Njia panda matumaini nyongeza ya pensheni

New Content Item (1)

Muktasari:

  • Wastaafu wa kada mbalimbali katika taasisi na mashirika ya umma wamemuangukia Rais Samia Suluhu Hassan wakimuomba aingilie kati madai yao ya nyongeza ya pensheni kutoka Sh100, 000 hadi angalau Sh300, 000 kwa mwezi ili kuakisi mwenendo wa gharama za maisha.

Dar es Salaam. Wastaafu kutoka taasisi na mashirika ya umma, wamemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuingilia kati madai yao ya muda mrefu kuhusu nyongeza ya pensheni, ambapo wanataka ipande kutoka Sh100, 000 hadi Sh300, 000 kwa mwezi ili kuakisi mwenendo wa gharama za maisha. 

 Hoja za wastaafu hao zimetolewa leo Jumamosi Desemba 30, 2023, jijini hapa  , mbele ya wanahabari, wakitaja kupanda kwa gharama za maisha, kumewafanya kuishi kwa mikopo, huku wakikosa ulinzi wa afya zao kutokana na kutokuwa na bima ya afya.

Hata hivyo matumaini ya nyongeza ya pensheni hiyo yatategemea taarifa ya ripoti ya tathmini ya uhimilivu na uendelevu ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), itakayokabidhiwa kwa mfuko huo mwakani.

Wizara ya Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu imesema tathmini hiyo inayofanyika kila baada ya miaka mitatu.

“Kwa utaratibu ulivyo, mfuko hauwezi kuongeza pensheni bila tathmini hiyo, ripoti ya kwanza ya tathmini ya mfuko huo ilifanyika mwaka 2021 na ya pili inafanyika mwaka huu 2023,” amesema Festo Fute ambaye ni Mkurugenzi wa Divisheni ya Pensheni katika wizara hiyo. 

Septemba mwaka jana, Waziri mwenye dhamana na mifuko ya pensheni nchini, Profesa Joyce Ndalichako aliliahidi Bunge kwamba, Serikali inaangalia uwezekano wa kuongeza pensheni hiyo baada ya tathmini hiyo kufanyika mwaka 2022/2023.

Meneja Uhusiano na Elimu kwa Umma wa PSSSF, James Mlowe amesema tayari kazi ya tathmini inaendelea na ripoti itawasilishwa Januari mwakani.

“Kwa mfano ripoti huangalia umri wa wanachama, jinsia, hali ya Pato la Taifa (GDP), uwekezaji wa nchi na maeneo mengine ili kutoa mwelekeo wa uhai wa mfuko kwa miaka mingi ijayo,” amesema Mlowe.

Wakati ripoti hiyo ikisubiriwa, Sheria ya PSSSF ya mwaka 2018 inaelekeza kuhuisha pensheni za wastaafu kila baada ya miaka mitatu kutokana na mabadiliko ya mwenendo wa gharama za maisha.

“Sheria ipo lakini kanuni zake bado hazijaandaliwa, zikikamilika ndiyo itakuwa hai rasmi,” amesema Mlowe.

Wakizungumza na Mwananchi katika mkutano huo, wastaafu hao wamedai kuwa baadhi yao wameshariki dunia wengine wakiwa hawajiwezi kutembea.

“Inashangaza kuona wastaafu tuliotumikia Taifa hili tunaendelea kusotea nyongeza ya pensheni hiyo kwa mwezi wakati kuna wabunge wanalipwa Sh300, 000 kwa siku kwa kukaa tu bungeni na wakati mwingine wasiwe na mchango wowote,” amesema Katibu wa umoja wa wastaafu hao, Haizer Leizer.

Grace Msangi aliyekuwa karani wa Benki ya NBC 1979/1998 amedai anaishi kwa mkopo wa Sh3.2 milioni, ambao anatakiwa kuulipa hadi mwaka 2030, sawa na Grace Mokimirya aliyekopa benki baada ya kustaafu Tipper refinery mwaka 2001.

“Mkopo huo ninakatwa Sh59,800 kila mwezi kwa dhamana ya pensheni hiyo ya Sh100,000 ili niendeshe mradi wa kuku ila umekwama, nihudumie familia yangu ya watoto sita inayonitegemea, pia ninameza dawa za presha kila mwezi kwa Sh15,000, sina bima ya afya,”amesema Grace.

Musa Salimu (77) aliyetumikia Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) mwaka 1969/1995,  anaishi na familia yake ya watoto wanane huku akiwa amekopa Sh2.4 milioni, anayokatwa Sh58, 000 kila mwezi.

“Rais Samia atusaidie suala hili ili tumalizie maisha yetu kwa utulivu, muda wetu umeisha lakini angalau tusaidiwe kupata milo mitatu kwa siku,” amesema Mokimirya huku Elias Mnyampiga (68), akihoji huduma za bima kutoandaliwa kwa waastafu hao na sababu za Serikali kutojali maisha yao baada ya kustaafu.


Harakati za madai

Wastaafu hao waliotumikia nafasi mbalimbali za uanasheria, uhasibu na uhandisi, wamedai kutumia njia mbalimbali kupigania nyongeza hiyo bila matumaini.

Mwenyekiti wa umoja huo, Sadick Msuya alitaja hatua mbalimbali walizopitia tangu mwaka 2018 ikiwa ni pamoja na  kuandika barua na kukutana na viongozi wenye mamlaka ya kushughulikia pensheni hiyo bila matumaini. 

“Kwa hiyo tumelazimika kutumia vyombo vya habari kwa sababu tunaamini kabisa huenda Rais Samia akawa hana taarifa za suala hili, huenda akisikia atatoa neno lolote,” amesema Msuya.

Msuya amesema Serikali ilianza kulipa pensheni ya Sh100, 000 Januari Mwaka 2017, ikiwa ni tofauti na Sh50, 000 iliyokuwa inalipwa awali.