Kesi kupinga wito wa Spika kwa CAG kuhojiwa ilivyosajiliwa kwa ‘jasho’

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad

Muktasari:

  • Licha ya kutekelezwa kwa agizo la Spika wa Bunge Job Ndugai kwa kuhojiwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad mbele ya Kamati ya Bunge ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge, Mbunge Zitto Kabwe na wakili wake Fatma Karume, wameendelea kutaka tafsiri ya kisheria kwa kufanikiwa kusajili kwa ‘jasho’ kesi ya kikatiba, kupinga wito wa Spika kwa CAG mbele ya kamati hiyo.

Dar es Salaam. Hatimaye Mahakama Kuu imekubali kuisajili kesi ya kikatiba, kupinga wito wa Spika kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad kufika mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge ili kuhojiwa.

Jumatatu, Mahakama hiyo ilikubali kuisajili kesi hiyo iliyofunguliwa na mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe dhidi ya Spika wa Bunge, Job Ndugai, baada ya kukwama kwa wiki nzima.

Hata hivyo, usajili wa kesi hiyo haukuwa rahisi kwa kuwa hadi inasajiliwa ilimlazimu mbunge huyo na wakili wake, Fatma Karume ‘kutokwa jasho’ kwa mizunguko ya kufuatilia huku wakikumbana na vikwazo.

Zitto ambaye pia ni kiongozi wa Chama cha ACT- Wazalendo, anaiomba Mahakama Kuu itoe tafsiri ya kinga ya CAG iliyopo kikatiba na tafsiri ya Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge katika kuwashtaki watu wanaodaiwa kulidharau Bunge.

Hatua hiyo ilitokana na taarifa ya Spika Ndugai kupitia vyombo vya habari na baadaye kumwandikia barua CAG akimtaka afike mbele ya kamati hiyo ya Bunge kuhojiwa kutokana na kauli yake aliyoitoa akiwa nchini Marekani kuwa Bunge la Tanzania ni ‘dhaifu’.

Jinsi ilivyoanza

Awali, kesi hiyo iliwasilishwa mahakamani Januari 14 na wabunge watano kutoka vyama vitatu wakiwakilishwa na wakili Fatma.

Wengine walikuwa ni mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea (Chadema); mbunge wa viti maalumu Shinyanga Mjini (Chadema), Salome Makamba; mbunge wa Mchinga, Hamidu Bobali (CUF) na mbunge wa Moshi Vijijini, Anthony Komu (Chadema).

Wakili Fatma alisema walipofuatilia (Januari 15) kuona kama ilikuwa imesajiliwa, waligundua bado haijasajiliwa.

“Jumatatu (Januari 14) msajili kapewa hiyo kesi, kakaa nayo, Jumanne (Januari 15) tumepoteza muda siku nzima tunakimbizana, ni kwa nini kesi haijapokewa rasmi kupelekwa kwa Jaji Kiongozi,” alisema Wakili Fatma.

Hata hivyo, Zitto alisema kuwa Jumanne hiyo walipofika mahakamani walishangaa kuelezwa kuwa jalada la kesi hiyo lilikuwa limepelekwa kwa Jaji Kiongozi.

“Utaratibu wa Mahakama, faili linakwenda kwa Jaji Kiongozi baada ya kuwa limesajliwa na kupewa namba na kulipiwa ili lipangiwe majaji wa kuisikiliza,” alisema Zitto.

“Cha kushangaza, tulijulishwa kwamba faili hili liko mezani kwa Jaji Kiongozi wakati hatujalipa, hatujapata namba ya usajili.”

Jumatano (Januari 16) waliporudi mahakamani hapo ndipo walipoelezwa rasmi kuwa kesi hiyo haiwezi kusajiliwa, huku Mahakama hiyo ikitoa sababu mbili.

Sababu hizo kwa mujibu wa barua ya tarehe hiyo iliyosainiwa na naibu msajili aliyefahamika kwa jina la S.S. Sarwatt ni kuwa, kuna wadai wengine wanne hawakuambatanisha hati za viapo vyao katika kesi hiyo, isipokuwa Zitto pekee yake.

Sababu ya pili ni kutokuwapo kwa nakala ya wito wa Spika kwa CAG na au kutokuwapo kwa kiapo cha CAG kuunga mkono kesi hiyo.

Kutokana na hoja ya wadai wengine kutoambatanisha hati za viapo vyao, waliamua kufanya marekebisho kwa kuwaondoa wadai wengine ambao hawakuwa wameambatanisha na hivyo mdai akabaki mmoja, yaani Zitto.

