Kipimajoto cha baraza la mawaziri

Monday November 09 2020
mawaziri pic

Dar es Salaam. Kwa kutazama miaka mitano ya kwanza ya Rais John Magufuli madarakani na hatua za awali za uteuzi wake katika kipindi cha pili, si vigumu kubashiri aina ya baraza la mawaziri atakaloliunda katika siku za usoni.

Tofauti na mwaka 2015 baada ya kukaa kwa zaidi ya mwezi mmoja akilisuka baraza lake la kwanza na kisha kulitangaza, safari hii akiwa amekwishawafahamu na wengine amewaandaa mwenyewe, inaweza kumchukua muda mfupi kukamilisha safu hiyo.

Katika baraza la kwanza, Rais Magufuli alianza na mawaziri 19 katika wizara 18 na aliacha nafasi nne alizosema angeendelea kutafuta watu wanaofaa.

Licha ya kuongeza mawaziri hao wanne, ndani ya miaka mitano, Rais Magufuli aliongeza wizara kutoka 18 na kufikia 21.

Katika kipindi hicho, mbali na kuteua mawaziri wapya na kuengua wengine, wakati mwingine hata wale aliowaengua aliwarejesha, hali inayoelezwa kuwa Rais bado anaridhika na mawaziri wengi alioanza nao.

“Sitegemei kuwa na sura mpya nyingi, hasa ukitilia maanani kuwa takribani wote wamerudi bungeni, anasema Mohamed Bakari, Profesa wa sayansi ya siasa, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Advertisement

“Kama ingekuwa wengine wamekwenda kwenye uchaguzi wakashindwa pengine ingekuwa tofauti, lakini kwa mazingira ya siasa yalivyohutegemei mabadiliko makubwa,” alisema.

Alipoulizwa kuhusu uwezekano wa kuingizwa sura mpya, Profesa Bakari alisema: “Bila shaka sura mpya zitakuwepo, lakini kama unaangalia baraza ni jipya, mategemeo ni mwendelezo wa baraza lile lile kuliko mabadiliko.”

Mtazamo wa Profesa Bakari unaonekana kuwa na nguvu hasa kwa kuangalia kuwa Rais Magufuli, aliamua kuendelea na makamu wake wa Rais, Samia suluhu Hassan kama mgombea mwenza

Na hata baada ya kushinda uchaguzi, siku chache baadaye akamteua tena Profesa Adelardus Kilangi kuendelea kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali .

Vilevile Ijumaa wiki hii Kamati Kuu ya CCM iliwateua Spika anayemaliza muda wake, Job Ndugai na naibu wake Dk Tulia Ackson kuwania tena nafasi zao.

Hali hiyo ndiyo inayoongeza joto katika nafasi hizo kutokana na wanaotarajia nafasi hizo kuwa wengi wakiwamo wapya na wakongwe.

Wanaopewa kipaumbele

Baada ya Bunge ambalo litakuwa na majukumu ya kumchagua Spika, kuapishwa na kuidhinisha uteuzi wa waziri mkuu, kitakachofuata ni Rais kuunda baraza lake la mawaziri.

Miongoni mwa mawaziri wanaotarajiwa kuwamo baadhi ni wale waliodumu katika baraza lake la awali.

Miongoni mwa wanaotajwa ni mawaziri sita ambao hawakuguswa tangu walipoteuliwa mara ya kwanza. Hawa ni aliyekuwa Waziri wa Fedha, Dk Philip Mpango na Profesa Joyce Ndalichako, waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Wengine ni aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, Ummy Mwalimu (Waziri wa Afya) na Jenista Mhagama (Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-Sera, Uratibu wa Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na wenye ulemavu).

Miongoni mwa wabunge hao ambaye hawezi kurudi ni Dk Hussein Mwinyi aliyekuwa waziri wa Ulinzi ambaye sasa ni Rais wa Zanzibar.

Walioenguliwa, warudi

Orodha nyingine ni mawaziri walioenguliwa na kurudishwa baadaye katika uwaziri akiwamo Mwigulu Nchemba ambaye awali alikuwa Waziri wa Kilimo na Mifugo na baadaye akahamia Mambo ya Ndani kabla ya ya kuenguliwa Julai 1, 2018. Baadaye alirejeshwa na kuwa Waziri wa Katiba na Sheria Mei 2, 2020.

