Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mgawo wa maji wapoa wa umeme ukitikisa

Dar/mikoani. Wakati mgawo wa maji ulioanza mwezi uliopita ukipungua jijini Dar es Salaam, maumivu bado yanaendelea baada ya mgawo wa umeme kushika kasi.

Kwa siku kadhaa sasa kilio cha wakazi wa jiji hilo kimehamia kwenye umeme unaoelezwa kukatika mara kwa mara hivyo kukwamisha shughuli zao za kiuchumi, hali iliyojitokeza kwa siku kadhaa sasa katika mikoa ya Kilimanjao, Arusha na Tanga kutokana na kupungua kwa maji katika vyanzo vya uzalishaji.

Miongoni mwa wanaoathirika zaidi na mgao huo ni wamiliki wa saluni, waosha magari, watengeneza juisi, wauza samaki wabichi hata vibanda vya kuonyesha mpira kipindi hiki cha michuano ya kombe la dunia iliyoanza nchini Qatar.

Hata hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Maharage Chande alipozungumza na wahariri wa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki kueleza mikakati waliyonayo aligusia mgao unaoendelea.

Chande alisema mgao uliopo umesababishwa na ukame ila mafundi wapo kazini kufanya ukarabati ili ikifika Januari kuwe kumetulia.

“Tunashukuru mwaka huu hali ya kukatika umeme sio mbaya sana kama ilivyokuwa kipindi kama hiki mwaka jana,” alisema.

Chande aliwataka wananchi kuelewa kuwa kunapokesekana umeme hata wao wanaumia lakini kuna mipango ya kuwapa huduma hiyo.

Kuhusu mgao katika kipindi hiki cha michuano ya kombe la dunia, Chande aliyetimiza mwaka mmoja tangu ateuliwe alisema “hili tutaliangalia ili kuwawezesha wapenzi wa mpira kushuhudia michuano hiyo mikubwa duniani.”

Jana, gazeti hili lilizungumza na wananchi katika mikoa yenye mgawo wwalioeleza machungu wanayokutana nayo hivi sasa.

Mary Mtweve, mfanyakazi wa saluni eneo la Toangoma wilayani Temeke alisema mgao wa umeme unaoendelea unamkwamisha kazini.

“Kwa kweli hali ni mbaya, yaani unashinda saluni umelala tu. Umeme unakatika kuanzia saa mbili asubuhi na unarudi saa mbili au saa moja usiku, biashara gani utaifanya muda huo wakati kila mtu yupo nyumbani kwake,” alisema Mary.

Hata Stanley Michael, mtengenezaji wa mageti eneo la Tabata, Dar es Salaam alisema ameanza kupoteza imani ya wateja wake kwa kushindwa kukamilisha kazi kwa wakati kwa kukosa umeme.

Mmiliki wa mashine za kusaga nafaka katika Mji wa Vwawa mkoani Songwe, Esta Msauye alisema kukosa umeme kunamkosesha biashara pale hasa unapokatika mchana kutwa na kurudi usiku wa manane.

Mkoani Mbeya, wafanyabishara wa maziwa ya mtindi na samaki wabichi walisema kukatika kwa umeme kumechangia kupunguza ubora wa bidhaa na kuwasababishia hasara.

Tamali John, mfanyabishara wa maziwa katika Soko la Mabatini alisema “kuna bidhaa zinazohitaji kuwekwa kwenye ubaridi kwa muda mrefu, sasa kukosa umeme kwa siku nzima kunatuathiri.”

Mkoani Njombe, vinyozi na wauza ice cream walisema mgao wa umeme umewasababishia hasara.

Kinyozi Faraja Lugome alisema hali si rafiki na ikiendelea hivi atalazimika kufunga ofisi kwani hafanyi kazi na kuingiza kipato.

“Kwa siku nilikuwa nanyoa watu wanane na kuingiza Sh20,000 lakini sasa hivi biashara imekuwa ngumu,” alisema kinyozi huyo.

Mfanyabishara wa ice cream, Salina Zenda alisema kutokana na changamoto iliyopo amekuwa akipata hasara ya kati ya Sh50,000 mpaka 60,000 kwa siku.

Mgao wa maji wapungua

Wakati mgao wa umeme ukianza kushika kasi, ule wa maji umeanza kupungua na wafanyabiashara wanaoyategemea wakifichua adha waliyopitia.

Mgao huo ulioanza mwezi uliopita ulitokana na kupungua kwa kina cha maji katika Ruvu hivyo kuilazimu Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa) kufufua visima vikiwamo vya Kigamboni na kuyaingiza kwenye mfumo.

“Mgao umepungua sasa, wiki mbili zilizopita upatikanaji wa maji ulikuwa mgumu na bei ya dumu la lita 20 ilifika Sh700 mpaka Sh1,000,” alisema Anitha Maira mkazi wa Tabata Bima jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya madereva bodaboda walinufaika na mgawo huo wa maji. Maulid Juma wa Ubungo Kibangu alisema “nilikuwa naingiza hadi Sh30,000 kwa siku kwa kuwachotea watu maji na pikipiki, niliweza kusomba madumu matano hadi sita kwa mara moja.”

Wafanyabiashara wanaotegemea maji katika shughuli zao wanasema walipitia kipindi kigumu mno.

Imendaliwa na Elizabeth Edward, Imani Makongoro, Nasra Abdallah, Baraka Loshilaa (Dar), Hawa Mathias (Mbeya) Seif Jumanne (Njombe) na Stephano Simbeye (Songwe.)