Miaka 20 ya Mapanga akiuza mapanga mitaani

Muktasari:

  • Licha ya kutaka kuzungumza nae kwa zaidi ya miezi mitatu iliyopita nilishindwa, kwa sababu haikuwa rahisi kukutana Oscar Abbas, maarufu kwa jina la ‘Mapanga’ au Oscar.

Iringa. Licha ya kutaka kuzungumza nae kwa zaidi ya miezi mitatu iliyopita nilishindwa, kwa sababu haikuwa rahisi kukutana Oscar Abbas, maarufu kwa jina la ‘Mapanga’ au Oscar.

Yeye mwenyewe anajiita Abbas Tagalile, japo watu wanaomzunguka wanasema jina hilo pia sio halisi.

Mapanga hamiliki simu mkononi ya mkononi, hana mpango huo na hakuna eneo unaloweza kwenda ukampata kirahisi zaidi ya kumvizia barabarani.

Kwa kawaida hapiti njia moja, kila anapoamka huwa na ratiba ya kupita eneo, mtaa au kata nyingine lakini sio ile aliyopita jana na juzi.

Aina yake ya uvaaji na namna anavyobeba Mapanga, imewafanya watu wengi kumuogopa na wengine huwa wanalazimika kukwepa njia wakimpisha apite na kwenda zake.

Hakuna mkazi wa Iringa asiyemfahamu Mapanga. Mara nyingi haongei na huku mwendo wake kama wa kijeshi.

Hacheki wala hatabasamu, yeye huangalia anakoenda tu jambo linalofanya watu kujiuliza, ni muda gani Mapanga huwa anauza bidhaa yake.

“Nauza sana tu ningekuwa siuzi ningeishije? Kwa siku naweza kuuza mapanga mawili au matatu na maisha yanaenda,” anasema Mapanga.

Japo awali nilihofia kukutana nae, lakini hofu ilipotea siku nilipokutana nae.

Haikuwa kazi ngumu kwangu kumsimamisha nikitaka kuongea na Mapanga.

Hapa ilikuwa ni kando ya barabara kuu ya Iringa – Dodoma eneo la Kihesa Kilolo.

Kaka habari za leo? Nilimuamkia huku nikimsogelea. Nzuri tu dada, karibu! Alinijibu huku akinitazama usoni.

Wakati huo wote, hakuwa anatabasamu lakini alisimama akijua nataka kununua mapanga yake.

Ilibidi niulize bei kabla sijaanza kuongea nae. Samahani, mapanga bei gani? Nilimuuliza huku nikiyatazama.

“Unataka mangapi? Nauza Sh12,000/= lakini bei inapungua. Unataka panga lipi kati ya haya, chagua tu,” anasisitiza.

Nilinunua panga moja, kisha nikaomba kukutana nae siku ya pili kama angepata nafasi.

Kwa sababu watu wengi huamini Mapanga ni mgonjwa wa akili, nilijua wazi kama tungepanga kukutana siku ya pili asingefika au angekataa.

Kwa mara ya kwanza niliona tabasamu la Mapanga. Ilibidi name nitabasamu, nikiamini atakubali ombi langu.

Oooh usijali, tunaweza kukutana. Kwanini unataka kukutana na mimi na wapi unataka tukutane?

Jibu lake lilifanya nigundue hayupo kama watu wanavyo mzungumzia.

Aina yake ya uvaaji huwa inawafanya watu waamini wakati wowote jamaa huyo anaweza kuwacharanga mapanga ndio maana wengi huwa wanamkwepa.

Wengine wanadhani kuna kazi maalum anaifanya kutokana na aina yake ya uuzaji wa mapanga ya kuzunguka mji mzima.

Mimi ni mwanahabari, nafanya kazi Mwananchi nilitaka tuongee mawili matatu kuhusu maisha yako, utakubali kuzungumza na mimi?

Nilijieleza kwa Mapanga. “Sawa, hakuna shida saa tatu kamili kesho tukutane. Usikose,” akanisisitiza.

Kwa sababu ilikuwa ni eneo la barabara kuu, watu waliokuwa wanapita walishangaa kuona nazungumza na mtu ambaye wengi huwa wanamkimbia.

Wengine walinicheka wakasema, dada na wewe umekuwa mwehu siku hizi?

Sikujali kama Mapanga asivyojali. Siku ya kwanza kukutana nae Ilikuwa Jumapili saa nane mchana, hivyo tuliaganaa na kila mmoja akaondoka tukipanga kukutana siku inayofuata, karibu na msikiti wa Kihesa eneo la Umati.

Japo nilitoka nyumbani saa 3.00 na kufika eneo la tukio saa 3.05 yeye alikuwa amefika na alisimama akitazama huku na kule kuona kama name natokea.

Nilimsogelea kisha nikamwamkia. “Nimekuwahi sana, saa 2.56 nilikuwa hapa nakusubiri. Mbona umechelewa?” aliniuliza na alikuwa akitabasamu, jambo lililonipatia nguvu zaidi ya kuzungumza nae.

Niliomba msamaha nikijitetea kwa dakika tano nilizokuwa nimechelewa.

Tuliketi kwenye msingi wa daraja na hapo mazungumzo yetu yalianza rasmi nikijitambulisha upya kwake.

Mwandishi: Naomba kujua majina yako halisi?

Mapanga; Mimi naitwa Abas, wengine wananiita na kuna watu wananiita Oska. Mapanga ndilo jina maarufu hapa mjini.

Mwandishi: Kwanini ulichagua biashara ya kuuza mapanga?