Dalili za kurudi kwa Mwigulu zinatiwa nguvu na kauli ya Rais Magufuli katika moja ya mikutano yake ya kampeni mkoani Singida ambapo alisema anataka ashinde ubunge sambamba na aliyekuwa mpinzani wake katika jimbo la Iramba, Profesa Kitila Mkumbo ambaye kwa sasa ni mbunge wa Ubungo.

“Mwigulu ninamfahamu...na Profesa Mkumbo naye nampenda, ndiyo maana nikasema huyu agombee hapa na yule akagombee Ubungo na nataka wote washinde,” alisema Rais Magufuli.

Mwingine aliyerudishwa ni George Simbachawene, mbunge wa Kibakwe ambaye wakati anajiuzulu Septemba 7, 2017 alikuwa Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais (Tamisemi) na aliporudishwa Januari 23, 2020 akawa Waziri wa Mambo ya Ndani. Wengine wanaopewa nafasi ni mawaziri walioibuka baada ya Rais Magufuli kufanya mabadiliko na kuongeza wizara.

Katika kundi hilo yumo Waziri wa Madini, Dotto Biteko ambaye ni mbunge wa Mbogwe na naibu wake Ladislaus Nyongo ambaye ni Mbunge wa Maswa Mashariki.

Pia, yuko aliyekuwa Waziri wa Madini kabla ya kuhamishiwa Wizara ya Uwekezaji katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Angela Kairuki (ambaye hakushinda ubunge), huku pia aliyekuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi Luhaga Mpina na aliyekuwa Naibu wake Abdallah Ulega nao wakipewa nafasi.

Wanaopewa nafasi ya pili

Mawaziri wengine walioenguliwa lakini wanapewa nafasi ya kuibuka katika baraza jipya ni pamoja Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye ambaye katika baraza la awali alikuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, sanaa na Michezo.

Kurejeshwa kwa Nape aliyeenguliwa mwaka 2017 baada ya sakata la kuvamiwa kwa studio za Clouds Media jijini Dar es Salaam, kunatajwa kutokana na hatua yake ya kwenda Ikulu Septemba 10, 2019 kuomba msamaha.

Mbali na Nape wengine ni aliyekuwa Waziri wa Nchi katika ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira na Muungano), January Makamba ambaye pia aliomba msamaha.

Walioko benchi

Mawaziri walioenguliwa na hawakupata ubunge ni pamoja na Charles Kitwanga aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Charles Tizeba (Kilimo) na Mhandisi Gerson Lwenge (Maji na Umwagiliaji).

Wengine ni Profesa Jumanne Maghembe (Maliasili na Utalii) na na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani Kangi Lugola na Dk Harrison Mwakyembe (Habari, Utamaduni, sanaa na Michezo).

Katika kundi hilo pia yumo Mbunge wa Muleba Kasakzini, Charles Mwijage ambaye alienguliwa mwaka 2018.

Walioibuka baadaye

Miongoni mwa mawaziri walioteuliwa katikati ya kipindi cha kwanza cha Magufuli na wanapewa nafasi kubwa kwenye baraza jipya ni pamoja na Profesa Palamagamba Kabudi aliyeteuliwa kuwa Waziri Sheria na Katiba mwaka 2017 akichukua nafasi ya Dk Mwakyembe aliyehamishiwa Wizara ya Habari.

Profesa Kabudi aliyepita bila kupingwa katika jimbo la Kilosa pia alihamishiwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akibadilishana na marehemu Dk Augustine Mahiga.

Sura mpya

Sura mpya zinazotajwa ni pamoja na Mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo ambaye hivi karibuni Magufuli alisema kuwa alimwondoa kwenye ya ukuu wa mkoa ili akagombee ubunge.

Nafasi hiyo pia anapewa Mbunge wa Misungwi na aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti na Profesa Kitila.

Kundi lingine la sura mpya ni waliokuwa makada wa vyama vya upinzani akiwamo Mbunge wa Ubungo, Kitila Mkumbo ambaye tayari Rais Magufuli alishasema ni miongoni mwa watu aliowahitaji washinde. Profesa Kitila alikuwa mwanzilishi wa chama cha ACT- Wazalendo baada ya kufukuzwa Chadema.Aliteuliwa na Rais Magufuli kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji akiwa bado mwanachama wa chama hicho kabla ya baadaye kuhamia CCM.

Wengine ni pamoja na aliyekuwa DC wa Dodoma, Petrobras Katambi (Shinyanga Mjini), aliyekuwa naibu Waziri wa Afya Dk Goodluck Mollel (Siha) na David Silinde (Tunduma), ambao wote waliondoka Chadema kwa nyakati tofauti.

Advertisement