Muliro ndani, mapokezi ya Lissu

Muktasari:

  • Ni mabadiliko ndivyo unavyoweza kusema hivyo, baada ya Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, kuwa miongoni mwa maofisa wa polisi walioshiriki kuimarisha ulinzi kwenye mapokezi ya Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu.

Dar es Salaam. Ni mabadiliko ndivyo unavyoweza kusema hivyo, baada ya Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, kuwa miongoni mwa maofisa wa polisi walioshiriki kuimarisha ulinzi kwenye mapokezi ya Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu.

Ilikuwa nadra katika kipindi cha miaka saba iliyopita kushuhudia ofisa wa polisi ngazi ya mkoa akiwa miongoni mwa wanaosimamia ulinzi katika mkutano wa kiongozi wa upinzani.

Badala yake, waliokuwepo ni askari kadhaa ambao hata hivyo, walitazamwa kwa jicho la chuki kutokana na vitendo vya uvunjaji haki za wananchi walivyokuwa wanadaiwa kuvitenda.

Leo, Januari 25, 2023 Muliro ni miongoni mwa maofisa walioonekana kuimarisha ulinzi wakati Lissu alipofika katika uwanja wa Bulyaga wilayani Temeke, uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) baada ya kuwasili kutoka Ubelgiji alikoishi tangu mwaka 2018 alikokwenda kwa matibabu na baadaye kuishi nchini humo.

Lissu aliondoka nchini kwa mara ya kwanza aliondoka nchini Septemba 7, 2017 baada ya kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 na watu wasiojulikana akitoka kuhudhuria vikao vya Bunge ambapo alikimbizwa katika hospitali ya Rufaa ya Dodoma na kisha kukimbizwa jijini Nairobi nchini Kenya.

Januari 6,2018 alihamishiwa nchini Ubelgiji kwa matibabu zaidi hadi Julai 27, 2020 aliporejea nchini na kuwania urais lakini alishindwa na mgombea wa CCM, John Magufuli.

Hata hivyo Novemba 10, 2020, baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu, Lissu aliondoka nchini kwenda Ubelgiji kwa madai ya kutishiwa usalama wake.


Alichokifanya Muliro

Tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma kati ya polisi na wafuasi wa vyama vya upinzani, leo mkuu huyo wa polisi katika Mkoa wa Dar es Salaam alionekana akisalimiana kwa kukumbatia na kupungiana mikono na wafuasi wa Chadema akiwemo Lissu.

Kama alivyouliza alipofika tu Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kuhusu yuko wapi Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Lissu akirudia kufanya hivyo hata alipofika katika viwanja hivyo.

"Mwenyekiti yuko wapi?" aliuliza Lissu muda mchache kabla ya Mbowe kuwasili viwanjani hapo dakika chache baadaye.

Si hayo tu, jingine la tofauti ni wimbo wa taifa kuimbwa katika mkutano huo, jambo ambalo aghalabu halifanyiki na linapofanyika huingizwa kipengele cha 'Mungu ibariki Chadema'.