Matukio 12 yaliyotikisa upande wa Burudani Bongo 2020

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

MWAKA 2020 unaelekea kukita nanga, imekuwa ni safari ndefu yenye milima na mabonde, mafupi na marefu, furaha na huzuni katika kiwanda cha burudani Bongo, lakini ni yapi hasa ya kukumbukwa? Ukihesabu kwa haraka ni kwamba zimesalia wiki tatu kamili kabla ya 2020 haujasepa zake ili kuupisha 2021.

MWAKA 2020 unaelekea kukita nanga, imekuwa ni safari ndefu yenye milima na mabonde, mafupi na marefu, furaha na huzuni katika kiwanda cha burudani Bongo, lakini ni yapi hasa ya kukumbukwa? Ukihesabu kwa haraka ni kwamba zimesalia wiki tatu kamili kabla ya 2020 haujasepa zake ili kuupisha 2021.

Kama kawaida ya Mwanaspoti kukuletea makala maaalumu za matukio mbalimbali yaliyojiri ndani ya mwaka mzima, leo tumeanza na kwenye anga za burudani kuangazia matukio 12 yaliyotikisa katika fani hiyo nchini 2020.

1. Albamu ya Harmonize

Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Jayaka Kikwete ndiye alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa albamu ya Harmonize uliofanyika ukumbi wa Mlimani City, Machi 14 mwaka huu. Ulikuwa si ugeni mzito kwa Harmonize pekee yake, bali kwa tasnia nzima ya burudani nchini, basi uzinduzi huo ukafana na kugonga vichwa vya habari kila kona.

Albamu hiyo ya kwanza kwa Harmonize inakwenda kwa jina la Afro East ambayo ina nyimbo 18 alizowashirikisha wasanii kama Burna Boy, Mr. Blue, Lady Jaydee, Morgan Heritage, Khaligraph Jones, Phyno, Skales, Yemi Alade, Mr. Eazi, Falz na DJ Seven.

Haikuchukua muda Afro East ikafutwa kwenye mitandao mikubwa ya kuuza na kusikiliza muziki duniani kama Tidal, Amazon, Deezer, Yandex na YouTube Music kitu kilichoibua mijadala la hisia za hujuma.

Iliporejea kwenye mitandao hiyo wimbo uitwao Your Body ambao amemshirikisha Burna Boy kutokea Nigeria haukuwepo. Ikumbukwe wimbo huo umechukua vionjo kutoka kwenye wimbo wa Hayati Papa Wemba uitwao Show Me the Way, inaaminika kuwa sababu ya kuondolewa kwa wimbo huo ni suala la hakimiliki na ndio ulioleta zahama yote hiyo.

2. Ujio wa Zuchu

Itoshe kusema haikuwahi kutokea msanii kuingia kwenye Bongo Fleva na kupata mafanikio makubwa kwa kipindi kifupi kama Zuchu, ndani ya miezi minane ya kusikikika kwake thamani yake ni Sh20 milioni kutumbuiza kwenye shoo moja pekee. Hiyo ni kwa mujibu wa lebo inayomsimamia, WCB Wasafi. Usiku wa Aprili 8 mwaka huu ndipo alipotangazwa kuwa chini ya WCB na kufanya lebo hiyo kuwa na wasanii wawili wa kike baada ya Queen Darleen. WCB ilikuwa hajamsaini msanii mpya kipindi kirefu kidogo, mara ya mwisho kufanya hivyo ilikuwa January 28, 2018 ambapo walimsaini Mbosso aliyewika vilivyo akiwa na Yamoto Band.

Mafanikio ya Zuchu yalionekana mapema pale alipoachia Extended Play (EP) inayokwenda kwa jina la I Am Zuchu ikiwa na nyimbo tano, huku Mbosso na Mama yake mzazi, Khadija Kopa wakiwa ndio wasanii pekee waliyoshirikishwa.

Baada ya mafanikio makubwa ya EP hiyo, Zuchu alifanya shoo kubwa Mlimani City Dar es Salaam Julai 18, mwaka huu kuwashukuru mashabiki kwa mapokezi, huku kwa mara ya kwanza akitumbuiza jukwaa moja na Lady Jaydee. Siku iliyofuata alizawadia gari jipya aina ya Toyota Vanguard na bosi wake, Diamond kama pongezi ikiwa ni miezi mitatu tangu kusainiwa WCB.

Ikumbukwe kwa sasa Zuchu ndiye msanii wa kike anayeongoza Afrika Mashariki kwa kuwa na wafuatiliaji wengi (subscribers) kwenye mtandao wa You Tube akiwa nao zaidi ya laki 6, pia ameweza kushinda tuzo ya African Muzik Magazine Awards (AFRIMMA) kama

msanii bora anaechipukia.

