Mifumo minne ya kimataifa ilivyoongeza ufanisi JNIA

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Mussa Mbura,  akionyesha mashine mpya ya kisasa ya ukaguzi wa taarifa za abiria katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA). Picha na Michael Matemanga.

Muktasari:

  • Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), imesema imefunga mifumo minne ya kimataifa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam, inayomwezesha abiria kutumia muda mchache kuchakata taarifa zake na za mizigo.

Dar es Salaam. Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), imesema imefunga mifumo minne ya kimataifa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam, inayomwezesha abiria kutumia muda mchache kuchakata taarifa zake na za mizigo.

Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Mussa Mbura, amesema hayo leo Machi 18, 2024 alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya miaka mitatu ya Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan katika sekta ya usafiri wa anga.

Amesema mmoja wa mifumo hiyo ni wa usimamizi wa uchakataji wa taarifa za abiria (AMIS), ambao mashirika ya ndege ya kimataifa 21 yanayokuja nchini huwezesha kuchakata taarifa na kuzitumia kulingana na viwango vilivyowekwa na Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (IATA).

“Mfumo wa pili ni E-Gate, huu ni ule wa utambuzi, uthibitisho na ulinganifu wa taarifa za abiria kupitia E-Pass yake ya kusafiria ndani ya muda mfupi. Umesaidia abiria kujikagua na taarifa kupokewa kwa ufanisi, usahihi, usalama na urahisi,” amesema.

Amesema mfumo huo ulioanza Februari, 2024 umesaidia kupunguza muda kutoka takribani dakika 45 hadi dakika moja pekee.

“Hii imesaidia pia kuepuka usumbufu wa kuachwa na ndege kama anasafiri vilevile kuondoa ucheleweshwaji unaoweza kujitokeza kwenye dirisha la ukaguzi,” amesema.

Mbura amesema mfumo wa tatu ni wa uchakati wa utunzaji mizigo unaotumika kuisafirisha, ambao una hatua tano za ukaguzi na umeunganishwa na mashine za uchunguzi wa usalama.

“Mfumo huu una uwezo wa kuchakata mizigo 1,800 ndani ya saa moja, kuhifadhi mizigo 150 kwa wakati mmoja. Umesaidia kuhakikisha huduma ya mizigo inakidhi vigezo vya kimataifa,” amesema.

Pia amesema kuna mfumo unaomwezesha abiria kujihudumia bila kukutana na wahudumu wa shirika la ndege, wenye uwezo wa kumfanya abiria akachagua ndege anayosafiri nayo.

Amesema katika kupanua huduma, mifumo hiyo itapelekwa kwenye viwanja vingine vyenye msongamano wa abiria kama vile KIA na Dodoma.

Mkurugenzi huyo ameishukuru Serikali kuwawezesha kufikia hatua hiyo.

Mafanikio mengine amesema ni kupaa kwa mapato ya Mamlaka kutokana na shughuli zinazoendelea kwenye viwanja hivyo.

“Mapato yameongezeka kutoka Sh71.42 bilioni mwaka 2020/21 hadi Sh128.84 bilioni katika mwaka wa 2022/23,” amesema.

Amesema safari za ndege za moja kwa moja za mashirika makubwa ya kimataifa ya AirFrance kutoka Paris, Saudia Airline na Airlink kutoka Afrika Kusini zimeongezeka.

Februari 2024, amesema uwanja wa JNIA ulitunukiwa na kutambuliwa kwa kupewa cheti na Shirika la IATA kuweza kuhudumia na kuhifadhi mizigo inayoharibika haraka. 

Amesema abiria pia wameongezeka kutoka milioni 2.4 mwaka 2021 hadi 3.9 milioni mwaka 2023, ambalo ni sawa na ongezeko la asilimia 63.

Mkurugenzi huyo amesema sababu ya ongezeko ni pamoja na filamu ya ‘The Royal Tour’ uboreshwaji wa miundombinu na kuendelea kuimarika kwa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL).

Amesema kwa kufungwa taa kwenye viwanja vya Dodoma, Mtwara, Songea na Songwe kumewezesha ndege kuruka na kutua kwa saa 24.

Akizungumzia Uwanja wa Ndege wa Msalato mkoani Dodoma, amesema ujenzi umefikia zaidi ya asilimia 40 ukitarajiwa kukamilika mwaka huu.

Kuhusu changamoto, Mbura amesema ipo ya fedha katika kukamilisha ujenzi wa uzio kwenye viwanja vya ndege.