Korti ilivyomwachia mtuhumiwa mauaji Siku ya Wapendanao
Muktasari:
- Siku hiyo, mume wa marehemu aliondoka nyumbani asubuhi kuelekea shamba na kumwacha mke wake nyumbani kwao katika Kijiji cha Buturi, Wilaya ya Butiama, mkoani Mara.
Dar es Salaam. Uhusiano wa mapenzi kati ya Mashimba Siligi na mke wa jirani yake Mecklida Hassani ulianza muda mrefu kabla ya kufikia mwisho wa majonzi Siku ya Wapendanao ya Februari 14, 2018.
Siku hiyo, mume wa marehemu aliondoka nyumbani asubuhi kuelekea shamba na kumwacha mke wake nyumbani kwao katika Kijiji cha Buturi, Wilaya ya Butiama, mkoani Mara.
Baada ya shughuli ya kutwa nzima shambani, Hassani alianza safari ya kurudi nyumbani kwake. Alipofika hakumkuta mke wake.
Mara moja alianza kumtafuta kwa majirani na sehemu nyingine bila mafanikio. Ilipofika saa 2 usiku aliamua kuwashirikisha wanakijiji wenzake ambao waliungana naye kumtafuta mke wake. Hadi ilipotimia saa 4 usiku hawakuwa wamempata. Waliamua kupumzika.
Siku iliyofuata, wanakijiji walikusanyika tena nyumbani kwa Hassani na kuendelea na kazi ya kumtafuta Mecklida. Hatimaye juhudi zao zilizaa matunda. Majira ya saa 3 asubuhi waliupata mwili ukiwa uchi kwenye kichaka, karibu na nyumbani kwake. Pembeni yake zilikutwa kondomu zilizotumika na mpya. Shingo yake ilikutwa pia na michubuko.
Hatua iliyofuata ilikuwa ni kulijulisha Jeshi la Polisi ambalo lilituma vijana wake kwa ajili ya kuchukua mwili na kuanza upelelezi wa chanzo cha kifo hicho.
Wakati hayo yakijiri, baadhi ya wanakijiji walikuwa wanafahamu kuhusu uhusiano haramu wa kimapenzi kati ya marehemu na Siligi, hivyo waliamua kwenda nyumbani kwa Siligi ambapo pia walikuta kondomu zilizotumika.
Wakizidi kuingiwa na wasiwasi juu ya uhusika wa Siligi, wanakijiji hao waliamua kumkamata na kumpeleka Kituo cha Polisi Butiama ambapo alitoa maelezo yake ya onyo juu ya nini anachojua kuhusu kifo cha Mecklida.
Baadaye Siligi alishitakiwa kwa kosa la mauaji ya Mecklida Hassani.
Alikufa tukifanya ngono
Askari polisi mpelelezi aliyejulikana kwa jina la Asukile aliiambia mahakama kuwa wakati wa mahojiano, mshitakiwa alikana kumuua Mecklida lakini alikubali kueleza nini hasa kilitokea.
Alidai mshtakiwa alimweleza kuwa yeye na marehemu walikuwa wapenzi. Alidai siku ya tukio walikubaliana kufanya ngono kama ada yao. Alidai mara ya kwanza walienda vizuri lakini walipokuwa wakifanya mara ya pili alimwona marehemu akianza kudhoofika.
Alidai alisimama kufanya ngono akiamini mwenzake atakuwa amechoka hivyo ampe muda wa kupumzika. Hata hivyo, Mecklida alizidi kudhoofika na baada ya muda mfupi alifariki akiwa mikononi mwake.
Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano kati ya mshtakiwa na askari mpelelezi:-
“Nakumbuka mnamo tarehe 14/02/2018 majira ya saa sita mchana marehemu alikuja nyumbani kwangu, nikiwa naanika mahindi, tukaingia ndani na kuanza kufanya mapenzi kitandani kwangu bila kutumia kondomu.
“Tulifanya mapenzi mara ya kwanza, tukamaliza kitendo halafu tukapumzika. Tukaanza tena mara ya pili kufanya mapenzi ndipo nilianza kuona hali ya tofauti kwa mwenzangu ambapo alianza kuwa kama ananyong’onyea tofauti na kawaida yake.
“Baada ya kuona hali ile nilisitisha kufanya mapenzi nikidhani labda tu amechoka anataka kupumzika. Hata hivyo, bado mwenzangu aliendelea kunyong’onyea na hatimaye alikata roho na kufariki dunia ndani kwangu kitandani. Baada ya kuona Mecklida amefariki dunia ndani kwangu nilikuwa kama nimechanganyikiwa….”
Ushahidi wa mume
Usikilizwaji wa kesi ya mauaji iliyokuwa ikimkabili Sigili ilipoanza, mume wa Mecklida, Hassani Nyamazazala ndiye alikuwa wa kwanza kutoa ushahidi.