3. Mwana FA bungeni

Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 28, mwaka huu ulimuwezesha msanii wa Bongo Fleva, Hamis Mwinjuma ‘Mwana FA’ kuingia bungeni kwa mara ya kwanza akiwa mbunge wa Handeni. Sio Mwana FA pekee kutoka kiwanda cha burudani Bongo aliyeingia bungeni mwaka huu, kuna Khadija Shaaban ‘Keisha’ pamoja na Meneja wa Diamond na Tip Top Connection, Hamis Shaaban Taletale ‘Babu Tale’.

Ushindi wa Mwana FA ulikuwa ukingojewa na wengi kwa namna alivyojipambanua kimuziki tangu aanze kusikika zaidi ya miaka 18 sasa. Rapa huyo aliyegombea kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) alipata kura 47,578, huku aliyemkaribia Chadema, Yosepher Komba akipata kura 12,036.

Ikumbukwe Mwana FA anakuwa msanii mwingine wa Hip Hop kuingia bungeni kwa kura za wananchi baada ya Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ (Mbeya mjini) na Joseph Haule ‘Prof. Jay’ (Mkumi) ambao hata hivyo wame-shindwa mwaka huu.


4. Kofia za JPM

Wasanii wengi walipata nafasi ya kushiriki kwenye kampenzi za uchaguzi Mkuu za CCM ambapo Rais John Magufuli alianzisha utaratibu wa kuwavisha wasanii kofia pindi wanapomaliza kutoa burudani.

Diamond ndiye alikuwa wa kwanza wa Bongo Fleva kumvishwa kofia katika uwanja wa CCM Kirumba Septemba 7 mwaka huu.

Baadhi ya wasanii waliovishwa kofia ni Mrisho Mpoto, Harmonize, Alikiba, Meja Kunta, Dulla Makabila, Mbosso, Zuchu, Nandy, Rayvanny, Kala Jeremiah na Snura.

5. Pira Biriani na Sebene

Mwaka huu lile pira biriani lilipata nafasi ya kukutanishwa na sebene la maana kutoka kwenye Bongo Fleva, Diamond na Harmonize ndio waliosimamia mchongo mzima kuanzia studio hadi uwanjani.

Diamond alikuwa ni miongoni mwa wasanii waliotumbuiza Simba Day katika Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam hapo Agosti 22 mwaka huu. Naye Harmonize alikuwa upande wa pili, Yanga ambapo alitumbuiza kwenye Kilele cha Wiki ya Mwananchi, Agosti 30 mwaka huu. .

6. Nandy pete kidoleni

Aprili 10, mwaka huu Billnass alipiga goti na kumvisha Nandy pete ya uchumba baada ya kuwepo tetesi za muda mrefu kuwa wawili hao ni wapenzi. Tukio hilo lilikuwa Mubashara kwenye shoo ya Homa inayoruka TV E Tanzania ambapo siku hiyo ilikuwa ni zamu ya Nandy kutumbuiza.

Hayo yalijiri baada ya mwaka jana Nandy na Billnass kutoa wimbo wa pamoja unaokwenda kwa jina la Bugana, ukiwa ni wimbo wa pili kufanya pamoja mara baada ya Nandy kufanya ‘back vocal’ za wimbo wa Billnass uitwao Sina Jana, kwa sasa wanatamba na wimbo wao mwingine, Do Me.

7. Ujio wa Zari Bongo

Usiku wa Novemba 5, mwaka huu mrembo Zari The Bosslady alitua nchini akiongozana na watoto wake wawili, Tiffah na Nillan wakitokea Afrika Kusini wanapoishi. Zari aliwaleta watoto kwa ajili ya kuonana na baba yao, Diamond Platnumz baada ya zaidi ya miaka miwili bila kuonana kutokana na wazazi hao kuachana.

Ujio wake ambao tayari ulikuwa umetangazwa hapo awali, ulikuwa ukingojewa na wengi kutokana na nguvu yake ya ushawishi hasa kwenye mitandao ya kijamii.

Ikumbukwe Zari alitangaza kuachana na Diamond Februari 14, 2018 ambayo ilikuwa ni siku ya wapendanao (Valentine’s Day), sababu ya kuchukua uamuzi huo alieleza ni kuchoshwa na habari za kusalitiwa, na kubwa zaidi ni kitendo cha Diamond kwenda kuzaa nje ya penzi lao.

Ndani ya Dar es Salaam, Zari alikatiza mitaa mbalimbali akiongozana na Diamond, kubwa zaidi ni pale Novemba 7 walipoonekana wote Uwanja wa Mkapa kushuhudia mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL) kati ya Simba na Yanga uliomalizika kwa sare ya goli 1-1.

