Lukuvi akutana na ‘ugeni’ wa watu 1,000 kero za ardhi Mara

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi.

Muktasari:

  • Lukuvi alifanya ziara hiyo ya kusikiliza na kutatua kero za idara ambazo zipo chini ya wizara yake hususan ya ardhi baada ya kuagizwa na Rais John Magufuli.

Musoma. Zaidi ya watu 1,000 kutoka wilaya tatu za Mkoa wa Mara wamejitokeza kuwasilisha malalamiko ya kero za ardhi kwa waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi aliyefanya ziara ya siku mbili mkoani humo.

Lukuvi alifanya ziara hiyo ya kusikiliza na kutatua kero za idara ambazo zipo chini ya wizara yake hususan ya ardhi baada ya kuagizwa na Rais John Magufuli.

Rais alitoa agizo hilo mwanzoni mwa mwezi huu alipofanya ziara ya kikazi ya siku nne mkoani humo.

Wananchi waliowasilisha vilio vyao kwa waziri huyo wanatoka katika wilaya za Bunda, Musoma na Tarime.

Pamoja na mambo mengine, Lukuvi aliwaelekeza waende kuwaona wakuu wa wilaya husika ili kero zao zitatuliwe.

Kabla ya kuonana na waziri huyo, watu hao walijaza fomu inayoitwa ‘Funguka kwa Waziri Lukuvi kuelezea kero yako.’

Inaelezwa kuwa zaidi ya watu 800 walijaza fomu hizo katika wilaya ya Tarime huku wengine 130 wakipata fomu hizo wilayani Bunda na 70 katika Manispaa ya Musoma.

Akizungumza kwa nyakati tofauti katika wilaya hizo, Lukuvi alisema kero nyingi amezielekeza kwa wakuu wa wilaya wenye jukumu la kuzitatua kwa kushirikiana na wataalamu wa idara ya ardhi walio chini ya halmashauri wanazoziongoza.

“Hizi kero si za kuzileta kwa waziri, ni za kutatuliwa kwenye halmashauri na wilaya tu na zingechukua muda mfupi tu kutatuliwa,” alisema Lukuvi mbele ya watalaamu wa idara hiyo mjini Musoma.

“Sema ni kwa vile wengi wenu mmejisahau sana mnataka wananchi waje kuwatafuta maofisini huku mkijiona kuwa ni maofisa wa hali ya juu kiasi kwamba hamuwezi kuwatembelea wananchi huko walipo ili kuwasaidia.”

Kero nyingi zilizowasilishwa kwa waziri huyo zilihusu fidia ya viwanja, kunyang’anywa ardhi pamoja na migogoro ya mipaka baina ya kijiji na kijiji.

Lukuvi alisema kero za ardhi nyingi katika maeneo hayo zimedumu kwa muda mrefu huku watendaji wa Serikali wakishindwa kuzitatua.

Alisema kuwa zipo ambazo zimesababishwa na watendaji wa Serikali hasa wa idara ya ardhi.

Alitoa siku 90 kwa halmashauri zote za wilaya, miji, manispaa na majiji nchini kuhakikisha wanamaliza migogoro ya ardhi.

Katika ziara hiyo, Waziri Lukuvi alisema Wilaya ya Tarime inaongoza kwa kuwa na kero nyingi za ardhi huku asilimia kubwa zikiwa ni za migogoro ya mipaka baina ya vijiji na vijiji.

Kufuatia tatizo hilo, alisema wizara itatuma wataalamu wa ardhi wilayani humo kutambua mipaka ya vijiji vyote kulingana na tangazo la serikali (GN) kwa kuwa mipaka hiyo siyo siri.