Mwakagenda: Uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 Mbeya itawaka moto

Muktasari:

  • Kilio hicho kimezidi katika awamu hii ya tano ambayo pia imeshuhudiwa baadhi ya wabunge na madiwani wakirejea CCM kutoka vyama hivyo.

Licha ya vyama vya upinzani kuwa na viongozi wa kuchaguliwa katika majimbo, kata na serikali za mitaa, bado kilio kikubwa kimekuwa ni kutokuwepo kwa mazingira sawa ya ushindani kati yao na chama tawala cha CCM.

Kilio hicho kimezidi katika awamu hii ya tano ambayo pia imeshuhudiwa baadhi ya wabunge na madiwani wakirejea CCM kutoka vyama hivyo.

Hata hivyo, baadhi ya wabunge wa upinzani akiwamo Sofia Mwakagenda, Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema) kutoka Mbeya, wanaamini kwamba katika uchaguzi wa mwaka 2020 wataigaragaza CCM katika majimbo ya mkoa huo na kitaifa.

Akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu hivi karibuni, Mwakagenda anasema mateso wanayopata viongozi na makada wa chama hicho ni kichocheo cha ushindi katika chaguzi zinazokuja. Yafuatayo ni mahojiano kati ya mbunge huyo na mwandishi wa gazeti hili:

Swali: Kumekuwa na shinikizo kubwa kutoka CCM inayonyemelea majimbo ya wabunge wa upinzani hususani Chadema, mnafanyaje kukabiliana na mapambano hayo?

Jibu: Kwanza katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, Chadema tulishinda majimbo karibu yote, vijana wetu wengi waliwekwa ndani, lakini kulikuwa na dhuluma katika majimbo mengi. Kwa mfano katika jimbo la Rungwe kuna vijana 126 walikamatwa na kuwekwa ndani.

Ilinigharimu Sh15 milioni kuweka wakili wa kuwatetea mahakamani, lakini wanne walifungwa, pia nao ni kwa sababu ya uzembe.

Tuliona jinsi wasimamizi wa uchaguzi walivyotangaza kwa nguvu wagombea wa CCM. Lakini, tumejipanga mwaka 2020 kuyarudisha majimbo yote.

Kuhusu jimbo la Mbeya Mjini, ile ni moja ya ngome zetu kubwa. Haijalishi polisi au jeshi wala nini. Mimi mwenyewe nimeshaandika urithi kwa ajili ya kulitetea hilo jimbo.

Kijana wetu Sugu (Joseph Mbilinyi- Mbunge wa jimbo hilo) anafanya vizuri sana na nafikiri ametuongezea credit (sifa) na umoja kama wana Chadema.

Mimi nafikiri kwa washauri wa upande wa pili, ule weledi wa kina Kingunge (Ngombare Mwiru) zamani waliokuwa wanafanya kubana wapinzani ungetumika sasa kuliko mikakati wanayotumia inayojenga chuki miongoni mwa Watanzania. Lakini Mbeya tuko vizuri sana.

Swali: Ukiwa kama Mbunge wa Viti Maalumu, je una mpango wa kugombea jimbo mwaka 2020?

Jibu: Labda tu ni kwambie 2015 niligombea jimbo la Rungwe na kwenye chama chetu tulikuwa 26, nilikuwa mtu wa nne na nilikuwa na Sh3,000 tu mfukoni na nusu tanki kwenye gari langu (kiwango cha mafuta kwenye tanki). Nitagombea tu jimbo lolote mwaka 2020.

Tulimchagua kiongozi wetu John Mwambigija ambaye naye alishinda ubunge lakini akatangazwa mtu mwingine, ikasababisha vurugu na moto ukachomwa barabarani.

Swali: Kama mnaamini mliporwa ushindi mlishitaki?

Jibu: Tulishtaki lakini unajua sisi bado hatujashika dola, mahakama zetu bado hazijawa huru.

Swali: Kesi ilikwisha?

Jibu: Kesi ilikwisha, lakini hakimu alisema ni makosa tu ya kibinadamu, kwa hiyo tukaona tumwachie. Kwa sababu kama ni binadamu ndiyo anayefanya makosa hayo hayo yanayoshitakiwa. Unaona kabisa hakimu alivyoelemewa.

Swali: Mbeya ni mkoa wenye viongozi wakubwa wa Serikali, hamwoni kwamba hiyo tayari ni mbinu ya kushinda majimbo zaidi?

Jibu: Mawaziri siyo wanaopiga kura peke yao na hiyo inatusaidia kwa Rais aliye madarakani anayeweka mawaziri akifikiri watamsaidia.

