Hospitali za kanda zatakiwa kuwekeza utoaji huduma kimataifa

Waziri wa Afya Jenista Mhagama
Muktasari:
- Mpango huo utawezesha kupatikana kwa huduma nzuri na bora zitakazowapa tumaini wageni kutoka nje.
Dodoma. Serikali imezitaka hospitali za kanda kote nchini kuanzisha huduma za afya za kimataifa ili kuvutia watalii wanaoingia nchini kwa ajili ya matembezi na utalii.
Agizo hilo limetolewa leo Alhamisi Julai 10, 2025 na Waziri wa Afya, Jenista Mhagama wakati wa uzinduzi wa Kliniki ya Matibabu ya Hali ya Juu kwa Wagonjwa wa Kimataifa na huduma ya Ukaguzi wa Afya (Royal International Patients and Master Health Check-up Clinic) katika Hospitali ya Benjamini Mkapa (BMH), jijini Dodoma.
Waziri Mhagama ametaja mpango huo kuwa utawezesha kupatikana kwa huduma nzuri na bora zitakazowapa tumaini wageni kutoka nje na hivyo kutohofia afya zao wawapo Tanzania.
Hata hivyo, Mhagama amesema huduma pekee haitoshi bali inapaswa kutangazwa kwa wananchi kupitia madawati ya mawasiliano katika hospitali husika, na vyombo vya habari ili watu wajue.
Mhagama ameagiza kutumia mifumo ya kidijitali ili kupunguza gharama za matibabu kwa wagonjwa, hususan wakati kwenye rufaa jambo litakalopunguza hali ya mgonjwa kurudia vipimo kila anapopelekwa hospitali nyingine, huku akisisitiza ushirikiano kati ya hospitali na vyuo vikuu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Profesa Abel Makubi amesema kuanzishwa kwa huduma za kimataifa kunalenga kurahisisha upatikanaji wa matibabu wa hali ya juu kwa Watanzania na wageni kutoka nje ya nchi.
Profesa Makubi amesema huduma hizo zitakuwa za haraka na zitatolewa kwa wagonjwa wa ndani na madaktari watafanya kazi kwa muda wa ziada ili kuwahudumia kikamilifu.
Amesema hospitali hiyo inatoa aina 20 za huduma za kibingwa na 17 za kibobezi, huku ikihudumia wastani wa wagonjwa 1,200 kwa siku ikilinganishwa na 900 wa awali.
“Hospitali imeanza kutoa huduma za upasuaji wa kisasa kwa kutumia njia ya matundu (laparoscopic surgery) badala ya upasuaji wa kawaida, sambamba na huduma za upandikizaji uloto kwa wagonjwa wa sikoseli, na matibabu ya macho na ubongo,” amesema Makubi.
Awali, Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dk Peter Kisenge amehimiza ushirikiano baina ya hospitali zilizoweka makubaliano katika utoaji huduma, ambazo ni Benjamin Mkapa, KCMC, na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, ambazo zimesaini makubaliano rasmi ya kuendeleza huduma za pamoja.