'Laana, kuchepuka hakusababishi mdomo sungura'

Ofisa Lishe wa Hospitali ya Bugando, Claudia Lugira akitumia mdoli kutoa mafunzo ya namna ya kumbaini mtoto mwenye ulemavu wa mdomo sungura na mdomo wazi kwa watoa huduma ya afya ngazi ya Jamii (hawapo pichani) kutoka Kata ya Bugogwa na Shibula wilayani Ilemela mkoani Mwanza. Picha na Mgongo Kaitira

Muktasari:

Kupitia mafunzo hayo yaliyotolewa leo kwa watoa huduma ya afya wa kata ya Sangabuye, Kayenze, Bugogwa na Shibula wilayani Ilemela mkoani Mwanza, Bugando imefanikiwa kuwabaini watoto nane wenye ulemavu huo.

Mwanza. Laana na kuchepuka ni miongoni mwa imani potofu zinazoaminika katika jamii kuwa zinasababisha ulemavu wa mdomo sungura na mdomo wazi kwa watoto.

Mdomo sungura na mdomo wazi ni ulemavu unaosababishwa na hitilafu ya kimaumbile ambayo mfumo wa mdomo unashindikana kuungana ipasavyo wakati wa utengenezwaji wa mtoto tumboni kisha kusababisha mpasuko ndani na nje ya mdomo wa mtoto huyo.

Ili kukabiliana na tatizo hilo, Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando leo Alhamisi, Septemba 22, 2022 imetoa elimu ya utambuzi wa watoto wenye ulemavu huo kwa watoa huduma ya afya ngazi za Jamii (CCW), 60 kutoka katika kata ya Bugogwa, Shibula, Kayenze na Sangabuye wilayani Ilemela mkoani Mwanza.

Akizungumza katika mafunzo hayo, Afisa Ustawi wa Jamii wa Hospitali ya Bugando, Gasper Mshana amesema utafiti mfupi uliofanyika kati ya Julai 2021 hadi Julai 2022 mkoani Mwanza ulibaini idadi kubwa ya watoto wanaofanyiwa upasuaji wa kutibu ulemavu huo wanatokea wilayani Ilemela mkoani hapa.

"Watoto wengi wenye tatizo hili wanafichwa katika jamii kwa hofu ya kuchekwa huku wengine wakiwa na imani potofu kwamba mtoto aliyezaliwa na ugonjwa huu mama yake alichepuka au amelaaniwa baada ya kumcheka mtu mwenye mdomo ulemavu huu, huo siyo ukweli," amesema Mshana

Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Watoto, Dk Florentina Mashuda amesema mtoto mwenye ulemavu huo asipotibiwa mapema anaweza kupatwa na ulemavu wa kusikia, kushindwa kula, utapiamlo na kushindwa kunyonya.

Ametaja visababishi vya ugonjwa huo kuwa ni pamoja na matumizi ya sigara, pombe, matumizi ya dawa asili, kutozingatia Kliniki na kutotumia dawa ya Folic Acid wakati wa ujauzito.

"Matibabu ya ugonjwa huu yanatolewa bure Bugando. Tunaiomba jamii itambue kwamba kuwaficha watoto wenye tatizo hili kunawanyima haki zao za msingi ikiwemo haki ya kupata matibabu na elimu," amesema Dk Mashuda

Kwa upande wake, Afisa Lishe katika hospitali ya Bugando, Claudia Lugira amesema hospitali hiyo pia, inatoa elimu lishe kwa kina mama wajawazito na wenye watoto walio na mdomo sungura na mdomo wazi ili kuwajengea mbinu za kuwahudumia watoto wenye tatizo hilo.

Naye, mtoa huduma ya afya ngazi ya Jamii katika kata ya Sangabuye wilayani Ilemela mkoani hapa, Lucas Guraka amesema elimu waliyoipata wataitumia kuelimisha jamii na kutembelea kaya kwa ajili ya kuwatambua watoto wenye ulemavu huo kisha kuwapeleka Bugando kupatiwa matibabu hayo.