Nondo za Zitto akielekea kung’atuka ACT-Wazalendo

Kiongozi wa chama cha  ACT- Wazalendo Zitto Kabwe akiwasili katika ukumbi kwa ajili ya mkutano wa halmashauri kuu ya chama hicho  jijini Dar es Salam leo .Picha na Said Khamis

Muktasari:

  • Zitto amesema vijana wa Tanzania wanataka kuona maamuzi yakichukuliwa ili ajira nyingi na bora zitengenezwe.

Dar es Salaam. Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amesema kuna masuala ambayo yakiendelea kufumbiwa macho yanaweza kusababisha madhara kwa Taifa.

Akihutubia mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho, leo Februari 12, 2024 makao makuu ya ACT-Wazalendo Magomeni, Dar es Salaam amesema la kwanza ni migogoro ya ardhi na mipaka kati ya hifadhi na vijiji.

Amesema katika maeneo ya Kusini mwa Tanzania chama hicho kilipokea malalamiko ya wakulima dhidi ya wafugaji kuvamia maeneo yao na hata kusababisha mauaji.

“Vilevile maeneo ya wafugaji kuna malalamiko ya wananchi kuporwa mifugo na maofisa wa hifadhi kama vile wa Tanapa, TFS na Mamlaka ya Ngorongoro,” amesema.

Zitto amebainisha hayo baada ya kuzuru mikoa yote ya Zanzibar na 17 ya Tanzania Bara, baaada ya kuondolewa zuio la kufanya mikutano ya hadhara Januari, 2023.

“Ziara hizi zimetuonyesha hali halisi ya wananchi na zimeibuliwa changamoto zinazowakabili na kupitia baraza letu kivuli la mawaziri tumekuwa tukifuatilia kwa kina masuala haya ili kuleta unafuu kwa wananchi,” amesema.

Amedai migogoro ya namna hiyo imesambaa kila kona ya nchi na isipochukuliwa hatua italeta madhara kama vita ya wenyewe kwa wenyewe na kuhatarisha utulivu wa nchi.

“Tumeona na kusikia malalamiko ya wananchi wa Mbarali, wananchi wa Ngorongoro, wananchi wa Kagerankanda na Kalelani kule Kigoma, na uvamizi mkubwa wa mifugo wilaya za Kilwa, Nachingwea, Tunduru na Liwale,” amesema.

Zitto ameongeza: “Tunarudia pendekezo letu la kuitaka Serikali kufanyia kazi suala hili kwa kuunda tume ya Rais ya kutazama mipaka ya vijiji na hifadhi au mapori ya akiba. Tumependekeza tume kama ile ya mwaka 1991 iliyoshughulika na ardhi maarufu Tume ya Profesa Issa Shivji.”

Zitto amesema lingine ni kupanda kwa gharama za maisha kunakosababisha wananchi kushindwa kumudu maisha ya kila siku.

“Bei za bidhaa za vyakula, nauli za usafiri na hata vifaa vya ujenzi zimeendelea kuongezeka kila kukicha. Licha ya sababu ambazo viongozi wa Serikali wanazitoa, wananchi wanachotaka kuona ni maisha yao kuwa nafuu,” amesema.

Amesema wajibu wa Serikali ni kuhakikisha wananchi wanamudu maisha kwa kubuni, kutunga na kutekeleza sera zinazohakikisha bei za bidhaa muhimu kama vile chakula, mavazi na usafiri haziwi mzigo kwa wananchi.

“Chama chetu kinaendelea kutoa wito kwa Serikali kutimiza wajibu wake huo na kwa kupitia baraza letu kivuli, tumekuwa tukitoa majibu ya hatua zinazopaswa kuchukuliwa, ikiwamo Serikali kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula kwa kuongeza tija kwa mkulima na kumwezesha kulima kisasa ili kuongeza mavuno,” amesema.

Zitto amesema:“Kuelekeza nguvu kutumia rasilimali tulizonazo kwa mfano gesi asilia katika kuendesha mitambo na magari ili kupunguza matumizi ya mafuta kama vile petroli na dizeli.”

Amesema wanaendelea kuisisitiza Serikali kuwekeza vya kutosha katika uzalishaji wa mafuta ya kula, sukari na ngano nchini.

Kuhusu ajira kwa vijana, amesema imekuwa changamoto ya kudumu na mwiba mchungu kwa Taifa, kwa sababu Serikali haijielekezi kisera kujenga uchumi unaozalisha ajira nyingi, bora na zenye staha.

“Serikali ifahamu kuwa vijana wa Tanzania wamechoka simulizi na sababu zilezile kila siku, Watanzania wanataka kuona maamuzi yakichukuliwa ili ajira nyingi na bora zitengenezwe na Taifa letu lipige hatua kubwa,” amesema.

Wosia wa Zitto  

Amesema kujenga uongozi imara na dhabiti, ni jambo muhimu kwa chama hicho, akiwataka viongozi  kuendelea kuthamini na kusisitiza utumishi wa pamoja kwa kutanguliza masilahi ya chama badala ya matamanio binafsi.

"Mafanikio ya kiongozi yeyote yapo kwenye uwezo wa kuandaa viongozi wengine bora na dhabiti. Nikinukuu msemo mashuhuri wa Kiingereza usemao "A good dancer knows when to leave the stage" yaani mwanamuziki bora ni yule anayefahamu wakati wa kushuka jukwaani, basi mimi niwaombe kwa heshima mlivyonipa, nafasi mliyonipa niweze kuongoza sasa ni wakati wangu wa kuondoka jukwaani, nikiwa na amani thabiti kuwa kama chama tumeandaa viongozi wengi na wa kutosha kukipeleka chama chetu juu na mbali zaidi," amesema.

Amesema anapoelekea mwisho wa uongozi wake anawashukuru kwa imani yao na ushirikiano wao, akieleza matumaini yake kuna viongozi madhubuti watakaowavusha katika hatua ya sasa, kwani kila zama na kitabu chake.

"Mwezi ujao tunaenda kufanya uchaguzi mkuu wa tatu wa chama chetu na ajenda mojawapo ya kikao hiki ni kuweka mazingira bora kikanuni na kikatiba kuwezesha uchaguzi wa viongozi wetu watakaoongoza chama chetu kwa miaka mitano," amesema.

"Kila mmoja wetu anao wajibu wa kusimama pamoja kama timu moja, tukiwa na lengo moja la kufanikisha malengo na mipango ya chama chetu. Tulinde na kuiimarisha umoja wetu, tukijua nguvu zetu zinapatikana katika umoja wetu. Tuweke kando tofauti zetu za kinafsi na tuzingatie masilahi ya pamoja ya chama chetu," amesema.

Kikao cha halmashauri kilihudhuriwa na wajumbe 124 kutoka kote nchini.

(Imeandikwa na Sute Kamwelwe na Tuzo Mapunda)