8. Mtikisiko Kings Music

Tunaweza kusema ni mtikisiko kwa Alikiba pale wasanii wawili wa lebo yake ya Kings Music walipotangaza kujitoa. Cheed na Killy walitangaza kuondoka katika lebo hiyo asubuhi ya Aprili 14, mwaka huu.

Ilikuwa ni habari ya kushtusha kwani hakukuwa na tetesi za wao kuondoka na ndio kwanza walikuwa wameanza kupata mafanikio kupitia lebo hiyo. Killy na Cheed ni miongoni mwa wasanii wa awali waliotambulishwa katika Kings Music mwanzoni mwa Oktoba 2018. Usiku wa Septemba 8 Harmonize ambaye ni mmiliki wa lebo ya Konde Music Worldwide alitangaza kuwasaini Killy na Cheed katika lebo yake hiyo ambayo imeanza kazi mwaka huu. Pia Harmonize mwaka huu amewasaini wasanii wengine kama Country Boy na Skales kutoka Nigeria.

9. Kipigo cha Shilole

Julai 8, Shilole alijitokeza kwenye mitandao na kudai kuwa amekuwa akipokea vipogo vya kutisha kutoka kwa mumewe, Ashiraf Geuza maarufu kama Uchebe. Katika ujumbe ambao aliuchapisha kwenye ukurasa wake wa Instagram alidai Uchebe amekuwa akimpiga mara kwa mara hadi kulazwa hospitali.

Wawili hao walifunga ndoa Desemba 2017 mara baada ya kukutana kwa mara ya kwanza visiwani Zanzibar kwenye sherehe ya siku ya kuzaliwa ya mwimbaji


Linah. Shilole aliiambia Clouds TV kuwa sababu ya kupigwa hadi kulazwa hospitali ni baada ya kumuuliza mume wake kuhusu habari zinazodai amezaa na dada mmoja maeneo ya Afrikana Dar es Salaam, lakini jibu alilopatiwa halikuwa na staha.

Hata hivyo Uchebe alikanusha kutenda kosa hilo kwa kudai picha alizoweka Shilole mtandaoni zikionyeshwa kupigwa ni za muda mrefu. Kwa sasa kila mmoja ana maisha yake, ingawa wamekuwa wakitupiana sana vijembe kwenye mitandao ya kijamii.

10. Vanessa Mdee ang’atuka

Juni 19, Vanessa Mdee alitangaza kuachana na muziki wa Bongo Fleva akiwa nchini Marekani ambapo anaishi na mpenzi wake, Rotimi ambaye ni mwanamuziki.

Vanessa alieleza sababu ya kufanya hivyo ni kutokana muziki kumfanya kuishi maisha mabaya kama ulevi wa kupindukia, uongo mbele ya vyombo vya habari na mitandao na kutopata kama alivyowekeza.

11. S2kizzy avamiwa

Tunaweza kusema ni mwaka ambao Prodyuza S2kizzy hawezi kuusahau katika maisha yake ya kuandaa muziki, ni baada ya kuvamiwa studio na watu wasiojulikana na kumpiga akiwa na wenzake kisha kumpora na kuharibu baadhi ya mali. Hiyo ilikuwa ni usiku wa kuamkia Oktoba 15 akiwa studio anayoimiliki inayokwenda kwa jina la Pluto World inayopatikana Sinza Lion Jijini Dar es Salaam.

Ikumbukwe Prodyuza S2kizzy amefanya kazi na wasanii wengi kwa mafanikio makubwa baadhi yao ni Country Boy, Weusi, OMG Tanzania, Jux, Vanessa Mdee, Lulu Diva, Moni Centrozone, Diamond na Rayvanny.

12. B Dozen, Lil Ommy na Jonijooo

Mwaka huu baadhi ya watangazaji wakubwa upande wa burudani Bongo wamehama vituo vya kazi na kwenda sehemu nyingine.

Juni 3, Hamisi Mandi maarufu kama B Dozen alijiunga E FM na TV E Tanzania akitokea Clouds FM alipokuwa akitangaza kipindi cha XXL alikofanya kazi kwa miaka 14.

Kabla ya hapo, Machi 30 mwaka huu Omary Tambwe maarufu kama Lil Ommy alijiunga na Wasafi Media mara baada ya kuondoka Times FM. Alijiunga na Wasafi akiwa na mwenzake, Mwanadada Ammy Gal waliyekuwa wanatangaza wote kipindi cha The Playlist kilichokuwa kikifanya vizuri.

Naye Jonijoo ambaye alikuwa anafanya kazi Wasafi Media, aliondoka kwenye kituo hicho Aprili 29 na kujiunga na E FM.