Zitto: Nang’atuka uongozi wa ACT-Wazalendo 2024

Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe

Muktasari:

  • Chama cha upinzani nchini Tanzania cha ACT-Wazalendo kitafanya uchaguzi wake wa ndani Machi 2024 huku Zitto Kabwe akitangaza kutogombea tena nafasi ya kiongozi wa chama hicho kwa kuheshimu na kujengi msingi ya kufuata katiba ya chama chao.

Buhigwe. Kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amesema hatagombea tena nafasi hiyo katika uchaguzi wa ndani unaotarajiwa kufanyika Machi, 2024.

Akihutubia mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Mnanila Wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma jana Alhamisi, Novemba 23,2023, Zitto alisema uamuzi huo unalenga kujenga misingi ya kila kiongozi ndani ya ACT-Wazalendo kuheshimu na kulinda katiba ya chama hicho.

“Mimi kuachia ngazi na kukabidhi madaraka kwa kiongozi mwingine baada ya mihula yangu miwili ya uongozi kuisha unaweka msingi na muongozo kwa viongozi wengine watakaokuja kutii na kuheshimu katiba,’’ alisema Zitto

Alisema mchakato wa uchaguzi ndani ya chama hicho tayari umekamilika katika ngazi ya majimbo yanayotarajiwa kufuatiwa na chaguzi za mikoa kabla ya kuhitimishwa kwa uchaguzi mkuu wa Kitaifa utakaofanyika Machi, 2024.

"Mwezi machi, 2024 tunafanya uchaguzi mkuu wa chama, uchaguzi huo utamchagua kiongozi wa chama. Chama chetu kina utaratibu wa vipindi viwili vya miaka mitano mitano na baada ya hapo kiongozi haruhusiwi kuendelea kwenye nafasi hiyo, nitaheshimu katiba ya chama ya vipindi viwili kwa kukabidhi uongozi kwa kiongozi mwingine," alisema Zitto

Alisema uamuzi wake unalenga kuonyesha siyo tu kuheshimu na kulinda katiba, bali pia utofauti kati ya ACT-Wazalendo na vyama vingine vya siasa nchini.

Uchaguzi mkuu ndani ya ACT-Wazalendo unafanyika mwakani baada ya mkutano mkuu kupitisha azimio la kurejesha nyuma ratiba ya uchaguzi kwa mwaka mmoja kutoka Machi, 2025 hadi Machi, 2024.

Zitto alichaguliwa kuwa kiongozi wa ACT-Wazalendo Machi, 2015 kabla ya chaguliwa tena kwa awamu ya pili Machi, 2020.


Uraia kwa wana Kigoma

Katika mkutano huo, Zitto alirejea wito wake kwa viongozi na watendaji wa Serikali na taasisi zake kubadilisha mitazamo na fikra zao kuhusu wakazi wa Kigoma wanaoishi katika vijiji vinavyopakana na nchi jirani za Rwanda na Burundi kwa kuwahisi kuwa siyo raia.

“Watu wa Kigoma tuna haki sawa na Watanzania wengine katika suala la uraia, hapa Buhigwe nimeambiwa watu anaokwenda kufuatilia vitambulisho vyao vya Taifa wanahojiwa kana kwamba ndio wanaenda kujiandikisha. Hii tabia ya kuwafanya watu wa Kigoma kuwa raia wa daraja la pili lazima ikome. Kigoma tupewe haki sawa na Watanzania wengine,’’ alisema Zitto

Alisema ACT-Wazalendo itaendelea kusimama imara kutetea haki za kila mtu bila kujali itikadi zao kisiasa huku akisema msimamo huo ndio ulikifanya chama hicho kuwakemea waliojaribu kumsema vibaya Makamu wa Rais, Dk Phillip Mpango kuhusu uraia wake.

Zitto alisema hakuna Mtanzania mwenye uraia nusu, bali wote wana haki sawa na wanastahili kuheshimiwa utu na heshima yao katika masuala yote.

Kuhusu ujenzi wa Kituo cha pamoja cha forodha katika mpaka wa Tanzania na Burundi eneo la Manyovu Wilaya ya Buhigwe, Zitto aliitaka Serikali kukamilisha mradi huo uliokwama kwa zaidi ya miaka saba sasa huku wananchi wakizuiwa kuyaendeleza maeneo yao.

“One stop centers zimejengwa Namanga mkoani Arusha, Mtukula na Kabanga Mkoa wa Kagera, Tunduma mkoani Songwe, Tarakea mkoani Kilimanjaro na Sirari mkoani Mara…kwanini ishindikane kujenga kituo cha pamoja cha forodha eneo la Manyovu ambao ndio mpaka mkubwa kati ya Tanzania na Burundi?’’ alisema na kuhoji Zitto

Awali, Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Mkoa wa Kigoma, Sendwe Ibrahim aliutumia mkutano huo kuwasilisha kwa Zitto malalamiko ya wajasiriamali wa mji wa Manyovu kuhusu ujenzi wa soko na gharama ya kupangisha vibanda na vizimba vya biashara.

“Wafanyabiashara wanatakiwa kulipa kati ya Sh20,000 hadi Sh30,000 kwa kizimba au kibanda cha biashara; hii ni bei kubwa kulinganisha na hali halisi ya kiuchumi kwa wananchi. Tunashauri gharama hii ishuke hadi angalau Sh10,000,’’ alisema Sendwe