Makonda ahojiwa kwa saa tatu CCM

Muktasari:

  • Makonda ambaye Aprili 16, mwaka huu, alitumiwa barua ya wito ikimtaka kufika mbele ya kamati hiyo Aprili 20, mwaka huu, jana Aprili 22, 2024 ndiyo alifika mbele ya kamati hiyo kwa mahojiano

Dar/Dodoma. Kamati ya Maadili ya Chama cha Mapinduzi (CCM) imemuhoji kwa takribani saa tatu Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda.

Makonda ambaye Aprili 16, mwaka huu, alitumiwa barua ya wito ikimtaka kufika mbele ya kamati hiyo Aprili 20, mwaka huu, jana Aprili 22, 2024 ndiyo alifika mbele ya kamati hiyo kwa mahojiano.

Mwananchi Digital  leo iliweka kambi kwenye ofisi za makao makuu ya CCM jijini Dodoma, ilimshuhudia Makonda akiingia kwenye ofisi hizo saa 3.15 asubuhi akiwa na gari aina ya Toyota Land Cruiser rangi ya kijivu.

Awali, haikufahamika wito wa Makonda mbele ya kamati hiyo ulihusu nini, huku ikihisiwa huenda ni kauli aliyoitoa kwenye kumbukumbu ya miaka 40 ya kifo cha Waziri Mkuu wa zamani, hayati Edward Sokoine.

Kwenye maadhimisho hayo, Makonda aliposimama kusalimia, alidai kuna baadhi ya viongozi wa Serikali wakiwamo mawaziri wamekuwa wakiwalipa watu ili wamtukane Rais Samia Suluhu Hassan kwenye mitandao ya kijamii.

“Kuna watu wanahusika na kumchafua Rais Samia kwenye mitandao ya kijamii. Nitumie fursa hii kuwaambia hasa kaka zangu, mnaotuma na kuwalipa watu kumchokoza mama yangu Ninawajua na ninyi mnanijua. Narudia tena hasa kaka zangu mnaotuma kulipa watu kumchokoza mama yangu Samia.”

“Nawajua kwa majina na leo tarehe 12 (Aprili 12, 2024), nataka iwe mwisho kuwatuma watu kwenye mitandao ya kijamii kumtuka Rais Samia na Jumatatu (Aprili 15, 2024) ikiendelea nataja majina, wengine ni mawaziri,” alisema Makonda na kuongeza:

“Naomba kukutia moyo, mimi nina mtoto wa kike na najua wengi wana watoto wa kike, wanatamani watoto wao wa kike, ikiwemo na mimi waje wasome hadithi njema za uongozi uliofanywa na kiongozi mwanamke na mahiri ambaye anaongoza Taifa hili.”

“Ulinzi wa bunduki na watu wa usalama kwa taarifa unaweza usiuponye moyo, lakini neno la uzima linalotoka kwa watumishi wa Mungu linaweza kuponya moyo wako, nakuombea kwa Mwenyezi Mungu, akupe wigo na utakaolinda moyo wako, ili ututumikie sisi Watanzania.”

Habari za kuaminika kutoka vyanzo vyetu zimeeleza, Makamu Mwenyekiti wa CCM-Bara, Abdulrahman Kinana, ndiye aliyeongoza mahojiano hayo ya Makonda akiwa na wajumbe wengine watano.

Ilielezwa Makonda alihojiwa kuhusu tuhuma hizo alizozitoa kuwa kuna viongozi wakiwemo mawaziri wamekuwa wakimchafua Rais Samia kupitia mitandao ya kijamii kwa kuwalipa watu kufanya kazi hiyo.

Chanzo hicho kilieleza wajumbe wa kamati hiyo walimtaka Makonda kuwataja viongozi wakiwemo mawaziri ambao amewatuhumu kuhusika na matendo hayo.

“Ni kweli leo (jana) asubuhi Makonda alifika hapa ofisini kwa ajili ya kuitikia wito wa kamati ya maadili. Kikao kiliketi kwa takribani saa tatu na kilikuwa cha kawaida.”

“Mahojiano yalikuwa ya kawaida lakini, kubwa Makonda alitakiwa kuwataja watu aliosema anawafahamu kwa majina kuhusika katika kumchafua Rais Samia ili chama kichukue hatua stahiki,” kilisema chanzo hicho.

Chanzo kingine kilidai Makonda hakuwa tayari kutaja majina ya wahusika, akieleza chama na Serikali kina vyombo vyenye uwezo wa kuchunguza, hivyo wanaweza kuvitumia kupata ukweli.

Chanzo hicho kilidai Makonda aliamini chama hicho kilipaswa kufungua jalada la uchunguzi na kuwaalika watu wenye taarifa kuhusu madai aliyoyatoa badala ya kumtaka yeye awataje.

