Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mwanafunzi asimulia alivyokwama saa 24 ndani ya kifusi Kariakoo

Jackson Clement mwanafunzi wa kidato cha Nne. Picha Azam TV

Muktasari:

  • Jengo la ghorofa Kariakoo lililoporomoka limesababisha vifo vya watu 16, majeruhi 86 na uharibifu wa mali za mamilioni ya fedha

Dar es Salaam. Mwanafunzi wa kidato cha nne Jackson Clement amesimulia namna alivyokwama chini ya kifusi kwa saa 24, wakati akijaribu kujinasua katika ghorofa lililoporomoka Kariakoo jijini Dar es Salaam Jumamosi ya Novemba 16, 2024.

Jengo hilo limesababisha vifo vya watu 16, majeruhi 86 na uharibifu wa mali za mamilioni ya fedha.

Kupitia mtandao wa Instagram wa AzamTv, leo Jumanne, Novemba 19, 2024 Jackson anayetarajia kumaliza mtihani wake wa mwisho wa somo la baiolojia Novemba 21, wakati akiendelea kupatiwa matibabu hospitalini amesema, “jirani na fremu yetu pale chini stoo walikuwa wanavunja ili watengeneze ‘underground’ nyingine wajenge fremu, kwa hiyo wakati zoezi la kuvunja linaendelea sisi dukani kwetu asubuhi tulikuwa ndiyo tunafungua.”

Jackson amesema, “ghafla nashtuka jengo limeshanifunika, nilijitahidi kukimbia kwenda eneo jingine nikanasa juu kwenye nondo, kifusi kilikuwa kingi nikawa napiga kelele siku ya kwanza nikakaa humo humo nikavumilia sijatoka.”

“Siku ya pili kama saa tano hivi watu wakanisikia, nikaanza tena kupiga kelele wakaanza kufukua tulikuwa kama wanne hivi, lakini mmoja alishafariki wakabaki watatu na mimi. Kwa kuwa nilinasa juu, wawili walikuwa chini, walipotoboa njia wale wawili wakatoka nikabaki mimi peke yangu ambaye nimenasa.

“Wakaniambia kaa huko ndani tuje tukutoe mkono maana akija mwingine watauvunja, nikaa pale dakika kadhaa wakaja wakanitoa mkono pale kwenye nondo nikapelekwa hospitalini.”

Alipoulizwa kuhusu hali ilivyo ndani ya kifusi hicho amesema,”hali ilikuwa ngumu ile sehemu tulipiga kelele sana wakatoboa chini, wakapitisha maji tukawa tunakunywa na hewa tunapata.”

Jackson ambaye ni mwanafunzi amesema,“huwa ninakuja kumsaidia shemeji yangu siku za wikiendi, nipo kidato cha nne nimefanya mitihani saba, biology mmoja bado practical, nilikuwa na ombi kwa mwalimu wangu atafute namna yoyote ili nisaidiwe niweze kuufanya mtihani.”

Katika hatua nyingine, Rais Samia Suluhu Hassan amemuelekeza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuongeza saa 24 za uokoaji katika jengo hilo.

Maelekezo haya yamekuja baada ya kukamilika kwa saa 72 tangu jengo hilo liporomoke.

Asubuhi ya leo Jumanne, wakati Rais Samia akizungumza kwa njia ya simu na Waziri Mkuu kuhusu kinachoendelea kwenye uokoaji, ameagiza kuongezwa kwa saa 24 katika uokoaji ili kuwapambania watu wengi ambao huenda bado wako chini wamefunikwa na kifusi.

Kupitia mazungumzo hayo ya simu Rais Samia amesema,"ninatambua utaratibu wa uokoaji una muda maalumu wa saa 72 mpaka kusitisha zoezi hilo. Binafsi nina matumaini Mwenyezi Mungu anaweza akatenda miujiza yake na kuweza kuwanusuru ndugu zetu wengine ambao bado wamenasa kwenye jengo hilo.”

Aidha, Rais Samia amevipongeza vikosi vyote na wananchi wanaoendelea kupambana kuokoa maisha ya waathirika wa janga hilo la kuporomoka kwa ghorofa.

“Wameonyesha utu, uzalendo mkubwa na uchapakazi wa hali ya juu sana. Hivyo, nawatia moyo na kuwapa nguvu ya kuendelea kuwapambania ndugu zetu kwani ninyi ni mashujaa wa Taifa letu," amesema.