Hata hivyo, waligonga ukuta baada ya naibu msajili Sarwatt kuwakatalia kutokana na kutokuwapo kwa hati ya wito wa Spika kwa CAG na kiapo chake CAG kuonyesha kuwa anaunga mkono kesi hiyo kufunguliwa.

Malalamiko kwa Jaji Mkuu

Kutokana na msimamo huo wa Mahakama Kuu kutosajili kesi hiyo waliwasilisha malalamiko yao kwa Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma, ambaye aliwashauri wamwandikie malalamiko hayo.

Jaji Mkuu aliwajibu kuwa suala hilo liko katika mamlaka ya Jaji Kiongozi na kwamba, hata huyo naibu msajili aliyekataa kuisajili kesi hiyo yuko chini ya Jaji Kiongozi.

Hata hivyo, aliwaandikia barua kumpelekea Jaji Kiongozi, Dk Eliezer Feleshi akimwelekeza alishughulikie jambo hilo.

Fatma, Zitto

Wakizungumza na waandishi wa habari baada ya kutoka kwa Jaji Mkuu, wakili Fatma na Zitto walidai kuwa naibu msajili hakuwa na mamlaka ya kukataa kusajili kesi hiyo kwa sababu alizozitoa.

“Viapo ni ushahidi. Kazi ya msajili siyo kutazama ushahidi uko vipi. Sasa ushahidi unatazamwa na jaji; na hati ya kiapo aliyotoa mheshimiwa Zitto lazima ijibiwe na Spika kama kweli alitoa ule wito au hakuutoa,” alisema Fatma.

“Sasa Mahakama inatoa uamuzi wa kesi kwamba haina ushahidi wa kutosha kabla hata ya kupelekwa mbele ya jaji. Halafu CAG siyo petitioner (mdai), siyo respondent (mdaiwa), sasa wanataka alete kiapo kui-support (kuunga mkono) petition (shauri la kikatia) isiyokuwa yake?”

Akizungumzia hilo, Zitto alisema Alhamisi iliyopita ilianza kuonyesha matumaini ya usajili wa kesi hiyo baada Mahakama Kuu kuachana na sharti la kutaka hati ya wito wa Spika kwa CAG.

Hata hivyo, baadaye waligonga mwamba baada Mahakama kubaini kuwa nakala moja kati ya saba walizokuwa wamewasilisha mahakamani hapo ilikuwa imesahaulika kusainiwa na wakili.

Wakili Fatma alilieleza Mwananchi kuwa kutokana na kasoro hiyo, naibu msajili Sarwatt aliwarejeshea nakala zote ili warekebishe kasoro hiyo.

Baadaye waliondoka wakiwa na matumaini kuwa siku inayofuata kesi hiyo ingeweza kusajiliwa baada ya kurekebisha kasoro hiyo, hasa kwa kuzingatia kwamba kikwazo kikubwa kilikuwa kimeshaondolewa.

Siku hiyo iliyofuata (Ijumaa), walipofika mahakamani hapo, wakili Fatma alisema naibu msajili huyo aliwarudisha akielekeza wafanye usajili huo kwa njia ya mtandao.

Alisema alipofika ofisini alijaribu kufanya usajili huo kwa njia ya mtandao bila mafanikio kwa kuwa mfumo wa mtandao wa Mahakama ulikuwa haufanyi kazi.

“Kwa hiyo niko hapa nimekaa tu. Wao hawataki kupokea kwa mkono na system (mfumo) yao ime-crush (haifanyi kazi), haiwezi kupokea,” alisema.

Kutokana na hali hiyo, wakili huyo alisema ameamua kufungua kesi dhidi ya Jaji Kiongozi.

“Sasa nimeamua kumshtaki Jaji Kiongozi na timu yake yaani na huyo msajili kwa kukataa kupokea hii kesi, ndiyo naiandaa hapa sasa. Nitaifungua na kama wataikataa kuisajili basi nitaipeleka Mahakama ya Afrika Mashariki,” alisema wakili huyo.

Mahakama yakubali kuisajili

Baada ya mvutano huo wa wiki nzima hatimaye Mahakama Kuu, Jumatatu (Januari 21) ilikubali kuisajili kesi hiyo.

Wakili Fatma alilieleza Mwananchi kuwa alitaarifiwa na Mahakama Kuu kuwa wameipokea kesi hiyo kwa njia ya mtandao na kwamba wamekubali kuisajili, hivyo wakamwelekeza akalipie ada ya usajili.

“Tayari nimeshalipia kabisa, sasa tunasubiri tu kupatiwa namba ya usajili,” alisema.