“Nilimuona Makonda hapa leo (jana) kwa ajili ya kuhojiwa na kamati ya Mzee Kinana. Ila ninachofahamu ni kuwa alitakiwa kuwataja watu aliodai anawafahamu kwa majina, lakini amegoma akitaka chama kitimize wajibu wake kwa kutumia vyanzo vyake ili kupata ukweli. Kwa hiyo jamaa kagoma kutaja majina, sijajua sasa kikao kitaamua kitu gani,” kilisema chanzo kingine.

Kauli ilivyogawa makundi

Makonda ambaye kabla ya kuteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha alikuwa akihudumu kama Katibu wa NEC ya CCM, Itikadi, Uenezi na Mafunzo aliyodumu kwa miezi mitano.

Uteuzi wake huo ulikuja siku chache baada ya kutoa kauli wakati wa mapokezi ya ndege ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) aina ya Boeing 737-Max 9, ambapo Makonda aliwashukia viongozi akisema ni unafiki kumtofautisha Rais Samia na mtangulizi wake hayati John Magufuli.

Tangu wakati huo kumekuwa na mitazamo tofauti kuhusu kauli za Makonda, huku wachambuzi wa siasa wakidai kuna vita kubwa ndani ya CCM ikihusishwa na makundi ya urais.


Uhalali CCM kumhoji Makonda

Ni halali kwa kamati ya maadili ya chama hicho kumhoji Makonda, bila kujali wadhifa wake ndani ya Serikali kutoshabihiana na uongozi wa CCM.

Kinachohalalisha hilo ni uanachama wake wa CCM ambao kwa mujibu wa kanuni ya usalama na maadili ya chama hicho, kamati hiyo ina haki na wajibu wa kumhoji mwanachama yeyote iwapo atakiuka maadili.

Hata hivyo, kanuni hiyo inaeleza kuhusu tuhuma lakini haijamwelezea mtuhumu. Isipokuwa imetaja kitendo cha unafiki na kuvuruga amani ndani ya chama kama miongoni mwa makosa ya kimaadili.

Kwa kosa kama hilo, adhabu iliyotajwa kwa mujibu wa kanuni hiyo ni onyo la karipio na itakapoonekana mkosaji hajirekebishi licha ya kuadhibiwa, ataadhibiwa zaidi, ikiwemo kufutiwa uanachama.

Kosa kubwa zaidi ya yote linalotajwa ndani ya kanuni hiyo ni kukisaliti chama hicho, ambalo adhabu yake moja kwa moja ni kufukuzwa uanachama na aghalabu hutangazwa hadharani.


Mtazamo wa wadau

Hatua ya Makonda kuitwa na mamlaka hiyo ya nidhamu ya chama chake, ilitarajiwa kwa kile alichokifanya, kama inavyoelezwa na Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Mohamed Bakary.

Profesa Bakary alisema tuhuma zake dhidi ya mawaziri ni jambo baya na hakupaswa kutumia jukwaa alilolitumia kuyaeleza aliyoyaeleza.

Kitendo cha Makonda kueleza hayo mbele ya umma kimechafua taswira ya Serikali kuwa kuna mikwaruzano ndani yake, ilhali wakati wote inapaswa kuonekana ni moja.

“Ni kauli mbaya na inaonyesha hakuwa na umakini katika kuongea katika majukwaa labda kama ilikuwa na nia ya kujipatia sifa mbele ya aliyemteua,” alisema Profesa Bakary.

Kwa mujibu wa Profesa Bakary, kwa kauli hiyo, lazima angeitwa na mamlaka ya nidhamu kupitia chama chake au Serikali ili ahojiwe na aeleze.

Mwanazuoni huyo alisisitiza hata kama Makonda ana ushahidi dhidi ya alichokizungumza, bado kitendo cha kueleza hadharani ni kosa.

Waliowahi kuhojiwa      

Makonda si kiongozi wa kwanza kuhojiwa na kamati hiyo; wapo vigogo kadhaa waliowahi kupitia hayo, akiwemo Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara wa sasa, Abdulrahman Kinana.

Kinana alihojiwa pamoja na Katibu Mkuu wa zamani wa chama hicho, Yusuph Makamba kwa tuhuma za utovu wa nidhamu.

Si hao pekee, Sophia Simba akiwa Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM Taifa (UWT), alikumbana na mahojiano na kamati ya maadili yaliyohitimishwa na uamuzi wa kufukuzwa kwake.

Sophia alifukuzwa na wenzake wakiwemo wenyeviti wa zamani wa CCM wa mikoa ya Dar es Salaam, Ramadhan Madabida, Iringa -Jesca Msambatavangu, Shinyanga -Erasto Kwilasa na Mara- Christopher Sanya kwa tuhuma za kukisaliti chama hicho.