Mtu mmoja afariki kwa kipindupindu Musoma, saba walazwa

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,  Said Mtanda ( Kushoto ) akimkabidhi  Mkuu wa Mkoa wa Mara, Evans Mtambi moja ya nyaraka ikiwa ni sehemu ya makabidhiano ya ofisi hiyo. Picha na Beldina Nyakeke

Muktasari:

  • Mtu mmoja amefariki dunia na wengine 34 kuugua baada ya kulipuka kwa ugonjwa wa kipindupindu katika halmashauri ya wilaya ya Musoma vijijini tangu Machi 20, 2024 ulipotangazwa kulipuka mkoani humo.

Musoma. Mtu mmoja amefariki dunia baada ya kulipuka kwa ugonjwa wa kipindupindu katika halmashauri ya wilaya ya Musoma vijijini mkoani Mara.

Kufuatia kulipuka kwa ugonjwa huo, Machi 20, 2024, jumla ya watu 34 wamebainika kuambukizwa na kuugua ugonjwa huo, ambapo hadi sasa wagonjwa saba wamelazwa na wanaendelea na matibabu.

Akizungumza mjini hapa leo Jumanne Aprili 9, 2024 wakati wa makabidhiano ya ofisi, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Evans Mtambi amesema ugonjwa wa kipindupindu ni wa aibu, hivyo mamlaka husika zinapaswa kuhakikisha unaisha.

“Nimeambiwa mtu mmoja amefariki na wengine saba wamelazwa, niwaagize wakuu wote wa wilaya na watu wa afya hakikisheni huu ugonjwa haufiki kwenye wilaya zenu, na kwa Musoma hakikisheni huu ugonjwa unaisha kabisa,” amesema.

Akizungumza kuhusu nafasi hiyo ya ukuu wa mkoa, Mtambi amewataka watumishi wa umma kutimiza wajibu wao na  kamwe hatamvumilia mtumishi yeyote atakayeshindwa  kutimiza wajibu wake kwa sababu mbalimbali ikiwamo uzembe.

“Sitavumilia uzembe wa aina yoyote, tumeaminiwa na kupewa majukumu wengine kwa nafasi za uteuzi, wengine kwa utaalamu na taaluma zenu, tunawajibika kuwatumikia wananchi kwa sababu wanatulipa, hivyo ni lazima tutimize malengo yetu kwa manufaa yao,” amesema Mtambi.

Mtambi ametuma salamu kwa taasisi zinazotakiwa kufanya kazi saa 24 ikiwemo hospitali na polisi na kwamba atazitembelea muda wowote, kwani yeye kama mwanajeshi pia yupo kazini saa 24.

“Hospitalini nitakuja usiku muda wowote, mchana muda wowote, siwaambii ni lini na wapi lakini kaeni mkijua nitakuja bila kutoa taarifa, lengo ni kuhakikisha huduma zinatolewa zenye kukidhi mahitaji,” amesema.

Ameuagiza uongozi wa idara ya afya kujitafakari na kuja na majibu kwa nini kwenye vituo vya kutolea huduma za afya vya Serikali hakuna huduma ya vipimo vya magonjwa mbalimbali siku za Jumamosi na Jumapili.

“Sidhani kama kuna mtu ana miadi na Mungu kwamba mimi nataka niugue kuanzia Jumatatu hadi Ijumaa, najiuliza hii ni sera ama kitu gani, mbona kwenye vituo binafsi wanatoa huduma saa 24, siku 7 za wiki ikiwemo huduma ya vipimo vya magonjwa tofauti na kwenye vituo vya umma?” amehoji.

Amesema anavyo vipaumbele vingi ikiwa ni pamoja na suala la elimu, afya, miundombinu ya barabara na kwamba hayo yote yatafanikiwa kwa ushirikiano baina ya watumishi wote.

Amesema ingawa yeye ni mwanajeshi lakini atajitahidi kubadilika kwenda na mazingira ikiwa ni sehemu ya shukrani yake kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumteua kuwa mkuu wa huo.

“Nitajitahidi kuwa mwanasiasa lakini mkumbuke kwenye uigizaji kuna wakati rangi yako halisi inajulikana, sasa wakati naigiza, naomba twende pamoja na hata nikibadilika rangi yangu halisi ikaonekana, naomba twende pamoja kwa sababu nia ni kufikia malengo na malengo yetu ni huduma bora kwa wananchi,” amesema.

Akikabidhi ofisi, aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Mara, Said Mtanda amesema hakutarajia kuhamishwa  kwa muda mfupi kama ilivyotokea lakini kwa vile ni utumishi wa umma, hana budi kukubaliana na hali hiyo.

 “Nilipokea kwa simanzi kidogo huu uteuzi kwa sababu kati ya vitu nilivyokuwa namuomba Mungu ni pamoja na angalau nikae Mara kwa mwaka mmoja lakini si haba, miezi 11 ni mingi na ninachoweza kusema ni kwamba nimefanya kazi kwa amani sana katika kipindi chote nilichokuwa hapa Mara,” amesema Mtanda.