Kinara wa pombe bandia atupwa jela miaka mitano

Muktasari:

Njamasi alihukumiwa kifungo hicho mwaka jana mbele ya Hakimu Mkazi, Sophia Masati bila mtuhumiwa huyo kuwepo mahakamani, hadi alipokamatwa mkoani Dodoma wiki iliyopita.

Moshi. Kinara wa kuzalisha pombe kali bandia aina ya Kiroba Original na Konyagi, Jonathan Njamasi (30) leo ametupwa gereza la Karanga mjini Moshi akianza kutumikia kifungo chake cha miaka mitano.

Pombe hizo zilikuwa zikisambazwa katika mikoa mbalimbali nchini ikiwamo Kilimanjaro, Arusha, Babati, Singida, Dodoma, Jiji la Dar Es Salaam na mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Njamasi alihukumiwa kifungo hicho mwaka jana mbele ya Hakimu Mkazi, Sophia Masati bila mtuhumiwa huyo kuwepo mahakamani, hadi alipokamatwa mkoani Dodoma wiki iliyopita.

Wakati Njamasi  anayekabiliwa na tuhuma mbalimbali katika mikoa mbalimbali akienda jela hiyo jana, bado kifungo kingine cha miaka saba kinamsubiri mkoani Singida kwa makosa kama hayo.

Juni 30,2016 katika mahakama ya Hakimu Mkazi mkoani Singida, Njamasi alihukumiwa kifungo cha miaka saba jela kwa kosa la kukutwa na kiwanda bubu cha kuzalisha Kiroba na Konyagi bandia.

Kama ilivyokuwa katika mahakama ya mjini Moshi, wakati hukumu hiyo ikitolewa mjini Singida, Njamasi hakutokea mahakamani ambapo mahakama iliamua kutoa hukumu bila ya yeye kuwepo.

Washirika wake watano ambao ni wafanyakazi wake waliokutwa katika kiwanda hicho bubu eneo la Unyankindi mjini Singida, nao walihukumiwa kifungo cha miaka mitano jela kila mmoja.

Akimsomea hukumu yake Hakimu mkazi Mfawidhi wa mkoa Kilimanjaro, Joachim Tiganga, alikataa ombi la mshitakiwa huyo la kutaka kujitetea upya.

Mshitakiwa alitoa ombi hilo baada ya kuelezwa anatakiwa akatumikie kifungo hicho alichohukumiwa akiwa hayupo kortini, na kwamba alishapewa nafasi ya kujitetea kabla ya kuingia mitini.

Hakimu Tiganga alimweleza kuwa kabla ya kuingia mitini, alishatoa utetezi wake na ndipo Mahakama ikapanga tarehe ya hukumu hivyo hukumu hiyo imezingatia utetezi wake na ushahidi wa Jamhuri.

Katika kesi hiyo, Hakimu Tiganga alisema Njamasi alishitakiwa kuwa mwaka 2014 tarehe na muda usiojulikana, aliiba malighafi ya kuzalishia Kiroba Original yenye thamani ya Sh1 milioni.

Hakimu alisema baada ya kutoroka, Mahakama ilitoa hati ya kumkamata ili atumikie kifungo chake na kwamba wadhamini wake wanatakiwa wafike mahakamani kujieleza kwanini wasishitakiwe.