RC Homera asimamisha kazi saba, Takukuru kuchunguza upotevu Sh500 milioni

Friday June 11 2021
rc pic
By Hawa Mathias

Kyela. Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera ameagiza kusimamishwa kazi kwa watendaji saba wa halmashauri ya Wilaya ya Kyela na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ifuatilie Sh500 milioni ambazo hazijaingizwa kwenye mfumo wa Serikali.

Homera ametoa maagizo hayo jana, wakati wa ziara yake ya kujitambulisha kwa watumishi na watendaji wa Serikali na kumhoji mtunza hazina wa halmashauri ya Kyela, Patrick Msafi kueleza sababu za fedha hizo kuonyesha ziko kwenye halmashauri lakini kwenye mfumo hakuna.

“Polisi na Takukuru nawaagiza watafuteni popote walipo watendaji hao saba, wawekwe ndani na pesa hizo zirejeshwe kabla ya Juni 25, mwaka huu kwa sababu haivumiliki fedha zipo mikononi mwa watu kwenye mifumo hakuna,” alisema.

Alisema licha ya Halmashauri kufanya vizuri kwenye makusanyo kwa asilimia 98, lakini suala la pesa kutoingia kwenye mifumo halikubaliki, waliohusika wote wasakwe, fedha zirudishwe.

“Sijaja hapa kumfukuza mtu kazi, bali turekebishane tu hizo ni pesa za umma na Serikali inahitaji kuona pesa zinaingia kwenye mifumo na si mifukoni,” alisema.

Advertisement