Ndalichako awapongeza upinzani, Waitara apinga

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako akipongezana na Naibu wake, William Ole Nasha baada ya Bunge kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2019/2020, bungeni jijini Dodoma juzi. Picha na Ericky Boniphace

Dodoma. Wakati Profesa Joyce Ndalichako, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia akiisifu hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mwita Waitara amesema ina takwimu nyingi za uongo.

Juzi, Bunge lilipitisha makadirio ya Sh1.38 trilioni ya mapato na matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa mwaka wa fedha 2019/20, ambapo mawaziri wanne walisimama kujibu hoja za wabunge 114 waliochangia.

Akifanya majumuisho, Profesa Ndalichako alisema kati ya wabunge hao, 63 walichangia kwa maandishi huku 51 wakizungumza na akaahidi kuwapa majibu ya maandishi.

Vilevile, aliishukuru Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa mchango wake na kuipongeza hotuba ya upinzani kwa ushauri makini iliobeba. “Kipekee kabisa, nimshukuru waziri kivuli (kwa Wizara ya Elimu), Mheshimiwa Susan Lyimo kwa hakika safari hii umekuja kivingine na hotuba yako imesheheni ushauri makini,” alisema Profesa Ndalichako.

Waziri huyo alitumia fursa hiyo kujibu hoja zilizoibuliwa na wabunge akianza na suala la vitabu.

Alisema mwaka 2013, mbunge wa Vunjo (NCCR-Mageuzi), James Mbatia aliingia na sanduku lenye vitabu vyenye makosa na ndiyo maana Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) imeongeza umakini.

Pia, alisema vitabu milioni 2.86 vya darasa la tano vimeshasambazwa na vilivyochelewa kufika ilikuwa Februari.

Kuhusu mitalaa ya shule za Kiingereza, alisema ilishaandaliwa tangu 2016 na inapatikana TET, duka la vitabu vya TET na mawakala wake waliopo nchi nzima huku vitabu vya kiada kwa darasa la kwanza hadi la tatu vikipatikana katika maktaba mtandao.

Akizungumzia hoja ya kuufumua mfumo wa elimu, Profesa Ndalichako alisema Serikali iko makini na inatambua bila mfumo imara wa elimu haiwezi kwenda vizuri.

Alisema ndiyo maana ilihakiki vyeti feki ambapo watumishi 15,336 waliondolewa kwenye mfumo wa ajira na kwamba, kwa kutambua akimwekwa mtu hana sifa hawezi kufanya vizuri, watumishi 5,300 walikuwa wameajiriwa katika nafasi ambazo hawana sifa nazo waliondolewa.

“Waheshimiwa wabunge mnataka Serikali ifanye nini zaidi ya hayo kuonyesha kwamba inatambua na kujali umuhimu wa elimu katika nchi yetu ya Tanzania,” alisema.

Wakati Profesa Ndalichako akitambua michango ya wabunge na kuisifu hotuba ya wapinzani, Naibu Waziri wa Tamisemi, Waitara alikuwa tofauti akisema imebeba takwimu nyingi zenye makosa.

“Nilipofuatilia nimegundua ziliandikiwa African Dream (Hotel). Hizi ni data za African Dream,” alisema Waitara. African Dream ni hotel iliyopo jijini Dodoma.

Miongoni mwa makosa aliyosema yako kwenye hotuba hiyo ni upungufu wa walimu 91,000 akisema si kweli na kueleza kuwa shule za msingi hazina walimu 66,485 na sekondari 14,080 hivyo kufanya jumla ya walimu 80,585.

Katika hotuba yake, Lyimo ambaye ni mbunge wa viti maalumu (Chadema), alisema idadi ya walimu, kwa takwimu za 2016 na 2017, imeshuka kutoka 197,291 hadi 191,772 sawa na anguko la asilimia 6.5.

Lakini, kwenye bajeti ya Wizara ya Elimu mwaka huu wa fedha, alisema wizara ilisema kuna upungufu wa walimu 85,916 na kuahidi kuajiri walimu 10,140.

Lyimo pia alitahadharisha kuhusu kushuka kwa bajeti ya elimu kwa miaka mitatu mfululizo akisema kunasababisha kutotekelezwa kwa baadhi ya miradi ya maendeleo.

Akitoa ufafanuzi kuhusu suala hilo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alisema ni kweli takwimu zinaonyesha uwiano wa fungu la elimu na bajeti nzima umeshuka kutoka asilimia 17 za mwaka 2015/16 hadi asilimia 16 mwaka 2016/17, asilimia 15 mwaka 2017/18 na asilimia 14 mwaka huu na ujao wa fedha.

“Bajeti ya elimu inashuka lakini fedha za maendeleo hazijapungua isipokuwa za matumizi ya kawaida ambayo yamepungua kwa miaka miwili na si mitatu iliyopita. Hii inatokana na hatua za Serikali kuwaondoa watumishi hewa pamoja na mabadiliko yaliyofanywa kwenye maeneo tofauti,” alisema Dk Mpango.

Waziri mwingine aliyechangia hotuba hiyo ni Naibu Waziri wa Elimu, William Ole Nasha.