VIDEO: Lissu awasili Tanzania, mamia wampokea

Muktasari:

  • Shamra zatawala nje ya lango kuu la kuingia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere muda mfupi kabla ya Lissu kuwasili.

Dar es Salaam. Makamu Mwenyekiti wa Chadema-Bara, Tundu Lissu amewasili leo Jumatano, Januari 25, 2023 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere akitokea Ubelgiji.

Katika uwanja huo, Lissu mzaliwa wa Kijiji cha Mahambe, Wilaya ya Ikungi, Mkoa wa Singida amepokewa na viongozi na wanachama wa Chadema.

Mamia ya wafuasi wa Chadema wamekusanyika nje ya lango hilo wakiimba na kucheza huku vigoma vikipigwa pamoja na mavuvuzela.

Mbali na ngoma pia zipo bodaboda zilizopambwa kwa bendera za Chadema zikisubiri msafara wa kiongozi huyo wa upinzani.

Lissu awasili Tanzania, mamia wampokea

Hata hivyo, Jeshi la polisi limeimarisha ulinzi na kuhakikisha wafuasi hao hawaingii ndani ya eneo la uwanja na badala yake wanabaki nje ya lango kuu pembezoni mwa barabara ya Nyerere.

Wakizungumza na Mwananchi Digital wafuasi hao wamesema wanaona furaha kurejea kwa kiongozi huyo kwani wanaamini ataleta mabadiliko kwenye siasa za Tanzania.

 "Tunafurahi kurudi kwa Lissu, anarudi wakati sahihi ambao mikutano imeruhusiwa tunaamini tukishirikiana ataleta mabadiliko kwenye siasa Tanzania," amesema Joseph Mwaipaya ambaye ni mwananchama.

Elizabeth Mwaikenda ambaye ni mwanachama kutoka Mbeya amesema anaona furaha kurejea kwa kiongozi huyo hivyo anaamini ni wakati sahihi nchi kupata mabadiliko.

"Najisikia raha sana pamoja na kufunga safari kutoka Mbeya Polisi wametuzuia kuingia uwanjani, kwa umati huu naamini atakapofika itakuwa kama 2020, ambapo polisi walishindwa kutuzuia waache watu waonyeshe furaha zao," amesema Mwaikenda.