‘Msimamo wetu ulituponza’ makada Chadema waeleza

Wanachama wa Chadema kata ya Dutwa wilayani Bariadi mkoani Simiyu, Kitala Kikaja (Kulia) na Ng'hulima Ilanga (Kushoto) wakiwa katika Ofisi za chama hicho Kanda ya Serengeti baada ya kushinda rufaa ya kesi yao iliyowafunga kwa makosa ya wizi, kubaka na unyang'anyi wa kutumia silaha. Picha na Mgongo Kaitira

Muktasari:

“Msimamo wetu ulituponza,” ndivyo wanavyosema Katala Kikaja (27) na Ng’hulima Ilanga (35), wakazi wa Dutwa wilayani Bariadi mkoani Simiyu waliohukumiwa kifungo cha maisha jela kwa kosa la kubaka, wizi na unyang’anyi wa kutumia silaha.


Mwanza. “Msimamo wetu ulituponza,” ndivyo wanavyosema Katala Kikaja (27) na Ng’hulima Ilanga (35), wakazi wa Dutwa wilayani Bariadi mkoani Simiyu waliohukumiwa kifungo cha maisha jela kwa kosa la kubaka, wizi na unyang’anyi wa kutumia silaha.

Vijana hao ambao walikuwa mawakala wa mgombea udiwani Kata ya Dutwa kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Saguda Bulahya walikamatwa baada ya kugomea matokeo wakishinikiza mgombea wao atangazwe mshindi baada ya kumshinda yule wa Chama cha Mapinduzi (CCM).

Msimamo huo ndio ulimfanya mgombea huyo kugoma kusaini fomu ya kukubali kushindwa uchaguzi huo, lakini mgombea wa CCM akatangazwa kwa mabavu, Oktoba 29 mwaka 2020 na Kikaja na Ilanga wakakamatwa na kufunguliwa mashtaka kabla ya kuhukumiwa kifungo cha maisha.

Kwa siku 748, makada hao waliishi gerezani tangu walipokamatwa Oktoba 29 mwaka 2020 na kuhukumiwa kifungo Aprili 12 mwaka 2022 kisha Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga kuwaachia huru Novemba 16 mwaka huu.

Hukumu ya kuwaachia huru ilitolewa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga, Athuma Matuma baada ya kuridhika na hoja za rufaa kuwa ushahidi uliowatia hatiani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Bariadi ulikuwa dhaifu, unaotia mashaka na usiokubalika kisheria.

Licha ya wizi wa Sh300,000, warufani hao walidaiwa kumbaka msimamizi msaidizi wa kituo cha kupigia kura. Wakizungumza na Mwananchi, Kikaja na Ilanga wanasema kwa miezi saba walikaa katika magereza ya Bariadi mkoani Simiyu, Kahama, Butimba jijini Mwanza na Shinyanga.

“Oktoba 28, 2020 saa mbili usiku nikiwa wakala wa mgombea udiwani tulimaliza kuhesabu kura ikaonekana mgombea wetu ameshinda, tukahakiki kisha kila upande ukakubaliana na matokeo, baadaye tukakabidhi matokeo kwa msimamizi wa uchaguzi Kata ya Dutwa,” anasema Kikaja.

Lakini, Kikaja alisema walishangaa kuona msimamizi wa uchaguzi akimtangaza mgombea wa CCM kushinda, jambo lililowafanya wapinge matokeo na polisi wakaanza kurusha mabomu ya machozi.

“Kesho yake, nikiwa na wenzangu, Emmanuel Sosoganya na Robert Busumadilu walikuja askari watatu waliovalia kiraia wa Kituo cha Polisi Dutwa wakanikamata bila kuniambia kosa nililofanya. Tulipofika polisi tulimkuta OCS (mkuu wa kituo) akiwa na mwanamke anayedai kubakwa kwenye kituo cha kupigia kura cha Shule ya Msingi Tunge-Mwamabu, kumjeruhi na kumnyang’anya mali zake,” alisema.

Hata hivyo, mwanamke huyo alipoulizwa iwapo anamtambua kijana huyo alikana na kumtaka OCS amwachie, lakini hakufanya hivyo, badala yake alipelekwa chumba kingine alikoambiwa avue viatu, nguo, kofia na mkanda kisha wakaanza kumpiga na Oktoba 30 akasafirishwa hadi Kituo cha Polisi Bariadi alikokutana na Ilanga, ambaye waliunganishwa kwenye kesi moja na Novemba 13 wakapelekwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Bariadi na kusomewa mashtaka ya wizi, kubaka na unyang’anyi wa kutumia silaha.

“Baada ya kusomewa mashtaka yale tulikana, lakini hakimu alikataa kutupa dhamana akisema shtaka la unyang’anyi halina dhamana tukarudishwa Gereza la Bariadi. Ilikuwa kila tukipelekwa mahakamani mashahidi hawapo,” anasema.

Ng’hulima Ilanga naye alisema baada ya mashahidi wa jamhuri kukamilisha ushahidi wao, hakimu hakutoa nafasi kwa washtakiwa kuwauliza chochote.

Alisema kutokana na hali hiyo mawakili wao, Amani Mwiru na Gaston Garubindi waliwataka kuwa na subira huku wakiwahakikishia kuandaa hoja za kukata rufaa kupinga hukumu itakayotolewa.

“Ushahidi dhidi yetu uligubikwa na utata, shahidi wetu tuliyemleta mawakili wa jamhuri walimkataa wakisema alitakiwa awe wa kwao na hakimu akaunga mkono hoja hiyo,” alisema Ilanga.


Mawakili kuzawadiwa

Katibu wa Chadema Kanda ya Serengeti, Jackson Mnyawami aliishukuru Mahakama ya Rufani kwa kutenda haki na kuoomba uongozi wa mahakama kuiangalia Mahakama ya Hakimu Mkazi Bariadi kwa kutoa hukumu ya kifungo cha maisha jela kwa kosa ambalo halikutendwa.

Alisema Desemba 12 chama kitajadili utaratibu wa kutoa mkono wa shukrani kwa mawakili waliofanikisha makada hao kuachiwa huru, ikiwamo kuwapa vyeti vya heshima kwa kazi nzuri waliyoifanya.

“Tutaendelea kukata rufaa kesi zote zinazoonekana kuwa kandamizi hata kwa wanachama wa vyama vingine,” alisema.