Majaliwa ashangazwa na kodi Sh 150,00 sokoni

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa

Muktasari:

Amesema anatambua maamuzi ya Baraza ni ya kikao halali lakini hakubaliani na ongezeko hilo ambalo ni sawa na asilimia 650 kwani linawaumiza wananchi.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameliagiza Baraza la Madiwani la Manispaa ya Dodoma lifanye marekebisho ya kodi inayotozwa kwenye soko la Majengo ambayo imepandishwa kutoka sh. 20,000 hadi sh. 150,000 kwa mwezi.

Amesema anatambua maamuzi ya Baraza ni ya kikao halali lakini hakubaliani na ongezeko hilo ambalo ni sawa na asilimia 650 kwani linawaumiza wananchi.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumamosi, Oktoba Mosi, 2016) wakati alipotembelea soko hilo akiwa kwenye ziara ya kukagua maeneo ya kutolea huduma za jamii mjini Dodoma.

Amesema soko hilo linatakiwa lifanyiwe mapitio ili liwekwe kwenye hali nzuri na Manispaa ihakikishe maboresho hayo yanafanyika bila ya kuwaumiza wafanyabiashara.

“Kwa kuwa uamuzi wa kupandisha kodi ulifanyika kisheria na kupitishwa na baraza la Madiwani, sitaki kuvunja sheria. Nawaagiza mkazungumze tena katika baraza na muangalie namna ya kupunguza gharama hizo,” amesema.

“Hali hii haiwezekani kuachwa iendelee, huku ni kuwaumiza wananchi. Mkurugenzi wa Manispaa nenda kaitishe tena kikao, mfanye mazungumzo upya kwenye baraza lenu na mje mnieleze mmekubaliana nini” amesisitiza.

Pia ameitaka Manispaa hiyo ihakikishe makusanyo yote ya fedha katika soko hilo yanakusanywa kwa njia ya kielektroniki ili fedha hizo ziweze kuleta tija na kuwataka Mkuu wa mkoa na wilaya kuwachukulia hatua wotewatakaobainika kuiba fedha hizo.