kesi hiyo Juni 2, 2025, alidai kuwa kinakiuka Katiba kwa kuwa kinaathiri haki zake za kikatiba za usikilizwaji sawa.

Shauri hilo lilipangwa kusikilizwa na Jaji Elizabeth Mkwizu, Juni 27, 2025, lakini Serikali iliwasilisha pingamizi la awali ikiomba Mahakama ilitupilie mbali.

Kutokana na pingamizi hilo, Mahakama ililazimika kama ilivyo utaratibu kusikiliza kwanza pingamizi hilo, na baada ya kusikiliza hoja hizo, Jaji Mkwizu alipanga kutoa uamuzi wa pingamizi hilo Julai 11, 2025.

Mbali na shauri hilo, pia Lissu amefungua shauri jingine la mapitio Mahakama Kuu, akihoji uhalali wa uamuzi wa Mahakama ya Kisutu kuruhusu baadhi ya mashahidi katika kesi hiyo kutoa ushahidi wao kwa njia ya siri, bila kuonekana wala utambulisho wao kuwekwa wazi, uamuzi uliotolewa Juni 16, 2025.

Shauri hilo, ambalo limepangwa kusikilizwa na Jaji Mkwizu, lilianza kusikilizwa Juni 27, 2025, na Jaji Mkwizu akaelekeza Jamhuri iwasilishe majibu yake Julai 8, 2025, na kupanga shauri hilo litajwe Julai 16, 2025 kwa ajili ya amri muhimu.

Kesi ya msingi, ambayo tayari imeanza kusikilizwa ushahidi, ilikuwa imepangwa kuendelea na usikilizwaji wa ushahidi leo, Julai 1, 2025.

Hata hivyo, kutokana na kuwepo kwa mashauri hayo ya Lissu Mahakama Kuu, upande wa mashtaka umeiomba Mahakama ya Kisutu iahirishe usikilizwaji wa ushahidi huo kusubiri uamuzi wa Mahakama Kuu katika mashauri yote mawili.

Kiongozi wa jopo la waendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga, amesema kuwa kwa kuwa maombi hayo yanahusu mwenendo wa kesi hiyo ya msingi, uamuzi wake kama yatakubaliwa utaathiri mwenendo wote kuanzia tarehe hiyo ya Juni 2 mpaka leo.

"Kwa sababu hizo, tunaomba Mahakama yako itumie kifungu cha 242(1) kuona kuwa sababu tulizozitoa ni za msingi, na ione kwamba si busara kuendelea na shauri wakati kuna mashauri mengine Mahakama Kuu yanayohusiana na shauri hili," amesema Katuga.


Jopo la mawakili wa Lissu ni Mpale Mpoki (kiongozi wa jopo), Dk Rugemeleza Nshala, na Peter Kibatala kwa niaba ya mawakili wote, wamepinga maombi na hoja za upande wa mashtaka.

Wamedai kuwa masuala waliyopeleka Mahakama Kuu katika mashauri yote mawili ya mapitio hayahusiani na ushahidi uliopaswa kutolewa leo.

Hivyo, wameiomba Mahakama ikatae kutoa ahirisho na badala yake iendelee na usikilizwaji wa kesi hiyo.


Kesi ya msingi

Katika kesi ya msingi, Lissu anakabiliwa na mashtaka matatu.

Kwanza, anadaiwa kumhusisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kutenguliwa kwa wagombea wa chama chake katika maeneo mbalimbali wakati wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, 2024.

Pia, anadaiwa kuwatuhumu askari polisi kuhusika katika wizi wa kura kupitia vibegi, na majaji kutotenda haki kwa madai ya kutaka wapate uteuzi wa Rais kuwa majaji wa Mahakama ya Rufani.

Anadaiwa kutenda makosa hayo Aprili 3, 2025, jijini Dar es Salaam, kwa nia ya kulaghai umma.