Tagalile: Niligundua ni biashara ya kipekee, hakuna mtu aliyekuwa amefikiria kutembeza mapanga hivyo nikaamua kuuza mimi. Ni miaka 20 tangu nianze kazi hii.

Mwandishi: Watu wanakuchukuliaje?

Tagalile: Wenye akili timamu hawaniogopi. Ila wajinga ndio wanao niogopa. Hivi mtu amebeba mapanga yote haya anauza unaweza kumuogopa? Anawezaje kukudhuru na anatembea barabarani?

Mimi huwa sijali watu wanao niogopa na nikijua mtu ananiogopa ndio nakaza zaidi mwendo ili akimbie anipishe kabisa njia.

Sijawahi kumdhuru mtu yeyote kwa miaka 20 yote niliyouza mapanga, ningekuwa nimeumiza watu polisi wasingeniacha hata kidogo. Wenye akili wananunua mapanga yangu, ninauza sana tu, sio kwamba siuzi.

Swali langu lilimfanya Tagalile afunguke zaidi. Ni kweli watu wengi wanamuogopa hata nilipoweka ‘status’ picha niliyopiga nae, wengi walikuja inbox wakishangaa nimewezaje kuzungumza nae.

Mapanga: Kuna watu wanajifanya wananiogopa wakati wao wanashinda vijiweni bila kazi yoyote ile. Sasa nani aogopwe? Yeye anayeshinda bila kazi halafu anaishi kwa kudandia au mimi ninaye uza mapanga? Alihoji kwa sauti ya ukali.

Mwandishi: Unawachukuliaje wanaokuogopa

Tagalile: Hupaswi kuishi vile wanavyotaka watu isipokuwa moyo wako unavyotaka.

“Unaona kabisa hawa watu wanakupotosha, na wewe unandoto zako kwanini usifuate ndoto zako? Mimi nawapenda watu wenye akili kama wewe,” anasema na kuongeza;

“Mbona jana hukuniogopa? Ulikuja ukaniambia ‘’habari za leo kaka’ nikagundua huyu mtu yuko timamu.”

Anasema hofu ya wengi ndiyo humfanya asipite vichochoroni isipokuwa barabara kuu.

“Kuna wakati unakuta mtu anapita kwenye majani kabisa au anaingia mtaroni akinipisha, huwa namwangalia tu halafu najiachia,” anasema.

Tabia yake ya kuwa kimya


Katika simulizi zake nyingi, anamtaja baba yake kama mwalimu kwake.

“Baba yangu alishanifundisha akasema, mwanangu usijibizane na mtu hata kama umejua amekusema vibaya. Wewe pita mbali na uende,” anasema na kuongeza;


“Huwa nawaona sana, unakuta mbele kuna watu wawili, wanakuangalia kwa kejeli kisha wanacheka kile kicheko… eheheee najifanya sijasikia naenda zangu.”


Mapanga anasema kuna haja gani ya kubishana na watu ambao hawasababishi ukapata kipato kwa ajili ya maisha yako zaidi ya kukusimanga na kukuvunja moyo.


“Kama mtu hanipi hata mia sina mpango nae, na waendelee kuniogopa hivyo hivyo wakae mbali na mimi, wakae huko kabisa wasinisogelee. Mimi naendelea na maisha yangu,” anasema.


Mavazi yake

Aina ya mavazi yake ndiyo ambayo inawafanya wengi wamuogope.

Huvaa nguo nyingi na nje koti kubwa lililochanika. Hubeba kibegi cha nguo kilichopachikwa pini nyingi zaidi ya 200 na kwenye kwapa huwa anabana mapanga.

“Nikivaa nguo laini si nitaumia kwa sababu nabeba mapanga mazito. Uvaaji huu ndio ninao upenda,” anasema Mapanga.

Wateja wake

Mmoja wa wateja wake, Erick Edward anasema hajawahi kuogopa kununua bidhaa kwa Mapanga.

“Nilimuungisha panga ambalo mpaka leo lipo imara sana, huyu mtu hana shida yoyote ni staili tu ya maisha yake. Ni sawa na wewe unavyoamua kuvaa suti au usivae,” anasema.

Wakati naongea na Mapanga kuna mteja mmoja alinunua panga, na aliuziwa kawaida tu akipunguziwa bei kutoka 12,000 mpaka 10,000.

Watu wanavyo muona

Bovan Mwakyambiki, ni miongoni mwa wadau wa maendeleo Mkoani Iringa yeye anasema ni miongoni mwa watu wanaomuogopa Mapanga.

Anasema ni muhimu kujiridhisha juu ya akili yake kulingana na biashara anayo fanya.

“Kama watu wengi wanamuogopa basi, muhimu zaidi tuthibitishiwe kama yupo timamu ili isijetokea shida siku zijazo,” anasema Mwakyambiki.

Mzee David Butinini anasema naye ni kati ya watu ambao huwa wana muogopa Mapanga lakini hajawahi kusikia amemdhuru mtu.


“Tumejitengenezea tu akili ya kuhukumu watu labda na mimi ni mtu wa kuhukumu, sijamzoea huyu jamaa huwa namwona tu na kwa kweli nilidhani mgonjwa wa akili,” anasema na kuongeza;


“Kama mlipanga kukutana, mkakutana na kuzungumza basi huyu anayo akili timamu ila ameamua tu kuwa hivyo alivyo.”

Meya wa Manispaa ya Iringa, Ibrahim Ngwada anasema kwa muda mrefu amekuwa akikutana nae barabarani lakini hajawahi kuzungumza nae kwa ukaribu.

“Kwa kweli huwa namwona lakini siwezi kuongea neno kwa sababu sijawahi zungumza nae,” anasema.