Kwa mfano, Haonga (Pascal- Mbunge wa Mbozi) aliyekuwa mwalimu aliyesimamishwa kazi kwa muda mrefu, lakini alimpiga waziri wa kilimo wakati huo, Godfrey Zambi. Mwalimu asiye na mshahara kwa sababu alikuwa hana kazi kwa muda mrefu, lakini alishinda.

Hata mimi nikiletewa Tulia (Dk Tulia Ackson) leo nitamshinda tu, kwa sababu hata katika kata 43 walitudhulumu kata 42, lakini kata moja nilishinda, mwanzo mpaka mwisho nilikuwapo.

Swali: Tuzungumzie uchaguzi mdogo unaoendelea sasa wa kata 77 na jimbo moja, kumekuwa na kuenguliwa kwa wagombea wa upinzani, tatizo ni nini?

Jibu: Tangu tupate uhuru, Tanzania imekuwa moja, lakini tulipoingia mfumo wa vyama vingi tumegawanyika. Kazi ya vyama vya upinzani ni kukosoa, mnapouliza kwa nini mnapinga tu mjue ndiyo kazi yetu.

Obama (Rais mstaafu wa Marekani, Barack Obama) alikuwa chama tawala, leo yuko chama cha upinzani, kwa sababu katiba yao imekaa vizuri. Sisi tulivyoingia mfumo wa vyama vingi tumesaidia sana nchi hii kufika hapa.

Sasa kwa nini wagombea wanaenguliwa? Je, hatuko makini? Hapana. Siasa za sasa zinataka Watanzania waonekane kuwa hawajui kitu.

Kwa mfano, kule Tunduma kuna vijana watano wa Chadema, jioni tumefanya uchaguzi, asubuhi polisi wamekwenda kwa madiwani wale, mmoja akaambiwa wewe unazuia TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) wasikusanye kodi. Mwingine anaambiwa kwamba wewe ulitaka uue saa sita usiku.

Saa sita mchana, tukiwa kwenye kesi ya Mbunge Haonga, vijana wetu wakiwa wameshajaza fomu, wanazipeleka kwa kiongozi wa tume anasema mimi nimeshapata watu wa Chadema, fomu zimeshaletwa. Watu wa Chadema? Ni kina nani? Majina hayajulikani, hayapo na msimamizi anang’ang’ania.

Sheria ya uchaguzi 2015 inasema, kama ngazi ya wilaya imeshapeleka majina na mkoa ambayo ndiyo ngazi ya juu inaweza kutengua hayo majina.

Kamati kuu ikaamua katibu mkuu apeleke barua ya wagombea anao watambua yeye. Msimamizi akakataa. Sasa huu ndiyo uhuni ambao hatupendi utufikishe pabaya.

Swali: Tunajua Rais ndiyo mwenye mamlaka ya juu ya kuruhusu mchakato wa mabadiliko ya Katiba. Lakini ninyi kama chama mna mkakati wowote wa kuchokoza jambo hilo?

Jibu: Labda nikukumbushe kitu kimoja, vitu hivi vya kitaifa huwa vinaonekana ni vya kundi fulani. Lakini hili ni suala la polisi, wanajeshi, waandishi wa habari na wananchi.

Wewe unafahamu, mahakama ya The Hague inawatazama zaidi viongozi wa siasa. Leo hii (Freeman) Mbowe akiwaambia wananchi waingie barabarani watamlenga yeye, lakini wananchi wakiamka wanaweza kudai Katiba tena ile ya Jaji (Joseph) Warioba. Kwa hiyo wananchi tuamke tudai Katiba.

Si kwa ajili ya uchaguzi, tunazungumzia uchaguzi tu kwa sababu tunataka madaraka, lakini Katiba inazungumzia haki.

Trump (Donald Trump- Rais wa Marekani) aliingia madarakani akiwa na mbwembwe nyingi, lakini sasa ametulia kwa sababu Katiba yao imenyooka.

Swali: Katika Bunge la Bajeti lililoisha hivi karibuni, kambi ya upinzani hamkusoma bajeti mbadala karibu zote, hamwoni kwamba pale mlipoteza umaarufu wenu hasa ikizingatiwa kuwa Bunge sasa halionekani moja kwa moja?

Jibu: Kwanza ieleweke kuna mihimili mitatu ya dola ambayo ni Bunge, Mahakama na Serikali. Tuko kwenye mabunge ya Jumuiya ya Madola (Commonwealth) ndiyo maana hata bajeti inasomwa pamoja kwa sababu tumesaini mkataba kama taifa.

Hatukusoma bajeti zetu kwa sababu, Kambi Rasmi ya Upinzani, awe Mbowe au mtu yoyote, analipwa na Serikali.

Wewe unafahamu Waziri anapoandika hotuba ya bajeti, haandiki yeye, ana wasaidizi wake wanaoiandaa kwa miezi sita. Kwa hiyo na sisi tuna wasaidizi wetu wanaotusaidia kuandaa kazi zetu waliopo kisheria kabisa.