Aliieleza mahakama kuwa siku ya tarehe 14 Februari, 2018 alidamka na kuelekea shambani kwao na aliporudi hakumkuta mke wake nyumbani. Alidai baada ya muda mfupi, mshtakiwa alifika nyumbani kwake na kuomba unga wa mahidi.
Hassani hakuwa na jibu lingine zaidi ya kumweleza kuwa isingewezekana kwani mke wake hakuwepo nyumbani na kumshauri asubiri hadi atakaporudi ili ampatie.
Kwa mujibu wa ushahidi, inawezekana kabisa wakati Siligi akienda kwa Hassan kuomba unga, marehemu alikuwa nyumbani kwake, hai au akiwa amekufa.
Alieleza pia jinsi walivyoukuta mwili wa mke wake ukiwa uchi huku kondomu zilizotumika na mpya zikiwa pembeni yake. Hassani aliiambia mahakama hakujua ni nani alimuua mke wake na kwamba yeye na mshtakiwa walikuwa majirani walioishi kwa uelewano mzuri.
Shahidi mwingine alikuwa ni mtoto wa marehemu, Wandiba Hassani Nyamazazala. Pamoja na mambo mengine, yeye aliiambia mahakama kuwa alikuwa akifahamu kuwa mshtakiwa alikuwa na uhusiano wa kimapenzi ya kificho kutokana na mienendo yao na kwamba baba yake hakufahamu.
Mahakama yachambua ushahidi
Ni kanuni ya msingi wa sheria jinai kwa suala la kuthibitisha shitaka siku zote itakuwa ni kazi ya upande wa mashitaka.
Katika kuthibitisha kosa la mauaji, mahakama lazima iridhike kuwa viwango vinne vya kuthibitisha kosa hilo vimefikiwa bila kuacha shaka kabla ya kumtia mshtakiwa hatiani na kumhukumu.
Kwanza, upande wa mashitaka lazima uthibitishe kuwa mtu anayedaiwa kufa amekufa kweli na pili lazima uthibitishe kuwa kifo chake hakikuwa cha kawaida.
Tatu, lazima Jamhuri ithibitishe kuwa mshtakiwa aliye mbele ya mahakama ndiye aliyemuua marehemu na nne lazima ithibitika mtu aliyefanya mauaji alidhamiria na alifanya hivyo kwa nia ya kuua au kusababisha majeraha makubwa mwilini.
Ikitokea ushahidi unaiacha mahakama na shaka yoyote kuhusu hatia ya mshitakiwa, basi mahakama lazima imwachie hata kama inaamini ana hatia.
Kisheria, hii ina maana kuwa kuachiwa kwa mshtakiwa yeyote katika kesi ya jinai hakuna maana kuwa mshtakiwa huyo hana au hakuwa na hatia bali humaanisha kuwa kesi dhidi yake haikuthibitishwa kwa viwango vinavyotakiwa na sheria na bila kuacha shaka.
Siligi aachiwa huru
Akisoma hukumu ya kesi hiyo hivi karibuni, Jaji wa Mahakama Kuu, Musoma, Merlyne Komba alisema hakuna ushahidi ulioletwa mbele yake kuonesha kulikuwa na ugomvi au kutokuelewana kati ya marehemu na mshitakiwa kabla ya kifo.
“Walikuwa wakifanya mapenzi. Hakuna uthibitisho wa silaha yoyote kutumika, hakuna nguvu iliyotumika kumdhuru marehemu, marehemu hakuwa na majeraha,” alisema Jaji Komba. Akaendelea: “Kuna ushahidi pia kuwa wakati wa usiku aliuvuta mwili wa marehemu hadi katika kichaka kilichoko karibu ambapo ungeonekana kwa urahisi asubuhi.
“Kitendo chake cha kuuvuta mwili wa mpenzi wake akitumia kamba iliyofungwa kwenye shingo yake kilisababisha michubuko kwenye shingo ya marehemu.
“Mshtakiwa hakuwa na namna zaidi ya kuuweka mwili wa marehemu ambapo wanakijiji wataupata kwa urahisi. Maelezo ya mshitakiwa pia yanaonesha kuwa hapakuwa na msuguano kati yake na marehemu na kwamba kifo kile kilitokea wakati wakifanya mapenzi. Mshitakiwa hakuwa na nia au hakudhamiria kuua kwa kuwa kitendo cha kufanya mapenzi na mtu unayempenda si kitendo cha hatari.”
Jaji Komba alisema ukitazama mazingira ya kesi hiyo, baada ya kuchambua na kupima uzito wa ushahidi uliotolewa na kukosekana kwa maoni ya mtaalamu juu ya nini hasa ilikuwa sababu ya kifo kile kuliacha pengo kubwa katika kesi ya Jamhuri, hivyo kushindwa kuthibitisha kosa la mauaji dhidi ya mshitakiwa.
“Hii ina maana haikuthibitishwa kuwa ni mshitakiwa ndiye aliyemuua marehemu kama ilivyodaiwa, kufanya mapenzi sio kitendo cha hatari kwa maisha ya binadamu,” alisema.