Othman awataka vijana wadai Muungano wenye manufaa pande zote

Miongoni mwa washiriki wa Kongamano la Maadhimisho ya miaka 10 ya ACT Wazalendo wakifuatilia na kupongeza hutuba za viongozi wao. Picha na Muhamme Khamis

Muktasari:

  • Amesema mfumo ulipo sasa wa Muungano una haja ya kubadilishwa kwa sababu hautoi haki sawa kwa pande zote mbili za washiriki.

Unguja. Chama cha ACT-Wazalendo kikielekea kuadhimisha miaka 10 ya kuzaliwa kwake Mei 5, 2024, Mwenyekiti wake Taifa, Othman Massoud Othman amesema kuna umuhimu wa vijana wa Kizanzibari kuendeleza harakati za amani, kudai Muungano wenye manufaa ya pande zote mbili Tanzania Bara na Zanzibar.

Othman amesema hayo leo Aprili 21, 2024 akitoa mada katika kongamano la vijana lililoshirikisha wanachama na wasomi wa vyuo vikuu, katika ukumbi wa Picca Dilly, uliopo Kombeni, wilayani Magharib B, Unguja.

Amesema tangu Zanzibar iungane na Tanganyika mwaka 1964 haijawahi kunufaika na usawa kwenye Muungano.

Amesema hilo limekuwa likilalamikiwa mara kadhaa na kuundiwa tume bila ya mafanikio.

Othman, ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) amedai kwa mfumo ulipo sasa wa Muungano, kuna haja ya kubadilishwa kwa sababu hautoi haki sawa, isipokuwa unaupa faidi upande mmoja pekee wa Tanzania Bara.

Amedai katika muda wote tangu kuasisiwa Muungano umekuwa ukifanya kazi zaidi ya kuidhibiti Zanzibar kila sekta na ndiyo maana mambo muhimu ambayo yanaendeleza nchi yamebaki kuwa ya Muungano.

Othaman ametaja miongoni mwa mambo hayo kuwa ni umiliki wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ambayo ina kazi ya kusimamia sarafu ya nchi na utambulisho nje ya mipaka ya Tanzania.

"Hata kuundwa kwake hiyo Benki Kuu ya Tanzani (BoT), sehemu ya mtaji ambao uliianzisha kuna asilimia ya fedha ambazo zilitoka Zanzibar, baada ya kuvunjika Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki ambayo Zanzibar ilikuwa mwanachama," amesema Othman ambaye aliingia upinzani baada ya kuondolewa kwenye nafasi ya Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, kutokana na msimamo wake juu ya Muungano kwenye Bunge Maalumu la Katiba.

Pamoja na hayo, amesema wataendelea kudai haki ya Zanzibar katika BoT kwa sababu wanao ushahidi wa kutosha juu ya uwepo wa asilimia ambayo ilitoka Zanzibar.

Othman akidai hayo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Hamza Hassan Juma amasema madai ya viongozi hao hayana ukweli na wanapaswa kujitathmini.

Amesema malalamiko mengi ya Muungano yamefanyiwa kazi na ndiyo maana Zanzibar inapiga hatua za kimaendeleo.

Amesema uhusiano mwema uliopo unazaa matunda mengi zaidi na kutoa fursa kwa pande zote.

Juma akizungumzia madai kuhusu BoT amesema jambo hilo wanaendelea nalo kwenye mazungumzo kama yalivyofanywa mengine na kutatuliwa.

Othman amesema changamoto nyingine ya Muungano ni suala la mafuta na gesi ambalo liliingizwa kwenye mambo ya Muungano bila makubaliano ya pande mbili husika.

Kwa mujibu wa Othman ni bahati mbaya baadhi ya watu wenye nafasi za juu serikalini upade wa Zanzibar wanaendelea kuamini wana mamlaka ya kuchimba mafuta na gesi kisheria iwapo yatabainika, wakati jambo hilo linabanwa na sheria ya Muungano.

Awali, Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Ismail Jussa naye amedai kuwa Zanzibar kwa muda wote iliopo ndani ya Muungano imepoteza fursa muhimu ambazo kama zingewekwa sawa ingepiga hatua zaidi kimaendeleo.

Amesema Zanzibar inahitaji aina ya Muungano wa nchi mbili huru ambao utatoa fursa sawa kwa washiriki wote na si upande mmoja kunufaika zaidi kuliko mwingine.

Katibu wa Ngome ya Vijana ya chama hicho, Mohamed Busara amesema vijana wana wajibu wa kujitambua na kufahamu wanachokitaka.

Amedai kwa bahati mbaya vijana wa Kizanzibari wamekuwa wakidanganywa na kupewa ajira, huku wakikataa na kuacha mambo muhimu kwa mustakabali wao na maisha yao.