Kesi tano zinazomsubiri Lissu mahakamani

Muktasari:

Takriban mara nne Lissu ameshindwa kufika mahakamani kuhudhuria kesi tangu aliporejea nchini Julai 29

Dar es Salaam. Wakati aliyekuwa mgombea urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) , Tundu Lissu akidai yupo ubalozi wa Ujerumani, ameomba kupatiwa hifadhi ya kisasa kwa maelezo ya kuwa ametishiwa maisha.

Kauli hiyo imekuja wakati Mahakama ya Hakimu ya Hakimu Mkazi, ikitoa hati ya wito kumtaka Lissu afike mahakamani Novemba 30, Desemba 3, 10 na Desemba 17, kusikiliza kesi zake tano zinazomkabili.

Hii ni mara ya nne, kwa Lissu kushindwa kufika mahakamani kuhudhuria kesi hiyo, tangu aliporejea nchini Julai 29, 2020, akitokea Ubelgiji alipokuwa anapatiwa matibabu baada ya kupigwa risasi na watu ambao hadi sasa hawajafahamika.

Hadi sasa, Lissu anakabiliwa na kesi tano za jinai, zote zikiwa na mashtaka ya uchochezi na zipo kwa mahakimu tofauti.

Kesi hizo ni ya jinai namba 208/2016; 233/2016; 279/2016; 236/2017 na 123/17 zote zikiwa katika hatua ya kutajwa, kusomewa hoja za awali( PH) na usikilizwaji.

Kesi ya kwanza ya jinai namba 208 ya mwaka 2016, iliyopo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, inamkabili Lissu na wenzake watatu ambao ni Jabir Idris, Mhariri wa Gazeti la Mawio, Simon Mkina na Mmiliki wa mtambo liochapisha gazeti hilo kutoka Kampuni ya Jamana, Ismail Mehbooh.

Katika kesi ya pili ambayo Mahakama imetoa hati ya kumuita mshtakiwa huyo afike mahakamani Novemba 30, ni kesi ya jinai 279/2016, iliyopo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Godfrey Issa, yenye mashtaka ya mashtaka matatu ambayo ni kutoa maneno yenye uchochezi, kuleta chuki na kuidharau mahakama.

Pia, kesi ya tatu inayomtaka mahakamani Desemba 3, ni ya jinai namba 123/2017 iliyopo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Kassian Matembele, yenye mashtaka ya kutoa maneno ya uchochezi akiwa Zanzibar.

Katika kesi hiyo, tayari shahidi mmoja wa upande wa mashtaka ameshatoa ushahidi wake dhidi ya mshtakiwa huyo.

Wakati kesi hizo tatu, Mahakama ikitoa hati ya wito ya kumtaka Lissu, ahudhurie kesi katika tarehe zilizopangwa, kesi nyingine namba 233/2016, iliyopo mbele hakimu Mkazi Mwandamizi, Rashid Chaungu yenye shtaka la kutoa maneno ya uchochezi.

Inamtaka mshtakiwa huyo afike mahakamani Desemba 17, kusikiliza uamuzi.

Katika kesi hiyo, wakili wa Serikali mwandamizi, Wankyo Simon aliieleza Mahakama kuwa tayari upande wa mashtaka umeshafunga ushahidi wao tangu Septemba 4, 2017, na kwamba kesi iyo ilitakiwa kutolewa uamuzi Oktoba 4, 2017 kama mshtakiwa ana kesi ya kujibu au la.

Hata hivyo uamuzi huo ulishindwa kutolewa baada ya mshtakiwa huyo kushambuliwa kwa risasi na watu ambao bado hawajafahamika na hivyo kwenda nje ya nchi kwa ajili ya matibabu.

Kesi ya tano ni kesi ya jinai namba 236/2017 iliyopo mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustina Mmbando, alimtaka mshtakiwa huyo Desemba 10, 2020 awepo mahakamani ili kesi hiyo iweze kuendelea.

Kesi hiyo ina shtaka la kutoa maneno ya kuhamasisha chuki baina ya wananchi dhidi ya Serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania.