Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Makonda awataka mawaziri wa viwanda, biashara kutembelea wananchi

Muktasari:

Makonda amerudia kusema kuwa akihitimisha ziara yake ya mikoa 20 atawasilisha ripoti wa Rais Samia kuhusu utendaji kazi wa watumishi kwa kila maeneo aliyopita

Njombe. Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Paul  Makonda amemtaka Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Ashatu Kijaji na naibu wake, Exaud Kigahe kufanya ziara katika maeneo mbalimbali nchini ili kusikiliza kero za wafanyabiashara na kuzitolea ufumbuzi.

Amesema wafanyabiashara wana changamoto zinazowakabili na Rais Samia Suluhu Hassan ameteua watu wa kumsaidia katika sekta hiyo na katika ziara yake, amebaini namna kundi hilo linavyolia kutokana na kero zao kutosikiliza.

Makonda ameeleza hayo leo Ijumaa Februari 9, 2024 wakati akizungumza na wananchi wa Mji wa Makambako mkoani Njombe katika mwendelezo wa ziara yake ya mikoa 20 akitokea Iringa.

"Namtaka Waziri (Dk Kijaji) na Naibu wake (Kigahe) kufanya ziara, juzi nilisema ninyi wateule mkifanya kazi yenu, Makonda, Dk Nchimbi (Emmanuel - katibu mkuu wa CCM) na Kinana (Abdulrahman- makamu mwenyekiti CCM bara), kazi yetu itakuwa nyepesi.

"Lakini msipofanya kazi zenu mkabaki kuvizia ziara za Rais mjionyeshe pale Mama anaupiga mwingi, wakati wananchi hamuwasikilizi mnatupa tabu wakati wa uchaguzi, mawaziri wa kisekta fanyeni ziara zenu," amesema Makonda.

Amemtolea mfano Waziri wa Maji, Jumaa Aweso akisema ni kiongozi ambaye amekuwa akifanya ziara bila kuchoka ya kutatua kero zinazokabili sekta ya maji na kutoa ufumbuzi.

"Niliona clip (video), nikamuona Waziri Aweso akimhoji bosi wa maji aliyechukua Sh637 milioni za kwenda kuchimba mabwawa ya maji, akamwambia twende ukanionyeshe ulipochimba, bwawa halionekani.

"Je, Aweso angekaa ofisini angejua kama Sh637 milioni zimeliwa, angesoma kwenye taarifa akaona mambo yapo sawa, migogoro mingi tulionayo ni watu kujifungia Dodoma na Dar ea Salaam, hawafiki kwa wananchi," amesema Makonda.

"Kwa sababu mama (Rais Samia) ni mpole acha sisi watoto wake watukutu tumsaidie."

Makonda amesema wafanyabiashara wanakichangia chama hicho si kwa sababu wanakipenda bali kwa hofu ya usipotoa unaweza kuletewa vyombo vya dola ikiwamo Takukuru (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana Rushwa), polisi au Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

"Rais Samia katuonyesha kuwa watu wanatakiwa kufanya kazi kwa mambo kutoka ndani ya mioyo yao, si kwa kutishwa, kulazimishwa au kuwa na hofu ya kwamba kesho itakuwa mbaya kwako.”

Makonda amerudia kusema kuwa akihitimisha ziara yake ya mikoa 20 atawasilisha ripoti wa Rais Samia kuhusu utendaji kazi wa watumishi kwa kila maeneo aliyopita, akisema yupo tayari kuonekana mbaya kwa niaba ya watu wengine.

"Kilichopatikana kwa maombi hakifi kwa majungu, kwa wale wasiotekeleza majukumu yao siku wakiona barua ya kutenguliwa kwa maeneo aliyopita wasimlaumu Rais Samia, Makamu wa Rais (Dk Philp Mpango) au Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa)," amesema.

Mbali na hilo, Makonda amekemea baadhi ya tabia ya chama hicho kusomba watu katika mikutano akitaka iachwe ili kupima uhalali wa CCM na kukubalika kwa wananchi.

"Tusijidanganye eti wanakuja viongozi pelekeni magari, nikija hata kama kuna watu 10 acha tu nione kwamba nakubalika kwa watu wachache ili tuone tunakosea wapi," amesema Makonda.

Awali akisikiliza kero za wananchi katika mkutano huo, Makonda ameahidi kumpatia bima ya afya mwanamke mmoja ambaye jina lake halikupatikana kwa ajili ya matibabu ya mtoto wake na kumpatia mtaji wa Sh5 milioni ili afanye biashara ya kujikimu.

Mwanamke huyo amesema mtoto wake alikuwa mzima, lakini alimwachia dada yake na ndipo alipompiga na kumvinja miguu na mikono na kumpasua kichwa na pia alilawitiwa na wanaume wawili.

“Nimekaa Muhimbili kwa miezi miwili huku mtoto akiwa ICU, nimekuwa nikifuatilia haki yangu ustawi wa jamii kwa miaka mitatu na mwisho wakahukumiwa kunilipa milioni mbili 2, na kifungo cha nje miaka mitatu kwa aliyempiga mtoto,” amesema huku akilia.

Amesema amekaa miaka mitatu kwenye kituo cha watoto yatima na baadaye kuamua kuondoka kituoni hapo.

Mwanamke huo amesema fedha alizolipwa fidia alizitumia kufanya vipimo vya mwanaye na ripoti ya madaktari imeonyesha kuwa mtoto atakuwa tegemezi maisha yake yote.

 “Pole sana mama, tutamkatia mtoto bima kubwa ambayo akipata tatizo lolote atahudumiwa popote, kikubwa hao walifanya hivi ni kumuachia Mungu,” amesema Makonda.

Katika kufanikisha upatikanaji wa fedha hizo, Makonda alifanya changizo kwa viongozi mbalimbali waliokuwa wamekaa jukwaani akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Halima Dendego.