Profesa Kitila awataka mawaziri, naibu mawaziri kuzipa nafasi taasisi za umma

Muktasari:

Wakati Serikali ikiangalia namna inayoweza kukusanya mapato zaidi katika taasisi inayomiliki hisa chache, Waziri wa Uwekezaji na Mipango, Profesa Kitila Mkumbo ametaka taasisi hizo zisiingiliwe

Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema umefika wakati mawaziri, naibu waziri na makatibu wakuu wanatakiwa kuzipa nafasi taasisi za umma zilizoundwa kwa mujibu wa sheria zifanye kazi kama taasisi zinazojitegemea.

Amesema uhusiano ulipo kati ya taasisi hizo na viongozi hao ni kwa sababu zinamilikiwa na Serikali.

Profesa Kitila ametoa kauli hiyo Ijumaa Machi 16, 2024 wakati akifunga mafunzo hayo ya siku tatu ya wakurugenzi wa bodi wanazoiwakilisha Serikali katika kampuni ambazo inamiliki hisa chache. Kikao hicho kimefanyika chini ya Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Akizungumza wakati akifunga mafunzo hayo, Profesa Kitila amesema ili kuzipa nafasi taasisi ni vyema mabadiliko ya kimtazamo yakafanyika hasa kwa watu wa Serikali ili kuzifanya kampuni hizo zijitazame na kuendana na  misingi ya kampuni za kibiashara na si kama idara za Serikali.

“Tuzipe nafasi bodi na menejimenti ziendeshe shirika, sisi tuwape vigezo vya upimaji, kwamba tunataka mwisho wa mwaka mtuletee hiki, baada ya hapo tuwape nafasi wafanye kazi,” amesema Profesa Kitila.

Amesema haipendezi taasisi ya umma kila siku asubuhi kutembelewa na kiongozi huku akitolea mfano wa Katibu Mkuu na kuagiza kupewa vitu tofauti.

“Hawana nafasi ya kufanya hiyo kazi, hivyo suala la kubadilisha mtazamo upo ni upande wa kampuni lakini lazima sisi upande wa serikali tubadilishe mtazamo kuwe na tofauti kabisa namna ya kuendesha hizo taasisi,” amesema Profesa Kitila.

“Bila hivyo, tutafanya mabadiiliko yote ikiwamo yale Rais (Samia Suluhu Hassan) anayoyafanya, tutatunga sheria mpya lakini kama mitazamo yetu itabaki kuwa ileile, hakuna namna tunaweza kuzisaidia hizi taasisi,” amesema Profesa Kitila.

Amesema kama ni taasisi itajiendesha kama idara ya Serikali, itashindwa biashara, jambo ambalo litakuwa mzigo kwa Serikali.

Amesisitiza kuwa Serikali inatakiwa kubadilika kwa kuzipa nafasi kampuni zilizo chini yake ili ziweze kuleta matokeo tarajiwa

Amesema hiyo ndiyo sababu ya Msajili wa Hazina kuwa katikati ya taasisi hizo na Serikali kwani amekuwa akiikumbusha Serikali kuwa kama inataka kampuni hiyo iende wanavyotaka ni lazima wawape nafasi wafanye kazi.

Profesa Kitila ametumia nafasi hiyo kuwataka wawakilishi wa Serikali katika taasisi zenye hisa chache kubadilishana uzoefu na wengine hasa katika uendeshaji wenye faida.

“Sasa ninyi ambao mnakaa katika kampuni zenye hisa chache mna nafasi ya kutusaidia, mna nafasi ya kubadilishana ujuzi, tujue inakuwaje shirika likiwa chini ya Serikali kwa asilimia 100 halifanyi vizuri na ukilikabidhi chini ya sekta binafsi linafanya vizuri,” amesema Profesa Kitila.

Hayo yanasemwa wakati ambao Serikali iliwakutanisha kwa pamoja wakurugenzi hao wa bodi kuangalia namna inayoweza kuongeza mapato kutoka katika taasisi inazomiliki hisa chache.

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Dk Tausi Kida amesema sasa wako katika hatua ya kufanya mabadiliko makubwa ili kuhakikisha tija inapatikana kupitia uwekezaji uliofanywa na Serikali katika mashirika ya umma.

Amesema kwa sasa mashirika yako 304 huku uwekezaji ukiwa zaidi ya Sh75 trilioni na  kati ya taasisi hizo 56 Serikali inamiliki hisa kidogo.

“Katika mabadiliko haya kuna vipengele, kwanza kutakuwa na sheria ya uwekezaji wa umma inayoweza kuendana na mabadiliko hayo itakayoenda sambamba na kuwapo kwa mamlaka ya uwekezaji wa umma na kuboresha usimamizi wa utendaji kazi kwa mashirika hayo,” amesema Dk Kida.

Awali, mkurugenzi wa utawala na rasilimali watu kutoka Ofisa ya Msajili wa Hazina, Amon Nnko amesema maazimio matano yamefikiwa katika mafunzo hayo ya siku tatu.

Miongoni mwa maadhimio hayo ni kila mjumbe wa bodi kuhakikisha anapata uelewa wa nyaraka zote muhimu zinazoihusu kampuni ikiwa ni pamoja na  mpango wa biashara, mikakati, mkataba wa wanahisa na kanuni za kampuni.

“Pia, wanawajibika kufahamu masuala na mwenendo wa biashara na uchumi duniani. Azimio lingine ni ofisi ya Msajili wa Hazina kuwa na utaratibu wa kufanya mafunzo ya awali kwa wajumbe mara wanapoteuliwa, pamoja na utaratibu huo kutakuwa na Kikao Kazi kila mwaka cha pamoja na vikao vya Kisekta,” amesema Nnko.