‘Mateso, vifungo, kufilisiwa vimejenga upendo Chadema’

Aliyekuwa mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema.

Muktasari:

  • Siku chache zilizopita Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimetimiza miaka 30 tangu kilipopatiwa usajili wa kudumu Januari 21, 1993.

Siku chache zilizopita Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimetimiza miaka 30 tangu kilipopatiwa usajili wa kudumu Januari 21, 1993.

Chadema kimekuwa kikiimarika kila kukicha, licha ya kupitia katika wakati mgumu katika uendeshaji wake, licha ya changamoto hizo bado kimekuwa mioyoni mwa wananchi na kimbilio la wengi.

Ni furaha kubwa kwa chama chetu, Chadema kufikisha miaka 30 kutoka kiliposajiliwa.

Ninawashukuru sana wale wote wenye maono ya umuhimu wa kupigania mfumo wa vyama vingi na demokrasia.

Miaka 30 iliyopita mimi nilikuwa bado mdogo sana. Lakini ninaweza kuwaza hali ilikuwaje nikilinganisha na sasa.Ndio sababu napata wajibu wa kufurahi na kuamini kuwa kuna watu wengi, hasa waasisi ambao majina yao pengine hatuwezi kuwataja na kuwakumbuka, lakini ustahimilivu wao na kuamini kesho bora umejenga chama imara sana nchini.

Nilikuwa mpenzi wa siasa tangu nikiwa mtoto na wakati wa harakati za Hayati Mzee Lyatonga Mrema nilijikuta nimekuwa mfuasi wa siasa zake, nikikumbuka pia Agustine Mrema alikuwa na mahusiano ya karibu na ndugu zangu wengi.

Nilikuwa nijiunge Chadema mwaka 2005 na mtu wa kwanza kunishawishi nijiunge Chadema alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Makongoro Nyerere.

Wakati huu nilikuwa nimeamua kugombea ubunge kwa mara ya kwanza kupitia TLP chini ya Agustine Lyatonga Mrema.

Makongoro alifanya jitihada na kunishawishi kujiunga na chama chenye malengo imara ya kuongoza nchi chini ya Mwenyekiti Freeman Mbowe, wakati huo sikuweza kushawishika, kwani nilikuwa nimeshajenga uhusiano wa karibu sana na TLP na ilikuwa na mtandao nzuri kisiasa Arusha Mjini kuliko Chadema wakati huo.

Nilikuwa namjua Mbowe kwa sababu tunatoka sehemu moja, lakini sikuwahi kuwa nimewaza kufanya kazi na Chadema.

Zilifanyika jitihada za mimi kuingia Chadema katika uchaguzi wa 2005, lakini ilikuwa wamechelewa ‘too late’ hata baada ya kuongea na Mwenyekiti Mbowe.

Ninaamini kabisa kuwa niliibiwa kura katika uchaguzi wa 2005 nilipogombea ubunge kupitia TLP na hivyo nilianza harakati za kujipanga kwa uchaguzi wa 2010.

Mwaka 2008 nilijiunga Chadema katika mkutano nilioundaa mwenyewe Arusha Mjini na nikapokelewa na mjumbe wa Kamati Kuu aliyekuwa ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Karatu wakati huo.

Nilipitia misukosuko mingi sana wakati nimeingia Chadema, leo sio rahisi kuisema yote hapa, lakini haikuwa rahisi kabisa hata mimi kupata tiketi ya kugombea ubunge Arusha 2010.

Tangu nimekuwa Chadema nimeshuhudia majaribu na mateso mengi sana katika ujenzi wa chama hiki, nilikuwa mjumbe wa Kamati Kuu mara tu nilipoingia bungeni na vile vile nillikuwa Waziri kivuli wa Mambo ya Ndani vipindi vyote nilivyokuwa bungeni.

Kwa hiyo naijua Chadema kiasi, viongozi wake na bidii zake.

Tumepita kwenye majaribu mengi sana, tumepoteza viongozi kwa mauti ya kulazimishwa, wengine wamefungwa, vilema na kufilisiwa.

Chadema imepita kwenye tanuru la moto kufika hapa tulipofika leo. Mafanikio ya Chadema yamejaa makovu mengi sana na kila mtu aliyelipa gharama hizi Mungu ambariki sana.

Binafsi nimepitia misukosuko mingi sana, ninaweza kusema ninaweza kuwa kiongozi namba moja wa kisiasa nchini ambaye nimepelekwa mahakamani na polisi mara nyingi pamoja na viongozi na wanachama na wafuasi wetu wengi, hasa katika miaka 7 iliyopita.

Jambo moja muhimu sana kujifunza Chadema ni ushirika wa wanachama na viongozi katika maono tuliyonayo.

Silaha yetu kubwa ni sifa moja aliyonayo Mwenyekiti Mbowe ya kusikiliza bila kuchoka na kukaa kimya wakati wa dhoruba, hii ni nguvu kubwa sana ya Mwenyekiti Mbowe katika uongozi wake Chadema.

Sidhani kama kurasa za gazeti zinaweza kunipa nafasi ya kuandika mengi, lakini niseme majaribu, mateso, vifungo, jela na mahabusu na kufilisiwa vimejenga zaidi upendo miongoni mwetu na kutufikirisha wajibu wa kazi hii ya kupigania demokrasia ni endelevu na daima..

Nawapongeza viongozi wenzangu wote kuanzia chini mpaka juu kwa kuweza kuvuka vikwazo katika nyakati zote ngumu na hata leo tunafikisha miaka 30 tukiwa na nguvu na muasisi wetu Mzee Edwin Mtei akiwa hai na mwenye afya.

Mungu ibariki Tanzania ,Mungu ibariki Chadema