Mimi siwezi kuchangia kuhusu Wizara ya Mambo ya Ndani kama siijui, lazima nisome vitabu jijue kabisa kama kuna Lugumi au vipi. Wale watu ndiyo wanatusaidia sisi.

Siyo kwamba wapo kwa upinzani tu, hata chama tawala wanao, tena wao mawaziri wao wanalipwa na Serikali kwa hiyo ni kama wanalipwa mara mbili. Walipoona wapinzani tumeweka wasaidizi na wenyewe wakaweka.

Sisi wabunge wa upinzani tunasoma sana, iwe ni wabunge wa majimbo au wa viti maalumu.

Kwa nini hatukusoma, huwezi kusoma kitu ambacho hujakifanyia kazi. Hata hivyo, sisi tuna njia nyingi za kujieleza ikiwa pamoja na ushawishi na kutoka nje ya Bunge.

Tuliendelea kuwalipia vijana wetu ili waendelee kuchapisha taarifa zetu. Tuliwatafutia hata ofisi kwa sababu walifukuzwa kwenye majengo ya Bunge.

Swali: Mbali na siasa, nimesikia wewe ni mwanamichezo. Umefanya nini mpaka sasa kuinua michezo nchini?

Jibu: Unajua kwenye siasa hatufanyi kwa kuiga bali unafanya kile kitu unachokipenda. Mimi ni mpenzi wa mpira wa miguu na kule nyumbani tuna timu ya Tukuyu Stars na sasa tuna mkakati wa kuchangishana ili tuirudishe juu. Tunafanya hivyo kwa Wanyakyusa wote bila kujali vyama.

Vilevile mimi pia ninaratibu mchezo wa ngumi nataka niwe promoter kampuni yangu inaitwa Lady in Red. Nitajikita kwenye ngumu hasa za wanawake. Tunandaa pambano litakalofanyika Agosti 18 kwa ajili ya kukusanya pesa za kununua taulo za kike.

Kwa mara ya kwanza nilipochaguliwa tu ubunge, niliandaa pambano kati ya Yanga na Mbeya City kwa lengo la kukusanya Sh600 milioni za kujengea vyoo na madawati, lakini kwa kuwa siasa Mbeya zinaturudisha nyuma. Ikashindikana.

Hata hivyo, nilikuwa mgeni, si unajua unapokuwa kidato cha kwanza unanyanyaswa, unapigwa konzi, lakini sasa nimejifunza.

Swali: Kwa muda mrefu sasa wabunge na makada wa Chadema mmekuwa na kesi nyingi, mnapangaje kujikwamua na kesi hizo ili zisije kuwakwamisha mbele ya safari?

Jibu: Imefika mahali sasa usipokuwa na kesi na wewe ni Chadema, tunaanza kukutilia shaka kwamba ama unatusaili au kuna kitu unakifanya ambacho hatukifahamu.

Swali: Wewe una kesi?

Jibu: Nyingi tu, nimeshagombana na polisi, sana mpaka sasa tumeelewana, nimeshakwenda mahakamani.

Serikali ya awamu ya tano inatumia muda mwingi kufanya viongozi wetu wazunguke. Kwa mfano sasa kina Mbowe wana kesi. Wakati wa Bunge la Bajeti walikuwa wanatakiwa kila Ijumaa waripoti Dar es Salaam.

Tukasema pale Dodoma kuna kituo kikuu cha Polisi, wakakataa. Kumbe ile ni mbinu. Walifikiri kuzuia mikutano na Bunge live inayoonyeshwa na TBC kwa kodi zetu, wanasema hawana fedha. Sasa hii mentality ya kutuziba mdomo haiwezi kuwasaidia.

Viongozi wetu wanatumia muda mwingi mahakamani, lakini Chadema ni taasisi. Mbowe akiwa mahakamani, Hai kazi zinaendelea, Mbeya sisi tunaendelea, wakiwafunga wale sisi tunaendelea na kazi na wakitufunga sisi watoto wetu wataendelea.

Swali: Kumekuwa na watu huru wenye mawazo mbadala yanayofanana na yenu wapinzani, je mna mpango wa kuungana nao ili kujiongezea nguvu?

Jibu: Siku zote unapotaka kushinda kitu chochote huwezi kushinda peke yako. Hatuwezi kushinda tu kama Chadema, lazima uwe na waandishi wa habari. Wakati sisi tunapigwa mlidhani tuna makosa, lakini leo hii kuna waandishi wa habari wamepotea, wengine wamefunguliwa mashitaka kutokana na kazi yao.

Tanzania bado ni yetu tunaipenda na ule msemo unaosema ukikosoa Serikali unaonekana msaliti siyo kweli. Uzalendo ni kusema ukweli.