Sababu za Albert Chalamila kutoswa

Muktasari:

  • Rais Samia Suluhu Hassan ametengua uteuzi wa mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Albert Chalamila ikiwa ni siku 28 tangu kiongozi huyo alipohamishiwa mkoani humo akitokea Mbeya.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ametengua uteuzi wa mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Albert Chalamila ikiwa ni siku 28 tangu kiongozi huyo alipohamishiwa mkoani humo akitokea Mbeya.

Chalamila aliteuliwa kwa mara ya kwanza kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya na Rais wa awamu ya tano, hayati John Magufuli, Julai 29, 2018 akichukua nafasi ya Amos Makalla, ambaye wakati huo alihamishiwa Katavi.

Mei 15, Rais Samia alifanya mabadiliko ya wakuu wa mikoa na kumhamisha Chalamila kutoka Mbeya kwenda Mwanza akichukua nafasi ya John Mongela ambaye amehamishiwa Arusha.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Jaffar Haniu, Rais Samia amemhamisha Mkuu wa Mkoa wa Mara, Robert Gabriel kwenda Mwanza akichukua nafasi ya Chalamila.

Taarifa hiyo inabainisha kuwa Rais Samia amemhamisha pia Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Ally Hapi kwenda Mara akichukua nafasi ya Gabriel huku akimteua Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, Balozi Batilda Burian kuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora.

“Zuwena Jiri ambaye ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Simanjiro ameteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga kuchukua nafasi ya Batilda Burian,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo ya Ikulu.

Chalamila naye ameingia kwenye orodha ya wakuu wa mikoa ya kanda ya ziwa ambao uteuzi wao ulitenguliwa ndani ya muda mfupi.

Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anne Kilango Malecela ndiye anayeshikilia rekodi ya kuwa mkuu wa mkoa wa kwanza wa kanda hiyo uteuzi wake kutenguliwa.

Uteuzi wa Kilango utenguliwa na hayati Magufuli Aprili 11, 2016 ikiwa ni siku 30 pekee tangu alipoteuliwa Machi 13, 2016.

Magessa Mulongo, aliyekuwa mkuu wa Mkoa wa Mara naye uteuzi wake ulitenguliwa na hayati Magufuli Juni 27, 2016. Mulongo alikuwa mkuu wa Mkoa wa Mwanza alikohamishiwa kutoka Arusha kabla ya kuhamishiwa Mara.

Licha ya kwamba taarifa ya Ikulu jana haikueleza sababu za kutenguliwa kwa Chalamila, kauli tata za kiongozi huyo zinatajwa kuwa sababu ya kutenguliwa kwake kwa sababu alipingana na agizo la Rais Samia.

Aprili 6 wakati wa hafla ya kuwaapisha makatibu wakuu, Rais Samia alisema viongozi wa kitaifa wakikutana na mabango katika ziara zao, atawaondoa kazini mkurugenzi wa halmashauri na mkuu wa wilaya husika. Hata hivyo, mapema wiki hii wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ziara ya Rais Samia mkoani Mwanza, Chalamila aliwahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kumpokea kiongozi huyo wakiwa na mabango mengi yaliyoandikwa chochote.

“Nachukua nafasi hii kwenu waandishi wa habari, kuwakaribisha wananchi wote tarehe 13, 14 na 15, tuweze kumpokea Rais kwa mabango mengi, ya aina yoyote ile hata kama ataandika tusi aandike, yoyote yale,” alisema Chalamila.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Paul Luisilie alisema Rais Samia ndiye anajua sababu ya kutengua uteuzi wa Chalamila, hata hivyo, uamuzi huo unahusishwa na kauli ya Chalamila ya kuhamasisha wananchi kumpokea Rais kwa mabango hata ya matusi.

“Nadhani hii ni hamasa ambayo imepitiliza kwamba wananchi waende na mabango hata yenye matusi. Hii ndiyo imerahisisha utumbuaji wake, kuna mambo mengi yalikuwa yanaendelea huko nyuma, lakini aliwapa muda,” alisema Dk Luisilie.

Mwanazuoni huyo alibainisha kwamba Chalamila ni mchangamfu katika hotuba zake, sasa uchangamfu huo umepitiliza na kusababisha kupoteza nafasi yake kama kiongozi kijana aliyeaminiwa. Nyongeza na Peter Saramba